Habari

BALOZI SEIF ALI IDD ADAIWA KUKOSA SIFA

NAIBU Katibu Mkuu wa CUF, Ismail Jussa amemuelezea Makamo wa pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Idd kuwa ni kiongozi aliyepoteza sifa katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa, Zanzibar.

 

Jussa akizumgumza katika mkutano mkubwa wa hadhara wa CUF uliyofanyika jana katika Jimbo la Bububu, alimtaka Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein na Makamo wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharifu Hamad, kulielewa hilo.

 

Aidha, akionekana kukerwa na utendaji wa kiongozi huyo Jussa, alisema Balozi Seif Ali Idd amepoteza sifa za kuwa kiongozi katika Serikali hiyo na utendaji wake wa kazi unaelekea kuwa wa uwakilishi wa Tanganyika:

 

“Sitaki kumung’unya maneno hapa Dk Shein na mwenzako Maalim Seif…Balozi Seif amepoteza sifa ya kuwa kiongozi katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa na wala sitafuni tena maneno huyu ni Balozi mkaazi wa Serikali ya Tanganyika ndani ya Zanzibar huyu sio Makamu wa pili wa Rais wa Zanzibar huyu ni Balozi mkaazi,” alisema na kuongeza:

 

“huyu…huyu…huyu ameletwa hapa kwa lengo maalumu la kuvuruga Serikali ya umoja na kuvuruga umoja wa Wazanzibari…nasema umoja wetu ndio silaha kubwa,” alisema Jussa.

 

Jussa ambaye pia ni Mwakilishi wa Mji Mkongwe, aliwatahadharisha wananchi wa Zanzibar, na mitego ya baadhi ya viongozi wa CCM kama Balozi Seif Ali Idd:

 

“Tukiingia katika mtego tutakuwa tumeingia katika mtego wa Balozi Seif Idd, nataka kumhakikishia Balozi Seif Ali Idd kwamba sisi hata siku moja hatutaondoka katika mstari huu ataondoka yeye na vibaraka vyao,” alisema Jussa.

 

Kuhusu kauli yake hiyo Naibu Katibu Mkuu huyo wa CUF Zanzibar, alisema ng’oo hawezi kubadilisha matamshi yake dhidi ya kiongozi huyo mwenye dhamana ya shughuli za kila siku za Serikali na Baraza la Wawakilishi:

 

“Ati Waziri wa nchi Mohamed Aboud, anasema tumtake radhi Balozi Seif Idd…nasema hatumtaki radhi hadi kiama lakini mimi kwa niaba ya Wazanzibari wote namwambia Balozi Seif Ali Idd jiuzulu,” alisisistiza Jussa.

 

Alisema Wawakilishi wa CUF, ndani ya Baraza la Wawakilishi, hawatamtambua Mwakilishi huyo mpya wa Jimbo la Bububu, kutoka CCM, kama Mwakilishi halali wa kuchaguliwa na wananchi:

 

“Jukumu letu ni kuirejesha Zanzibar katika mamlaka kamili, nasema na sisi Wajumbe wa CUF ndani ya Baraza la wawakilishi hatutamtambua kama ni mwakilishi wa jimbo la BUBUBU na hatutampa mashirikiano kama ni mwakilishi halali bali tutamtambua Issa Khamis Issa kuwa ndio Mwakilishi halali wa Jimbo hili la Bububu”, alisema Jussa..

Share: