Habari

BARUA YA WAZI KWA RAIS WA VISIWA VYA ZANZIBAR/AMIRI JESHI WA VIKOSI VYA SMZ.

MHESHIMIWA RAIS WA VISIWA VYA ZANZIBAR,

AMIRI JESHI MKUU WA VIKOSI VYA ULINZI VYA SMZ,

MAKAMO MWENYEKITI WA CCM TANZANIA/ZANZIBAR,

DAKTARI, AL-HAJ SHEIKH ALI MOHAMMED SHEIN.

MPENDWA NDUGU YETU, ASALLAM ALEYKUM.

Baada ya kuchukua muda wa kutosha na kutafakari hali halisi ya visiwa vyetu, kwa unyenyekevu, heshima na taadhima kubwa, niruhusu nikutumie warka huu mfupi kwa nia safi kabisa, kwa sababu usalama  wako binafsi, pamoja na wetu sote Wazanzibari, na  wa visiwa vyetu uko hatarini kutoweka sasa na kila siku zikisonga mbele, hasa ikiwa sisi wenyewe kwa wenyewe tutaendelea kutofautiana, na kuziendekeza tofauti zetu za kisiasa hizi za vyama vingi huku visiwa vinazama au kuchukiwa mchana kweupe.

Ni kweli tuna matatizo ya ndani katika visiwa vyetu, ambayo mengine au mengi tumeyarithi toka enzi za wakoloni, na bado tunayatumia matatizo, au tofauti hizo kama vigenzo vya kuendeleza ugomvi au kutokuelewana kwetu mpaka leo, kwa taadhima tena hekima na utu wako ambao nina uhakika nao, nina kuomba kwa hisani na imani ya dini yetu, huu sio wakati tena wa kuwatafuta maadui baina yetu Wazanzibari, kwa kuwa hatari inayotukabili  ni yetu sote.

Ikiwa sisi bado hatujachoka kushughulikiana, ni wazi kazi inayofanywa miaka yote hii na ndugu zetu wa Tanganyika ya kunyakua na kuzifuta kila alama ya dola ya visiwa hivi tutazidi kuifanya kazi hiyo iwe rahisi mno, sisi tuliungana na ndugu zetu hawa kwa hiari tupu, lakini kwa bahati mbaya kabisa hiari hiyo imegeuzwa kuwa deni na utumwa juu yake, kiasi kinachompelekea Rais mwenzio wa ardhi ya Tanganyika anakuingilia katika mamlaka na madaraka yako, bila kujali mipaka iliyowekwa na katiba zetu zote mbili za taifa hili ambazo nyote mmezilia kiapo kuwa mtaziheshimu sawa sawa.

Huu sio wakati tena wa sisi Wazanzibari kukutambua au kuto kukutambua wewe, iwe rais halali au haramu wa visiwa vyetu, wewe ndie Kiongozi wa visiwa hivi unaetuwakilisha duniani kote, misuguano ya kisiasa hatukuianza sisi katika sayari hii, wala hatutokuwa wa kwanza kuimaliza, mapenzi tuliyonayo baina yetu, ni aibu na fedheha kubwa kwa kizazi chetu kuona bado tunachezewa, kisa siasa, bila ushawishi unaofanywa kwa makusudi na wenzetu, wanaotumia mwanya au udhaifu wetu, ili wao waendelee kunufaika na Muungano huu wa upande mmoja.

CCM au CUF kwa hapa visiwani sisi sote ni Wazanzibari kwanza, hivi vyama isiwe ndio msumari wa mwisho wa kulifunga jeneza ili sote tuteketee, sitaki kurudi nyuma na kuanza kuyafukua makaburi na kumtafuta nani alaumiwe kuhusu Muungano wetu, au aliehusika na kukiuwa chama cha Afro Shirazi kilichotukomboa na utumwa mmoja na kututia katika utumwa mwingine.

Sisi tulipindua au kupinduana kwa maslahi ya watu wetu wote, bila kujali dini zao, rangi zao, asili zao, vyama vyao vya siasa au vile vya jumuia zao vilivyokuwepo kabla ya Mapinduzi. Tulijenga Zanzibar moja, asili moja, nchi moja, utamaduni mmoja na watu wamoja. Zanzibar haikusifika kwa ukarimu wake baada ya Mapinduzi matukufu ya January 12, 1964, sisi ni watu karima tangu enzi na enzi kabla hata wakoloni hawajaja kututawala na kutugeuza watumwa au watu wa tabaka la chini.

Asili yetu hii ya utu ,uungwana na kupendana kwetu na baina ya watu, ndio iliyotufanya tukakubali kirahisi  kuungana na Tanganyika bila kufanya tafakari ya kina. Historia ya wakati huo sasa hatunayo tena kwa maana hiyo hatuwezi kuendelea kuishi au kutumia vigezo visivyokuwepo, hii ni karne ya 21 ambayo nayo ina mitihani yake. Mmoja wapo ni huu wa wewe kusubiriwa siku zote ukiwa safarini nje ya visiwa hivi, tena huku nyuma Rais wa Tanganyika upesi upesi kabla hujarudi huanza kutoa amri zisizo muhusu, kama zile za zima umeme au hili la juzi la kusajili meli. Nakushuru yote mawili umeyajibu kiungwana na kihekima, sisi masikini vibatali ndio asili yetu na hili la meli ndio usafiri wetu.

Mimi nina kawaida ya kuota mchana, mioyo ya Wazanzibari wote itapata faraja kubwa pale watakapo kuona wewe pamoja na mwenzio Maalim Seif Sharrif Hamad, ambae ni ndugu yako mtakapo kaa meza moja na kusameheana na kusafiana nia na nafsi, ili muirudishie Zanzibar amani na furaha iliyotoweka baada ya chaguzi.

Hii sio kazi rahisi naelewa, lakini hakuna lisilowezekana chini ya juu ikiwa ALLAH anataka kwa umma wake. Ni jambo la kustaajabisha sana, kuwa huu muungano wetu kuna wakati unatufanya unatuzuwia hata kusali, kuzika au kufanya kazi pamoja, huu ni msiba mkubwa Alhaj Shein.

Maridhiano tuliyokuwa nayo yaliyozaa serikali ya umoja wa kitaifa, yalianza na ndoto za mchana baina ya waungwana wawili, walioweka maslahi ya visiwa vyetu mbele badala ya Muungano, asili zao au vyama vya siasa. Huu ndio mfano wa kuigwa, wengi tulihusika katika ndoto hii, mimi nikiwa mmoja ya waasisi wake.

Mapinduzi yetu matukufu ya 1964 yalianza na ndoto za mchana  vile vile walizoota waasisi wetu wa ASP, wakiongozwa na baba wa taifa letu, hayati Mzee Abeid Amani Karume, Mungu amlaze mahali pema peponi, Ameenn. Mzee ametangulia kilichokufa nakuzikwa ni kiwiliwili chake tu, mawazo, fikra na maelekezo yake yapo, yatadumu na tutayatekeleza milele.

Muungano huu unaotutesa ulianza na ndoto za mchana pia za hayati Mwalimu Nyerere, baba wa taifa la Tangayika na baba wa taifa letu hayati mzee Karume, kama kawaida ya watu wengine huota wako peponi, wengine huota wako katika shida au motoni, sisi na muungano wetu tumegawika vile vile.

Mji mpya wa Fumba uliojengwa na Mzanzibari mwenzetu, Bwana Said Salim Bakhresa haukuja bila ndoto za mchana  alizokuwa nazo ndugu yetu huyu. Nimearifiwa kuwa umeshautembelea zaidi ya mara tatu, hii ni fakhari yetu sote, na matunda yake tutakula sote, bila kujali tofauti zetu za rangi, dini au tunatoka vyama gani vya siasa, sababu hiyo sio asili yetu kubaguana, tunajaribu tu.

Mheshimiwa Amiri jeshi wetu mkuu wa vikosi vyetu vya ulinzi vya Serekali ya Mapinduzi ya visiwa vya Zanzibar, naona faraja kubwa kukupa pongezi za dhati kwa uwezo na rehema aliyokupa Mola wetu, mpaka leo ukafikia kuwa kiongozi wetu wa cheo cha juu au mwisho kabisa katika ardhi au visiwa hivi. Nina hakika miaka kiasi hamsini na tano hivi iliyopita, wewe binafsi hukuwahi hata kuota kama kuna siku vyeo hivi vyote vitakuwa vyako. Lakini baada ya Mola wako kukupa umri wa kutosha, naamini ulianza “KUOTA” mchana kweupe, kuwa iko siku utakuwa kiongozi wa visiwa hivi, na sasa umekuwa, nani atakataa lile Mola analo amuru kumruzuku mja wake, kwa namna yoyote ile aipendayo yeye.

Nafahamu muda ulionao unahitaji kufanya kazi nyingi muhimu, sitaki uupoteze bila kiwango kwa warka wangu huu. Naomba nimalizie kwa kukutaka radhi za dhati kabisa ikiwa nimekukwaza au nimetoka nje ya mstari kwa lolote nililonena humu. Kwa kuwa sikuja kwako kukuvunjia heshima bali uchungu nilio nao umenifanya nishindwe kuvumilia, machozi yananibugujika nikiviona visiwa vyetu vinavyoangamia taratibu huku nimekaa kimya kwa kuwa mimi ni mwanachama wa ccm, ni lazima tuwe tayari kukosoana na kufamishana kwa sababu sote tunavitakia “kheri visiwa hivi”. Hapo nimekopa maneno yako, Maendeleo ndio shida yetu, pamoja na utambulisho wetu, SISI NI WAZANZIBARI KWANZA NA SIKU ZOTE TUTABAKIA KUWA HIVYO.

Tofauti zetu katika mitizamo ya kisiasa isitufanye tukasahau wajibu wetu kwa vizazi vyetu, tuitumie dini yetu vizuri katika kutuunganisha na sio kutugawa. Hivi karibuni  wakati unafungua jengo jipya la mahakama, umewaomba majaji na mahakimu wasicheleweshe kesi, kwa kuwa haki haitotendeka ikiwa watakuwa wazembe katika hilo. Niko chini ya miguu yako nakuomba Alhaj usiwasahau masheikh wa Uamsho.

Dhiki wanazo zipata wao binafsi pamoja na familia zao hazisemeki. Ugumu huu wa maisha uko nje bado ni mauti, jee viumbe hawa kesi zao huu ni zaidi  ya miaka minne bado hakuna ushahidi, huoni kuwa hapa umekosea? Kauli yako mwenyewe inagongana na mwenendo wa kesi hii? Wazungu husema “justice delayed is justice denied” kauli hii ndio maneno uliyosema mwanakwerekwe. Sasa ni wakati wa kuitimiza kwa vitendo, ni haki yao hawa wenzetu kupata “due process” katika nchi yoyote inayofuata sheria, iwe kesi ya ugaidi, wizi, uhaini au hata kuuwa.

Naomba uniruhusu nikutake radhi tena, mheshimiwa Amiri jeshi wetu, wewe ndie mlezi wetu, baba yetu, kiongozi wetu na hawa ni Wazanzibari wenzetu, bila wewe hawana mtetezi mwengine huko bara.

Nakushukuru kwa kuniazima sikio japo moja.

Shukran/Asante.

Tagsslider
Share: