Habari

Bi Mwanajuma : wema mkubwa duniani ni kujua thamani ya wazee

June 10, 2018

Imeandikwa na Salmin Juma, Zanzibar

Naibu katibu mkuu Wizara ya kazi, uwezeshaji wazee, wanawake na watoto anaye shughulikia mas-ala ya ustawi wa jamii, wanawake na watoto Mh: Mwanajuma Abdalla Majid alisema kuwa, wema mkubwa duniani ni mtu kujua thamani ya wazee kwani ndiko kutakapo wapelekea kuishi katika hali nzuri za kimaisha kama ilivyo kwa makundi mengine ya watu nchini.

Ameyaeleza hayo jana katika nyumba za wazee Sebleni Amani Zanzibar katika hafla maalum ya futari iliyoandaliwa na jumuiya ya kiisilamu ya Alfatah Charitable Association ambapo alisema , ni jambo la umuhimu kuwafutarisha wazee hao kwani hupata faraja na kujisikia amani.

Akizungumza kwa hamasa kubwa mbele ya wazee hao Bi Mwanajuma alisema, jumuiya zipo nyingi nchini lakini kitendo kilichofanywa na Alfatah ni cha kuigwa kwani kinajenga mapenzi baina ya waisilamu jambo ambalo taasisi nyengine hawajathubutu kufanya hivyo.

‘’ kama tulivyoambiwa, pepo ipo chini ya nyayo za mama zetu , hivyo kuwajali na kuwathamini wazee huu ni wema mkubwa ‘’ alisema Bi Mwanajuma.

Alisema, Binafsi amefarijika kuona wazee wanafuraha kwani kila mmoja anahitaji kuishi kwa amani , hivyo jumuiya ya Alfatah inayo wajibu wa kuhakikisha inazidisha juhudi katika zake ili jamii izidi kunufaika.

Kwa upande wake mkurugenzi wa Jumuiya ya Alfatah Charitable Association Sh Rashid Salim Mohd alisema, kuna maeneo tofauti ya kwenda kuwafutarisha waisilamu lakini jumuiya yake imeona umuhimu mkubwa wa kuwafutarisha wazee kwanza, alisema unapo wajali na kuwathamini wazee ni moja kati ya njia ya mafanikio hapa duniani.

Akijibu suala la mwandishi wa habari aliyetaka kufahamu vipi jumuiya inawatazama wanananchi wa kisiwa cha Pemba ambao pia wanaishi katika mazingira magumu Mkurugenzi huyo alisema , jumuiya yao imejipanga kuwafikia watu wote wanao ishi katika mazingira magumu Unguja na Pemba na kila upande utanufaika na kile wanachokipata kwani ndio majukumu yao.

‘’kesho kutwa tunajiandaa kwenda Pemba , lengo na madhumuni ya safari yetu ni kupeleka faraja kwa familia za wasiojiweza , kwa kuwafutarisha na kuwasaidia katika huduma nyengine, lakini hata hivyo tokea kumi la mwanzo jumuia inawafutarisha wananchi wa kijiji chote cha mkia wa ng’ombe Micheweni ‘’ alisema Sh Rashid.

Akiendelea kueleza, mkurugenzi huyo alisema, hakuna raha kubwa kama kuishi na wazee vizuri na jambo la kuwafutarisha limepelekea jumuiya kujihisi ni wabora kwakua lengo la kuwaondoshea huzuni wazee hao limetia.

Sambamba na hayo alitoa wito kwa wenye vipato vya hali ya juu kushirikiana kwa karibu na jumuiya hiyo ili kufikisha faraja katika makundi ya watu ambayo yanaonekana kuishi katika mazingira magumu kama vile umasikini uliyokithiri, na mengineyo.

‘’jumuiya inafika katika maeneo ya mbali vijijini kuchunguza shida na changamoto za kimaisha wanazokabiliana wananchi, jumuia inajua mengi sana juu ya yale yanayowasibu watu , na watu hao wanatutumainia sisi kuwasaidia katika shida zao, kama tutawatupa wataishi katika mazingira gani kila siku, hivyo wahisani wanayonafasi ya kushirikiana na taasisi hii ili kwa pamoja tufikie lengo la kuwapa unafuu wa maisha watu hao.

Mwamize Nyange Saleh, mzee katika nyumba hizo alisema , kitendo cha kuwekwa pamoja na kuwafutarisha, kimewapa furaha na kujihisi kuwa ni watu wa kawaida katika jamii.

‘’ tunafurahi sana kwa futari, yaani najihisi kushiba na alhamdulillah mungu awalipe mema waliyotufanyia hivi’’ alisema Bi Mwamize.

Mzee mwengine aliyejitambulisha kwa jina la Majid Khamis Saleh alisema ‘’ tunawashukuru waliyotuletea futari hii, nimekula mpaka vyengine nimeviwacha , nimeshiba najisikia raha ‘’ alisema Majid

Bi Asha Rajab ambae pia alikuwemo katika hafla hiyo ya futari, alitoa wito kuwataka jumuia hiyo na nyenginezo , wawe na utaratibu wa kuendelea kuwafariji kila siku ili wajihisi wanaishi katika mazingira mazuri.

Pembatoday

Share: