Habari

Bunge la Umoja wa Ulaya (EU) latoa maazimio 15 kwa Tanzania

Rais John Magufuli akiwa na Mjumbe wa Umoja wa Ulaya (EU), Balozi Roeland van de Geer

George Njogopa – Mwananchi
Jumamosi, Disemba 15, 2018

Bunge la Umoja wa Ulaya (EU) limepitisha azimio lenye vipengele 15 vinavyohusu Tanzania kwa kugusia masuala ya utawala wa sheria, haki za binadamu na kamatakamata ya viongozi wa upinzani.

Lakini, Waziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania, Dk Augustine Mahiga amesema anasubiri maelekezo kutoka kwa Rais kuzungumzia suala hilo.

Azimio hilo namba 2018/2969 ni mwendelezo wa hoja zilizowahi kuibuliwa na jumuiya hiyo ya kimataifa kuhusu Tanzania.

Hoja hizo zinahusu mambo kama haki za binadamu, masuala ya afya, elimu, haki za kupata habari, kuzuiwa kwa matangazo ya moja kwa moja ya bunge, mikutano ya kisiasa, sheria kandamizi na matamko.

Aidha, Waziri Mahiga jana alinukuliwa akisema kuwa hawezi kutolea majibu yoyote azimio hilo.

“Siwezi kuzungumzia lolote kuhusu hili. Bado nasubiri maelekezo kutoka kwa Rais. Eh nasubiri maelekezo ya Rais,” alisema kwa kifupi,” Dk Mahiga.

Bunge hilo la EU lilipitisha azimio hilo lililoandikwa Desemba 12, baada ya majadiliano yaliyofanyika mjini Brussels, Ubelgiji ikiwa ni mara ya kwanza kwa chombo cha kimataifa kutoa azimio dhidi ya Tanzania.

Huku likiwa limenukuu vifungu kadhaa vya kimataifa na kugusia uhusiano wake na Tanzania, azimio hilo ambalo limesambazwa sehemu mbalimbali linataka Tanzania irekebishe baadhi ya sheria.

Bunge hilo limebainisha matukio kama kupigwa marufuku mikutano ya kisiasa, kuandamwa kwa waandishi wa habari na watetezi wa haki za binadamu, kufungia vyombo vya habari, kuzuia Bunge Live kuwa ni kati ya mambo yanayokwenda kinyume na misingi ya haki za binadamu.

Azimio hilo limehoji kampeni iliyotangazwa na mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda ya kuwasaka watu wanaojihusisha na mapenzi ya jinsia moja. Azimio limetaka serikali imzuie Makonda, kuendelea na kampeni hiyo.

Hata hivyo, hivi karibuni serikali ilishabainisha kuwa kampeni hiyo haikuwa na ridhaa yake na alichokuwa akikifanya Makonda ni maoni yake binafsi.

Bunge hilo limetoa wito likitaka kuachiliwa kwa wafungwa wote wa kisiasa, kufanyiwa marekebisho kwa baadhi ya sheria.

Sheria hizo, inayohusu makosa ya mtandao, sheria ya vyombo vya habari, sheria ya Elektroni na Mawasiliano ya Posta (Epoca) na kuachiwa uwanja wa watetezi wa haki za binadamu kufanya shughuli zao.

Pia, limetaka tume huru itakayochunguza matukio yenye utata kama kutekwa na kukamatwa kwa waandishi wa habari na matukio ya watu kutoweka katika mazingira ya kutatanisha.

“Tungependa kuona wale watakaobaini kuwa nyuma ya matukio hayo, hatua za kisheria zinachukuliwa dhidi yao,” linasema azimio hilo.

Hii ni mara ya pili kwa EU kuelezea jinsi isivyoridhishwa na mwenendo wa Tanzania baada ya awali kumuita mwakilishi wake Brussels kwa ajili ya majadiliano.

Akizungumza baada ya kuombwa kutoa maoni yake kuhusu sakata hilo, Profesa Kitojo Wetengere wa Chuo cha Diplomasia (CFR) alisema Serikali isipuuzie azimio hilo.

“Kuna umuhimu wa kukaa meza moja ya majadiliano na EU ili serikali iwaelimishe kwa nini inafanya inachokifanya sasa,” alisema Wetengere.

Wakati huo huo VOA News Swahili, Imeandika:

Maseneta wa Marekani wamemuandikia barua Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo, Mike Pompeo wakieleza wasiwasi wao juu kushuka kwa kuheshimiwa kwa haki za binadamu na demokrasia nchini Tanzania.

Maseneta hao wamesema: “Tangu mwaka 2015 nchi hiyo inaongozwa kwa sera zinazotengeneza mazingira ya uvunjifu wa amani, vitisho na ubaguzi.”

Haki za binadamu

Wamedai katika barua iliyotumwa Desemba 12, serikali inaminya haki za binadamu na demokrasia. Wameongeza kuwa tangu mwaka 2016 nchi hiyo haina Balozi rasmi nchini Tanzania hivyo ni lazima Balozi ateuliwe.

Maseneta wanataka ubalozi wao uanze kufanya juhudi za kuhakikisha kunakuwa na uchaguzi huru na wa haki mwaka 2020.

Pia wameitaka Marekani ihakikishe hakuna fedha zinazotolewa na taasisi yoyote ya kimataifa kufadhili sera zinazoonekana kuwa kinyume na haki za binadamu.

“Tunakuandikia tukiwa na wasiwasi mkubwa juu ya kuminywa kwa uhuru wa kisiasa Tanzania, na tunahimiza uongozi wa Marekani kuongeza mawasiliano kuonyesha ongezeko la mmomonyoko wa haki za raia na uhuru wa kidemokrasia katika nchi hiyo.”

Uongozi wa Magufuli

Tangu uongozi wa Rais John Magufuli uchukue madaraka mwaka 2015, umekuwa ukiendeshwa na sera za kutumia mabavu, vitendo vya uvunjifu wa amani, vitisho dhidi ya jumuiya za kiraia, vyombo vya habari na vyama vya upinzani.

Barua hiyo imeandika pia, wasichana wanalazimishwa kupimwa mimba; wale walio wajawazito wanafukuzwa na kuzuiwa kumaliza masomo yao.

Imeeleza kuwa Rais Magufuli amezuia ufadhili wa Marekani wa programu ya HIV/AIDS iliyokuwa inawafikia na kutoa huduma ya afya kwa mashoga, idadi muhimu ya watu wanaolengwa na jitihada za kupambana na HIV/AIDS.

Vyombo vya habari

Barua hiyo inaeleza kuwa magazeti yamekuwa yakidhibitiwa kwa kutozwa faini au kufungiwa kwa kuripoti habari ambazo zinaonekana kuikosoa serikali.

Sheria ambazo zinaminya uhuru wa vyombo vya habari na kuzuia maudhui kwenye mitandao ya jamii zimepitishwa kuwa sheria. Yote hayo ni wakati wa utawala wa Magufuli.

Viongozi wa upinzani

Viongozi wa upinzani bungeni wamepigwa risasi baada ya kumkosoa Rais, wamekamatwa na kubughudhiwa na polisi, na wengine wameshtakiwa kwa makosa ya uchochezi.

Barua hiyo inaelelza hatua za wadau katika jumuiya ya kidiplomasia walizochukuwa kukabiliana na kutetereka kwa demokrasia na kuzuka kwa vitendo vya ubaguzi.

Umoja wa Ulaya

Tayari Umoja wa Ulaya umemwita Balozi wake kutoka Tanzania baada ya kile kilichoitwa ni ‘kulazimishwa kuondoka’ kutoka Tanzania, na msaada wake wa kifedha na sera zake kwa Tanzania zinajadiliwa.

Serikali ya Denmark

Mfadhili mwengine muhimu, Denmark, amesema itazuia msaada wa kifedha wenye thamani dola za Marekani milioni 10, ikieleza wasiwasi wake juu ya uvunjifu wa haki za binadamu na “kauli za sheria kali na vitisho zisizo kubalika dhidi ya wapenzi wa jinsia moja” zilizotolewa na maofisa wa serikali.

Benki ya Dunia

Benki ya Dunia ilikuwa tayari imezuia ujumbe wake kwenda Tanzania, na kusema itaruhusu ujumbe huo kuzuru nchi hiyo iwapo tu serikali itawahakikisia kuwa itajizuia na kuwabughudhi na kuwabagua watu kutokana na mwenendo wa jinsia zao.

Benki hiyo imetishia kufuta mpango wa mkopo wa dola za kimarekani milioni 300 ziilizotengwa kwa ajili ya Tanzania baada ya nchi hiyo kurejea tena msisitizo wa sera yake ya kuwapiga marufuku wasichana wenye mimba kurudi shuleni.

Na serikali kuacha mpango wake wa kufanya ni kosa la jinai “kuhoji takwimu rasmi” za serikali hadharani.

Lakini akizungumza katika uzinduzi wa maktaba ya kisasa ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) Jumanne, Novemba 27 Magufuli aliwaambia viongozi wa upinzani watulie “la sivyo wataishia gerezani”.

Rais Magufuli alipeleka ujumbe mpya kwa viongozi wa vyama vya upinzani wa Tanzania akiwaonya kuwa iwapo ‘hawataheshimu sheria’ wataishia magerezani.

Rais huyo alimpa ujumbe huo Waziri Mkuu wa zamani Edward Lowassa ambaye sasa ni mjumbe wa kamati kuu ya chama cha upinzani cha Chadema.

Magufuli aliongeza: “Hii ndio Tanzania mpya tunayoitaka…Nimeona hili nilizungumze kwa heshima kubwa, Mzee Lowassa, ili wale unaowaongoza kule, uende ukawashauri…’otherwise’ (la sivyo) wataishia kwenye magereza ili wakajifunze namna ya kuheshimu sheria za Watanzania.”

Tayari viongozi kadhaa wa upinzani Tanzania wakiwemo wa chama cha Chadema ambacho Lowassa ni mjumbe wa kamati kuu wanashtakiwa kwa tuhuma mbalimbali.

Share: