Habari

BOT yachukua usimamizi Bank M

AUGUST 5, 2018 BY ZANZIBARIYETU

BENKI kuu ya Tanzania (BOT), imechukua usimamiza wa benki (M) Tanzania Plc kuanzia jana baada ya kubaini kuwa benki hiyo ina upungufu mkubwa wa ukwasi kinyume na matakwa ya sheria ya benki na taasisi za fedha ya mwaka 2006 na kanuni zake.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Gavana wa benki kuu Prof. Florens Luoga, alisema kuwa upungufu huo wa ukwasi unahatarisha usalama wa sekta ya fedha na hivyo kuendelea kutoa huduma za kibenki kwa benki hiyo kungeweza kuhatarisha usalama wa amana za wateja wake.

Prof.Luoga alisema kutokana na uamuzi huo benki kuu imesimamisha bodi ya wakurugenzi na uongozi wa benki hiyo, kuanzia jana na imemteua meneja msimamizi ambaye atakuwa na jukumu la kusimamia shughuli za benki M kwa kipindi ambacho itakuwa chini ya usimamizi wa benki kuu.

“BOT tunapenda kuuhakikishia umma kuwa itaendelea kulinda maslahi ya wenye amana katika benki hiyo na kwamba uendeshaji wa shughuli za benki hiyo utakuwa chini ya BOT”, alisema.

Aidha alisema kuwa Januari 4 mwaka huu, benki kuu iliongezea muda wa miezi sita, benki tatu ambazo ni Tandahimba Community Bank limited (TACOBA), Benki ya Wanawake Tanzania PLC (TWB) na Kilimanjaro Cooperative Bank Limited (KCBL) Juni 30 mwaka huu, ili kufikisha kiwango cha mtaji kinachohitajika.

“Sheria ya mabenki na taasisi za fedha ya mwaka 2006 na kanuni zake imeweka kiwango cha chini cha mtaji cha shilingi billion 2 kwa benki za wananchi, ambapo benki hizo ziliongezewa muda wa mwezi mmoja hadi Julai 31 mwaka huu ili kukamilisha taratibu za kuongeza mtaji”, alisema.

Aidha alisema mkakati wa serikali ya Jamhuri ya Muungano wa kurekebisha na kuboresha muundo wa benki za uuma, wanahisa wa TWB na TPB wameamua kuunganisha benki hizo, ili kuboresha ufanisi na utendaji wa benki hizo.

Alieleza kuwa Benki kuu ya Tanzania imeridhia ombi la uunganishaji wa benki ya wanawake Tanzania (TWB) na benki ya posta Tanzania (TPB) na kuwa benki moja kuanzia Agosti 3 mwaka huu itayoitwa TPB BANK PLC.

Alifafanua kuwa muunganiko huo utaifanya benki mpya ya TPB kuwa na mtaji wa kutosha kama inavyotakiwa kisheria chini ya kifungu cha 17 cha sheria ya mabenki na taasisi za kifedha ya mwaka 2006.

Hata hivyo, alieleza kuwa kuhusu benki za kijamii Tandahimba community bank pamoja na Kilimanjaro community bank, ambazo Januari 6 mwaka huu, zilipewa muda wa miezi sita na baadaye kuongezewa kipindi cha mwezi mmoja ili ziweze kujiongezea mtaji, sasa zimekidhi kiwango cha mtaji kinachohitajika na zinaendelea na shughuli zake kama kawaida.

Zanzibar Yetu

Share: