Habari

Balozi Seif atembelea jumba la treni Darajani

Balozi Seif akizungumza na maofisa wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar (ZSSF) na baadhi ya maofisa wa serikali alipofanya ziara ya kukagua hatua za mwisho za matengenezo ya Jumba la Treni Darajani linalotarajiwa kufunguliwa mwezi ujao.

Othman Khamis – OMPR
Ijumaa, Julai 20, 2018

MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi ametaka umuhimu wa kuzingatia utunzaji wa usafi wa mazingira katika eneo la Jumba la Biashara Darajani Unguja maarufu ‘Jumba la Treni Darajani’ ambalo ndilo sura halisi ya muonekano wa mji huo.

Alikuwa akizungumza Ijumaa, Julai 20, 2018 baada ya ziara fupi ya kukagua maeneo mbalimbali ya ndani na nje ya jumba la treni Darajani, Unguja linalotarajiwa kufunguliwa mwezi ujao na kuanza tena shughuli za biashra baada ya matengenezo yote kamilika.

Akitoa shukrani zake kwa Uongozi wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar (ZSSF) na Kampuni ya Uhandisi ya ujenzi huo CRJ, Balozi Seif alitahadharisha umuhimu wa kutunzwa kwa jengo hilo katika kuzingatia usafi wa mazingira katika eneo hilo.

Alisema serikali kupitia taasisi zake imekuwa ikiimarisha matengenezo ya majengo yake kwa lengo la kuwarahisisha wananchi waliowengi mjini na mashamba kupata huduma muhimu zikiwemo za biashara.

Aliwasihi wafanyabiashara watakaobahatika kupata nafasi katika jumba hilo kuzingatia usafi pamoja na kulipa kodi kwa wakati na kuutaka uongozi wa ZSSF kupanga utaratibu utakaowapa fursa nzuri wafanyabiashara hao kulipa kodi kila baada ya miezi sita badala ya utaratibu wa awali wa kulipa kodi kwa mwaka.

Hata hivyo, Balozi Seif aliitaka ZSSF wasiogope kuvunja mikataba kwa wafanyabiashara watakaokiuka masharti yaliyowekwa kwenye mikataba hiyo.

Huduma za biashara katika jumba la treni ambalo lipo katikati ya kitovu cha biashara Zanzibar, zinatarajiwa kuanza rasmi mwezi ujao wa Agosti, pamoja na kufanya mchujo wa majina ya wafanyabiashara walioomba kupatiwa milango ya kufungua biashara.

Matengenezo ya jengo hilo yanasimamiwa na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar (ZSSF) na mkandarasi ni Kampuni ya Uhandisi ya CRJ kutoka nchini China.

Mapema akimweleza Balaozi Seif kuhusu matengenezo ya jumba hilo, Kaimu Meneja Mipango wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar (ZSSF), Abdulaziz Ibrahim Iddi alisema ushauri uliyotolewa na Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) wa kutaka mbao maalumu zinazofaa kutumika kwa milango ndiyo ulioongeza muda na kuchelewesha kukamilika kwa wakati.

Alisema kuwa mbao za milango inayokusudiwa kufungwa ndani ya maduka yaliyomo kwenye jumba hilo zimeshawasili na tayari ziko bandarini na kazi ya kuzifunga katika maduka hayo inatarajiwa kuanza wakati wowote.

Abdulaziz alisema jumba hilo litakuwa na milango ya maduka 58 ambayo kati yake matano yatarejeshwa kwa wamiliki wake wa awali waliokuwa wakifanya biashara kabla ya matengenezo hayo kwa mujibu wa mikataba na milango ya maduka 53 yaliyobaki ndiyo yaliyotangazwa kukodishwa kwa wafanyabiashara waliojitokeza kuomba.

Kaimu Meneja huyo alisema kwamba katika jumba hilo zipo nyumba 10 za kuishi watu, sehemu ya kufanyia mazoezi ya viungo (GYM), mkahawa pamoja na supermarket. Alisema: “Nafasi zote hizo zitakodishwa kwa wananchi.”

Lakini alisema kwamba katika mchujo wa majina wa wafanyabiashara waliomba kupatiwa nafasi, kipaumbele cha kwanza kitatolewa kwa kuzingatia wafanyabiashara waliyokuwa wakifanyabiashara zao hapo kabla ya matengenezo hayo.

Kadhalika, Abdulaziz alisema kuwa kwa wafanyabiashara watakaobahatika kupata milango ya maduka watatakiwa kufunguwa biashara zao siku rasmi ya ufunguzi wa jumba hilo na papo hapo huduma kwa wateja zianze.

Alisema: “Tunataka siku ya ufunguzi wa jumba hili milango yote iwe wazi na huduma za biashara ziwe tayari kuanza kwa kuwauzia wateja mahitaji yao, hii itarudisha mandhari na sura hali ya jumba la treni ambalo ni la kihistoria.”

Jumba la treni la Darajani ambalo ni maarufu kwa shughuli za biashara linakadiriwa kuzidi karne mbili kabla ya kufanyiwa matengenzo lilikuwa linakabiliwa na hali mbaya ya uchakavu kiasi kuweza kuhatarisha maisha ya watu.

Share: