Habari

Barua ya wazi kwa Balozi Ali Karume na Maalim Seif Sharrif.

Wapenzi Waheshimiwa.

Naomba nichukue nafasi hii kuwatakia afya njema nyote wawili pamoja na familia zenu. Baada ya salaam ni vema nikaja kwenye lengo kuu la barua yangu kwenu, moja kwa moja bila kuwapotezea muda wenu adhimu mabwana waheshimiwa. Kutokana na hali halisi ilivyo ya visiwa vyetu ni wazi nyote wawili mnafahamu kuwa Zanzibar sio nchi wala hatuna kujitawala au kujiamulia wenyewe kitu chochote kinachohusu ardhi au watu wetu, juu ya kujivunia kote mapinduzi yetu ya january 1964, bado sisi tuna tawaliwa na Tanganyika tangu marehemu Baba yako bwana Ali Karume alipoamua tuungane nao April 26 1964 baada ya mazungumzo mafupi na marehemu Nyerere.

Historia inatufundisha mengi mema aliyoyafanya mzee wetu marehemu Karume baba wa taifa letu la watu wa Zanzibar. Nia yake kuhusu muungano huu ilikuwa safi na yenye kueleweka, lakini hatuwezi kusema wala kujua sisi Wazanzibari kuhusu nia au sababu za kuutaka Muungano huu dhidi yetu ndani ya nafsi ya mwalimu nyerere, wakati huo au hata baadae. Lakini historia hiyo hiyo kwa sasa imetuwekea wazi nia, dhulma, unyanyasaji, kutawaliwa na kila aina ya madhila tunayofanyiwa na tunaowaita ndugu zetu wa Tanganyika, ambao bila soni hivi sasa hata katika bunge la jambhuri ya muungano, wanasema wazi kuwa sisi tunadai nini zaidi kwa kuwa udogo wetu umegeuzwa kuwa ndio kigezo cha kupewa hadhi ya moja ya mikoa ya Tanganyika, na sio mshirika wa Taifa hili la Tanzania, ambalo bila Zanzibar itabidi waitafute au waifufue Tanganyika na ndio itakuwa mwisho wa Tanzania.

Mola wetu aliyeumba mbingu, watu, bahari, pamoja na kila tunavyovijua na tusivyovijua mara zote huweka mkono wake katika kila jambo analolitaka. Maalim Seif kama utakumbuka niliwahi kukuomba karibu miaka 20 na kitu iliyopita kuwa ni vema ukaanza kumtafuta mrithi wako ili aje akusaide kuliongoza jahazi hili la kuikomboa Zanzibar mapema. Nilichokihofia muda wote wa uongozi wako ni ile dhana ya baada ya wewe kupumzika CUF inaweza ikaporomoka au ukaondoka nayo, kwa kuwa hukuwawekea mfumo mzuri wa kukabidhiana madaraka. Ni wazi wafuasi karibu wote wa chama chako ni watu wanokuamini siku zote.

Kutokana na hali ilivyo ya kisiasa hapa visiwani kwa sasa, CCM tayari Zanzibar wana mtayarisha mtu wa kuja kukikalia kiti cha urais baada dk Sheni kuondoka. Tanganyika nao hasa Magufuli, yeye sie Kikwete, kwa maana hiyo yule ambae ataweza kuona kuwa anaweza kumtumia kuitawala Zanzibar kwa niaba yake, huyo ndie atakaempa Urais na hakuna wa kumzuwia.

Wagombea ndani ya ccm Zanzibar ni wengi mno, la kushangaza sana ni kuwa waungwana hawa wanadhani kuwa maamuzi yao ndio yatakayozingatiwa Dodoma. Hawajawahi kuangalia huko nyuma nani waliemtaka wao aliwahi au alipitishwa Dodoma? Wengine wanaoyajua haya tayari wameshaanza kutumiwa na Magufuli, na wana peleka fitina mbili tatu dhidi ya wenzao, ili wao waaminike zaidi. Kwa kuzitumia asili zao, Bwana Ali Karume, Zanzibar inahitaji mkombozi mwenye ujasiri, sura, uchungu na asieogopa kama ya mzee wako.

Nimepata habari kuwa ccm hawana nia wala azma ya kukukubali wewe kuwa mgombea. Wanaelewa uwezo wako huo hawana mashaka nao hata kidogo, wengine wanaongelea kuhusu unywaji wa sharbati, lakini hata hilo linaweza kudhibitiwa, kwani marehemu Aboud Jumbe na Nyerere wote walikuwa hawanywi tongwa peke yake na waliongoza bila tatizo.

Ninachotaka kusema hapa kwenu waheshimiwa, huu sio wakati wa kuangalia vyama vyenu au itikadi zenu, ni lazima Zanzibar muionee uchungu na muiweke mbele ili watu wenu wanusurike na kutawaliwa. Ni lazima mfanye mapinduzi ya kiitikadi na kimitazamo kwa mapana yake, katika siasa hakuna adui wa kudumu, wala rafiki wa maisha. Siku zote kuna kuwa na ‘rafiki wa lengo moja’ awe wa muda maalum au kudumu, hilo hutegemea mahitaji ya wakati mlionao, na mnako elekea.

Ombi langu kwenu mimi nikiwa mwana ccm wa kadi ninae amini kuwa Zanzibar ndio baba na ndie mama yetu sio vyama. Maalim Seif sasa umefika wakati wa wewe binafsi kuwasilianana na kuanzisha mazungumzo ya kumtaka Balozi Karume endapo atakataliwa kugombea kwa tiketi ya CCM, kitu ambacho nina uhakika nacho, Basi hiyo itakuwa nafasi adimu na adhimu sana kwetu kupatikana, na hatuna budi sisi wazanzibari kumchukua Balozi huyu na kumkubali agombee kwa tiketi ya CUF.

Hili sio jambo geni tafadhalini msishituke waungwana, katika siasa haya yanafanyika duniani kote. Nani alidhani au kujua kuwa Lowassa atagombea kwa tiketi ya chadema? Mbowe aliutumia mfumo huu huu ambao wengine hapa leo wanaweza kuubeza, matokeo yake ccm ilishindwa urais kwa mara ya kwanza tangu kuanzishwa kwa vyama vingi, lakini wakamtangaza Magufuli kama kawaida yetu. Muhimu hapa ni kuweka mgombea ambae ataleta ushawishi au msuguano wa hali ya juu na asie ogopa kutuamrisha kuingia barabarani kuidai Zanzibar baada ya kuporwa ushindi, kwa sababu ccm watarudia mfumo huu siku zote kama wapinzani hawatokuwa tayari kufanya mabadiliko ya kifikra na kiuongozi. Mimi namjua Balozi Karume vizuri, kama kuna waliokuwa hawakuwahi kumjua marehemu mzee Karume, basi Mola awape fursa ya kumjua mwanawe.

Balozi Karume ccm kimekuwa au kimegeuzwa chama cha kibaguzi hili unalijua. Hivi sasa hata watoto wako binafsi  na hata wale wa kaka yako mliowazaa pamoja na wajukuu zenu hao tuna jina tunawaita “machotara”. Marehemu baba yenu alitukomboa na alitutaka tuchanganye damu ili tuondoe UBAGUZI sasa unarudishwa mchana kweupe na nyie mnaona. Haiwezekani mvumilie haya wakati uwezo bado mnao wa kuirudishia Zanzibar heshima yake, ili vizazi vyetu vyote viishi kwa amani na kupendana kama walivyofanya wazee wetu na sisi wenyewe.

Maalim Seif nafahamu hili sio ombi rahisi. Nafahamu pia kuwa una watu au kuna mtu unae katika nafsi ambae ameitumikia cuf uhai wao/wake wote, na wana uwezo wa kutosha kushika usukani pale utakapoona wakti umefika. Lakini itakuwa haina maana kumuweka mtu huyo ikiwa kiti tutakikosa, lengo sio kuridhishana kwa sasa lengo ni kukiondoa ccm madarakani kwa mbinu yoyote.

Ulipofanya mazungumzo na kaka yake balozi Karume yaani rais msataafu Amani Karume na mkafanikiwa kuisimika serekali ya umoja wa kitaifa, haikuwa kazi rahisi vile vile. Lakini nia zenu safi kwa visiwa hivi na uungwana wenu, Mola ALIWABARIKI na mkaleta neema ndani ya shamba letu hili la mikarafuu. Mliweka itikadi zenu pembeni na mkaangalia maslahi ya Zanzibar na watu wake mbele, sio ya cuf wala ccm, sasa nini kitawashinda kwa sasa?

 

Naelewa vema kuwa barua hii itasomwa sehemu nyingi sana na wengi wanaweza hata kushtuka hao sio wana siasa, kwa kuwa kama nilivyo nukuu awali kuwa hili sio jambo geni. Pia nimewapima na kuwaangalia wagombea karibu wote wa ccm lakini najikuta narudi kwa balozi Karume, mikakati ndio ushindi sio wingi wa watu peke yake. Siku zote Maalim una umati nyuma yako wa kutosha kukuhamishia ikulu, lakini bado uko mbweni kabla ya hapo mtoni, ni wazi sasa wakati umefika wa kuzitumia siasa kama hizi. Mimi huziita za “ki-odinga odinga” kwa sababu wenzetu wa Kenya huwa hawaoni tabu kuungana hata dakika za mwisho mwisho muhimu waingie IKULU.

Nina uhakika barua hii inaweza kuwa kisingizio cha ccm kumkosesha ugombea  balozi Karume, lakini kama ninavyosema kisingizio kwa sababu wao wamesha amua ndio maana wameanza kwa kumteremsha cheo na kumpa wizara ya michezo, akachee huko mbali. Tayari wameshaona kuwa huyu ni tishio na ni mtu asie aminika katika kuutukuza Muungano, chungwa huwa halianguki mbali na mchungwa. Aliyokuja nayo kaka yake bado hawajamsamehe juu uaminifu na mapenzi yake kwa Zanziar. Wahafidhina wanaoamini Uafrika wao ndio kigezo cha kuwabagua wengine hawako tayari kumtafuta kiongozi mwingine ndani ya nyumba ya Karume.

Haya ni maajabu kwa kiasi fulani, mkombozi wa visiwa hivi aliye ongoza Mapinduzi tunamkumbuka siku zote lakini hakuna moja tunalo lifanya linalo fanana na yale aliyoyasimamia katika uhai wake. Hivi sasa wananyimwa Wazanzibari pasi za kusafiria {passport] na wanaitwa wahamiaji wasiohamishika. Wengi au wote ni  Wazanzibari wenye asili ya UARABU, UNGAZIJA, USHIHIRI, UHINDI au mchanganyiko wowote unaoonekana kuwa hauna maslahi kwa ccm yaani ni wapinzani. Sasa hivi kweli leo Zanzibar tunarudi kule kule tulikotoka salama, hawa wote wamezaliwa hapa ndio maana wanaitwa hawahamishiki lakini hawawezi kuwa raia, kwa sababu gani? Kama sio ubaguzi?

Natumai waheshimiwa mtanielewa, muda tunao inshaalah msifanye haraka kukutaka kwa sasa. Hili ni wazo nawapa mlifanyie kazi kwa manufaa yetu sote. Safari hii kitaeleweka ikiwa mtajua kuzitumia karata mlizo nazo mikononi vizuri na kuacha malumbano yasio na tija.

Tanganyika wana tumia kila mbinu kukuvurugeni ikiwemo kumnunua Lipumba, wabunge, madiwani na wale walioingizwa bungeni kwa amri ya mahakama na tume ya uchaguzi. Huu ni mpango endelevu kuelekea 2020, sasa kwa nini na nyie msifanye ya kwenu ili muinusuru ZANZIBAR, HIVI NI VITA MSICHAGUE SILAHA.

Asanteni.

Nawashukuru kwa kunisikiliza.

Share: