Habari

BALOZI IDDI AWATAKA VIJANA KUJENGA TABIA YAKENDA MASOMO YA SAYANSI

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ametoa wito kwa Jamii Nchini kuwaasa Vijana wao kupenda masomo ya Sayansi ili kuondosha upungufu wa Wataalamu katika fani hiyo unaolikumba Taifa.

 

Wito huo ameutoa katika mahafali ya kumi ya Chuo Kikuu cha Kumbu kumbu ya Hubert Kairuki { HKMU } zilizofanyika katika ukumbi wa Diamond Jubilee Mjini Dar es salam.

 

Balozi Seif alisema moja ya changamoto kubwa katika Taifa hivi sasa ni kwa wanafunzi wengi siku hizi kupenda masomo ya sanaa kama vile uhasibu, sheria na biashara kwa madai ya kupata maslahi ya haraka.

 

Alisema bila ya kuwa na masomo ya sayansi Taifa halitaweza kuwa na wataalamu na Nchi itashinwa kumudu kupiga hatua za haraka za maendeleo endapo itakosa wataalamu wa fani zote.

 

Balozi Seif alielezea matumaini yake kuwa wahitimu hao 114 wa Sekta ya Afya katika ngazi ya Udaktari, Uuguzi, Ushauri nasaha pamoja na MD’s watakuwa mabalozi wa kuhamasisha jamii kupenda masomo ya sayansi hasa ikizingatiwa kwamba karne hii ni ya sayansi na teknolojia.

 

“ Hatuwezi kuwa na Madaktari, Wauguzi au wahandisi bila ya kuwa na msingi mkubwa na imara wa masomo ya sayansi”.Alisisitiza Balozi Seif.

 

Aliwataka wazazi kuendelea kuisaidia Serikali katika kuchangia gharama za elimu kwa watoto licha ya kuwepo wenye uwezo wa kuwalipia watoto wao lakini wanasusa kwa kutegemea mikopo inayotolewa na Serikali.

 

Balozi Seif alisema tabia hiyo ya baadhi ya wazazi hao si haki na ni dhambi inayowanyima fursa watoto wasiokuwa na uwezo wa kuendelea na masomo yao ya juu ambao hutegemea kupata mikopo hiyo.

 

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alizipongeza juhudi za Taasisi binafsi katika kuchangia maendeleo ya elimu hapa Tanzania na kukitolea mfano chuo Kikuu cha Kumbu kumbu ya Hubert Kairuki ambacho mchango wake unatambuliwa na kuthaminiwa na Serikali.

 

Aliwaomba Watanzania wengine waliojaliwa uwezo kuiga mfano huo kwa kuisaidia kusomesha wataalamu katika Nyanja mbali mbali na hatimae kuliwezesha Taifa kusonga mbele katika maendeleo.

 

“ Profesa Kairuki alikuwa na uwezo wa kufungua Hoteli au kuwekeza katika sehemu nyengine za Biashara lakini hakufanya hivyo kwa kuwa alikuwa mzalendo wa kweli aliyekerwa na uhaba wa madaktari na wauguzi. Ndipo alipoamua kuanzisha hospitali na baadaye chuo kikuu ili kupunguza uhaba wa wataalamu wa afya nchini”.Alifafanua Balozi Seif.

 

Akizungumzia tatizo la migogoro mingi iliyowahi kujichomoza katika baadhi ya vyuo vikuu hapa Nchini Balozi Seif aliupongeza Uongozi wa Chuo Kikuu cha Kumbu kumbu ya Hubert Kairuki kwa kuepusha kutotokea kwa migogoro chuoni hapo.

 

Balozi Seif alivishawishi vyuo vikuu vyengine nchini kuiga mfano huo wa chuo kikuu cha Kumbu kumbu ya Hubert Kairuki.

 

Alieleza kuwa inawezekana kwa baadhi ya wakati kukatokea migongano baina ya uongozi wa chuo Vikuu na wanafunzi lakini hitilafu hizo zinaweza kutafutiwa ufumbuzi kwa kupitia meza ya majadiliano badala ya kuingia bara barani kwa maandamano na kugomea masomo.

 

Akigusia mmong’onyoko wa maadili katika taaluma unaoonekana kulikumba Taifa hivi sasa Balozi Seif aliwaasa wahitimu hao kuzingatia taaluma , Miiko na wawe weledi katika utendaji wa kazi zao.

 

Alisema Jamii ya Watanzania inatarajia kuwategemea katika kuwapatia huduma bora na iliyosheheni uadilifu, uaminifu pamoja na utiifu.

 

Balozi Seif alieleza kwamba ni aibu na ni kosa la jinai kwa daktari , muuguzi au mtu mwengine ye yote yule tena msomi kuomba rushwa au kujihusisha na vitendo vya ufisadi.

 

Mapema Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Kumbu kumbu ya Hubert Kairuki Profesa Keto Mshigeni alisema chuo hicho kimepata mafanikio makubwa tokea kuanzishwa kwake Miaka kumi iliyopita na kuzalisha wahitimu 919 kati yao asilimia 68% wakiwa wanawake.

 

Profesa Keto alisema idadi ya wanafunzi walioandikishwa mwaka huu wa masomo imefikia wanafunzi wapya 245 ikiwa ni ongezeko la wanafunzi 56 ambao wanatoka katika Mataifa ya Malawi, Kenya,Zambia, Botswana, Namibia, Marekani na wenyeji Tanzania.

 

Makamu Mkuu huyo wa chuo Kikuu cha Kumbu kumbu ya Hubert Kairuki Profesa Keto Mshigeni alieleza changamoto nyingi zinazokikabilia chuo hicho kuwa zaidi ni uhaba wa wahisani wenye kuelewa umuhimu wa Taaluma ya juu katika Maendeleo ya Taifa na Wananchi wake.

 

Akimkaribisha Mgeni rasmi Balozi Seif Ali Iddi Mwenyekiti wa Bodi ya Mtandao wa Elimu Mikocheni ambae pia ni mwanzilishi Mwenza wa Chuo hicho Mama Kokushibila Kairuki aliziponeza juhudi za Viongozi na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar za kuunga mkono chuo hicho.

 

Mama Kokushibila Kairuki alizitaja baadhi ya juhudi hizo kuwa ni pamoja na michango iliyokwenda sambamba na ushawishi wa wanafunzi wa Zanzibar kuelekezwa kupata taaluma ya Afya katika Chuo hicho.

 

Chuo Kikuu cha Kumbu kumbu ya Hubert Kairuki Kiliyopo Mjini Dar es salaam kimefanikiwa kushika nafasi ya 49 katika vyuo vikuu Barani Afrika na nafasi ya Pili katika vyuo Vikuu Nchini Tanzania kikitanguliwa na Chuo Kikuu cha Dar es   salaam.

 

Share: