Habari

Bajeti ya Zanzibar hadharani

SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) imewasilisha bajeti yake kwa mwaka 2016/2017, huku ikidhamiria kuongeza mishahara ya wafanyakazi na kupunguza kodi.

Baraza la Wawakilishi, Waziri wa Fedha, Dk. Khalid Salum Mohammed, alisema pamoja na dhamira ya serikali ya kubana matumizi, pia imekusudia kutekeleza ahadi yake ya kuimarisha maslahi ya wafanyakazi, hususan wa kipato cha chini.

Alisema licha ya kuwawezesha kumudu gharama za maisha, hatua hiyo pia itasaidia kuhamasika kufanya kazi kwa bidii zadi.

“Bajeti hii inakusudia kutekeleza ahadi ya Mheshimiwa Rais Dk. Ali Mohamed Shein, ya kupandisha kima cha chini cha mshahara kutoka Sh. 150,000 hadi Sh. 300,000, katika mwaka wake wa kwanza wa kipindi hiki cha pili cha uongozi wake,” alisema.

Alisema kuwa serikali imesikia kilio cha wafanyakazi cha kupunguziwa kodi katika kipato cha mshahara na kuweka sawa viwango vyake na Tanzania Bara.

Pamoja na kufanya marekebisho ya mishahara, alisema serikali itafanya marekebisho ya kodi ya mapato kwa kupunguza kiwango wanachotozwa watu wa kipato cha chini kutoka asilimia 13 hadi asilimia tisa.

Alisema kuwa lengo la hatua hiyo ni kuimarisha kipato cha wafanyakazi wa kima cha chini kwa kumbakishia kipato zaidi ili kukidhi mahitaji ya maisha.

Aidha, alisema ili kukidhi mahitaji ya kijamii, lengo kuu la bajeti ni kujenga jamii iliyoelimika, yenye siha na yenye uhakika wa chakula, uwezo wa kiuchumi na inayothamini na kufuata misingi ya utawala bora.

Akizungumzia kuhusu bajeti iliyopita, alisema ukusanyaji wa mapato katika kipindi hicho umeathiriwa zaidi na mwenendo usioridhisha na mapato ya nje, uliosababishwa zaidi na kuendelea kusuasua kwa utekelezaji wa miradi mikubwa kama vile ujenzi wa jengo jipya la abiria la Uwanja wa Ndege wa Abeid Amani Karume, ujenzi wa barabara ya kati na mradi wa kuimarisha usalama.

“Mwenendo wa mapato umeathiri utekelezaji wa bajeti kimatumizi. Hadi Machi 31, mwaka huu, matumizi halisi yalifikia Sh. bilioni 352.9 yakijumuisha Sh. bilioni 298.4 za matumizi yatokanayo na mapato ya ndani na Sh. bilioni 54.5, matumizi yatokanayo na mapato ya nje,” alisema.

Aidha alisema kuwa bajeti hiyo inakusudia kubana matumizi na kuimarisha usimamizi wa mapato ili kuhakikisha fedha zinazotumika zinaleta tija kubwa zaidi.

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iatarajia kutumia Sh. bilioni 841.5 ikiwa Sh. bilioni 445.6 kwa matumizi ya kawaida na Sh. bilioni 395.9 kwa ajili ya maendeleo, huku ikilenga kukusanya Shilingi bilioni 482.4 kutoka katika vyanzo vya ndani na Sh. bilioni 93.3 kutoka kwa washirika wa maendeleo.

Chanzo: Nipashe

Share: