Habari

Barua ya wazi kwa Serikali ya Dr.Shein.

Na.B.OLE,
Nimategemeo yangu kwamba Dr. Shein na Serikali yako mumejipanga vizuri katika kukabiliana na Wazanzibar wanaodai haki zao za msingi na  wenye nia na malengo ya kuitetea Nchi yao ambayo kwa sasa imeporwa na Watanganyika. Ni dhahiri kwamba wimbi hili la mageuzi halitoishia hapa lilipo bali ni vyema Serikali yako ikazidi kujiimarisha kukabiliana na walalahoi ambao tayari wameshakata tamaa na Serikali ya C.C.M inayotawala kwa Mabavu na unyanyasaji usio kwisha kwa Wazanzibar.

Mheshimiwa mtukufu Rais, tokea utwae madaraka sasa ni miaka miwili,tulitegemea angalau utakuwa na chembe ya huruma kwa Wananchi wako lakini pia utaongoza nchi hii kwa kuzingatia misingi na haki kwa wote lakini huku ukiongozwa na Ik-lass za Mola wetu mtukufu kama kiongozi muadilifu.Tumeshuhudia mengi kupitia serikali yako lakini haya yanayo endelea hivi sasa hatuwezi tena kuvumilia, hivi tukuulize Rais wetu mpendwa Serikali pamoja na Washauri wako munaipeleka wapi Zanzibar?

Mheshimiwa  mtukufu Rais,kikubwa na cha kushangaza zaidi ni kwamba hukufanya kosa tokea Dodoma hadi kupigiwa kampeni na hatimae kusimbikwa kama Rais,unachojaribu kukifanya ni kufuata nyayo za watawala wenzako waliopita kurithi uoza wao na kama hilo halitoshi  laskini pia kuongeza na ya kwako ili uadui uzidi kuwa mkubwa hapa Zanzibar  kwa lugha nyengine  chinja chinja.

Mheshimiwa  mtukufu Rais,inatupa  nadharia kwamba unayafanya haya kwa kulipa fadhila za Watawala walio kuweka hapo ulipo yaani Tanganyika lakini kumbuka kwamba na wewe ni Binaadamu lakini pia ni kiumbe ulieumbwa labda  niseme unaamini (siku ya mwisho) kufa na kufufuliwa, lakini pia unaamini hesabu na malipo kesho mbele ya kiama kwa wale wanaofanya wema na vile vile kwa wale wanaofanya mabaya kama Serikali yako. Kama hivyo ndivyo jee tujiulize sisi kama Marais hatutosimamishwa kujibu hoja na alie tuzidi  na anae miliki siku hiyo ya malipo?

Mheshimiwa  mtukufu Rais, uhai ni neema kubwa sana lakini pale tu kiumbe chochote seuze Binaadfamu mwenye akili timamu atakopoitumia hidaya hiyo kwa makini na uangalifu  neema hiyo. Mwisho wa yote ukubwa wako basi kumbuka ya kwamba utakwenda kuulizwa na Mola wako ni kitu gani uliwafanyia Wazanzibar katika utawala wako. Elewa muheshimiwa kwamba hapa hutoulizwa wewe kama Serikali lakini utaulizwa wewe kama Shein na kiongozi uliejipachika  madaraka na kuahidi kuwatumikia Watu kwa wema na usawa bila ubagudhi.

Mheshimiwa  Mtukufu Rais,najua unaelewa fika kinachowakumba Wazanzibar hivi sasa,ukatili,unyanyasaji,uonevu,kutotendewa haki,kuuliwa bila sababu,kudhalilishwa bila msingi ,yote haya wewe ndie dhamana na wewe ndie ambae umechukua dhamana na haya yote utaulizwa na yanataka majibu sahihi kesho mbele ya haki. Serikali yako inafanya dhulma bila kificho,inaadhibu watu,haki hakuna,sheria inawagusa wanyonge na wengine wako juu ya sheria.Yote haya muheshimiwa wewe ndie utakae ulizwa sasa chagua katika nafsi  yako ama ulwa na raha za Dunia na ukubwa au kumbuka na utanabaghi kwamba maisha ya akhera ni bora kwa kuifanyia mema nafsi yako.

Mheshimiwa mtukufu  Rais,elewa kwamba hakuna refu lisilo na mwisho hata hii Dunia ina mwisho wake na kama ni hivyo na wewe pia Urais wako utafika mwisho wake,hichi kinachofanywa hapa Zanzibar ni unyama ambao hata hao I-srail basi wana nafuu hawajafikia hatua hii.Inakuwaje mtu anakamatwa mbele ya watu,anapigwa na askari wako mpaka anakata roho halafu Kamishana wako anafanya jeuri kwa roho mbichi eti anasema yule ni mwizi,mla unga na mengineyo hivi kweli ndivyo, jee mwizi ,mla unga hii ndio hukumu yake ?

Mheshimiwa mtukufu Rais, Serikali yako chini ya amri za wakubwa wako kutoka Tanganyika mumeleta Majeshi  Visiwani kuwatisha watu wasidai haki zao,Askari hawa  kutoka Mrima hawana tone la uchungu, hawana hata ndugu hapa Zanziibar,wala hawana chembe ya imani na huruma kwa Wazanzibar,lengo ni kuwakandamiza na kuwauwa kwa kisingizio cha uwekaji wa Amani ,hivi tuseme Amani inakuwa hivi au ndio hivyo tena  Punda life ila mzigo wa bwana ufike ?

Mheshimiwa  mtukufu Rais, katika kipindi cha wiki mbili tumeshuhudia Zanzibar ikiwaka moto,tatizo ni Serikali yako ambayo haina  dira wala Washauri wazuri lakini na wewe mwenyewe pia,hivi hata hekma na busara inashindikana katika kuweka amani !Washauri wako wakiwemo usalama wa Taifa wamesoma wapi ? Maanake hata hizo mbinu za kiuaskari hazieleweki,hivi inakuwaje Askari kumteka Raia halafu Serikali hiyo hiyo inakuja kwenye vyombo vya habari na kuonesha dharau kwa kusema maneno machafu ambayo hayana hata chembe ya ukweli kwa Wananchi wake,hii ni aibu na fedheha kwa Serikali ya kidemokrasia.

Mheshimiwa mtukufu  Rais, unawachukua Masheikh na Wanazuoni wanaosimamia  njia ya Allah, unawanyanyasa na kuwa funga jela katika siku tukufu alizotusia Mola na Mtume wetu, kwa kujiridhisha wewe nafsi yako na hao waliokutuma bila kujali kwamba Masheikh hawa wamesimama na kamba  ya mola wetu yenye kuamrisha haki na kupinga batili !. Imani yao hii haitopotea bure, haki siku zote hushinda.

Mheshimiwa  mtukufu Rais, hivi umetumia vipimo gani kwa kumchagua Kamishina wa Polisi,Makamo wa pili wa Rais na baadhi ya Mawaziri wako ? Maana inaonesha dhahiri kwamba ndio vinara vya uchochezi unafiki  na kusema uongo lakini pia ni wafitinishaji wakubwa wa Wazanzibar. Hawa ndio wanaosababisha Zanzibar kuwaka moto hivi sasa. Na haya yasifikiriwe kwamba kuwatisha Wazanzibar kwa njia hii ndio munawapunguza kasi bali ni njia mojawapo ya kuwafanya watu kuwa masugu na hatimae kuja mwilini.

Mwisho Mheshimiwa  mtukufu Rais, nitoe mfano wa Watawala ambao wewe na utawala wako humjawafika hata robo ya ukatili wao  waliofanya kama vile utawala wa Firauni pale Misri,utawala Roma enzi hizo,soma historia ya as-hab Qaff,gadaffi,Hossein Mubarak na wengine lakini leo hii imebaki ni historia tu, malipo yao anayajua Mola muumba wa mbingu na ardhi,kwa maana hiyo tunakumbushana kwamba kuwaonea watu wengine haya kwa maslahi  binafsi huku unaua nafsi za waja  wenye kudai haki zao bila sababu ni dhahiri iko siku inshallah kizambani hatopanda Ustadh Farid na Msellem peke yao bali na wewe utapanda kwenye mahakama ya Muumba  wa ardhi na mbingu, na siku hiyo hutokuwa na bodi guard,usalama wa Taifa wala Washauri, tumuugope M/mungu kwa sote.

Share: