Habari

Balozi Seif Atowa ufafanuzi Kuhusiana na Taarifa Zilizotolewa na Baadhi ya Vyombo vya Habari.

Na Othman Khamis OMPR.
Wanahabari wanapaswa kuwa makini zaidi katika utoaji wa Habari zao hasa kipindi hichi ambacho Zanzibar inaendelea kutafuta njia muwafaka ya hatma yake ya baadaye kufuatia Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar { ZEC } kufuta Uchaguzi Mkuu wa Mwezi Oktoba mwaka huu baada ya kubaini hitilafu kadhaa katika zoezi zima la uchaguzi.
Nasaha hizo zimetolewa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi hapo Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar alipotoa ufafanuzi wa kina juu ya taarifa zilizotolewa na baadhi ya vyombo vya Habari vikieleza kuwa Viongozi wanaokutana kujadili suala hilo wamekubaliana kurudiwa kwa uchaguzi huo.

Alisema Kalamu za waandishi wa Habari kwa sasa ni vyema zikawaelekeza na kuwaongoza Wananchi kujihusisha na harakati zao za kimaisha badala ya kuwaendeleza katika wimbi la mizozano na mifarakano inayoweza kuamsha hamasa.

Balozi Seif akiongea na Redio ya Kiswahili ya Kimataifa ya Ufaransa { RFI } juzi alichokisema kuwaeleza wanahabari hao ni kwamba Chama cha Mapinduzi { CCM } pekee ndicho kilichotamka na kuthibitisha kuwa kiko tayari kurejea uchaguzi huo endapo utapangwa upya.

“ Nilichokieleza juzi ni kwamba CCM peeke ndio Tuliothibitisha na kukubali kurejea uchaguzi endepo utapangwa tena na hili tunaloendelea nalo la vikao na wenzetu bado tunajadiliana na maamuzi ya pamoja yatatolewa kwa Waandishi hapo baadaye “. Alisema Balozi Seif.

Alisema hadi sasa hakuna chombo chochote cha Habari ndani na nje ya Nchi kilichoitwa au kupewa Habari za mazungumzo yanayoendelea kati ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dr. Ali Mohammed Shein na Katibu Mkuu wa CUF ambae pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamadi kwa kuwashirikisha Marais wastaafu wa Zanzibar.

Balozi Seif alisema utaratibu maalum utaandaliwa wa kutolewa taarifa rasmi kwa vyombo vyote vya Habari ili ziwafikie Wananchi wote mara baada ya kukamilika kwa mazungumzo hayo na makubaliano yatakayofikiwa baina ya pande hizo mbili.

Aliwathibitishia Wananchi na wageni kwamba hali ya Zanzibar bado iko shwari na salama na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na ile ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia vyombo vyake vya Dola vitasiamia ipasavyo hali hiyo.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwaomba Wananchi wabakie kuwa watulivu, wastahamilivu na kuendeleza Umoja na mshikamano utakaosaidia kulivua Taifa hili katika shari inayoweza kuepukwa.

Share: