Habari

Butiku:Wazanzibari msikubali kuridia uchaguzi

Salma Said,

Taasisi ya Mwalimu Nyerere imeitaka Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) kufanya kazi kwa kuzingatia katiba na sheria za nchi na kuacha kutanguliza mbele maslahi binafsi ya kisiasa.

Akizungumza na vyombo vya habari mjini Musoma, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi hiyo, Mzee Joseph Butiku, amesema amekerwa na tabia ya Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar kusitisha uchaguzi na kushindwa kuwatangazia wananchi kiongozi wao waliomchagua, huku ikishindwa kuheshimu matakwa ya wananchi waliopiga kura katika visiwa vya Zanzibar.

Taasisi hiyo imeitaka Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar kufanya kazi kwa uweledi na kuheshimu maamuzi ya wananchi na sio kwa kutanguliza mbele maslahi binafsi ya kisiasa hatua ambayo inaweza kusababisha machafuko na umwagaji wa damu katika visiwa vya Unguja na Pemba.

Aidha Mzee Butiku amewataka wananchi wa Zanzibar kutokubali tena kurudia upigaji wa kura hadi hapo yatakapotolewa maelezo ya kuridhisha na wahusika waliosababisha uchaguzi huo kufutwa pia waweze kuchukuliwa hatua kali za kisheria

Mzee Butiku amesema kwa sababu hiyo amewataka viongozi kuheshimu sheria na katiba ya nchi na kwamba chama ambacho kinadhani kimeshindwa katika uchaguzi huo kikubali matokeo badala ya kuifanya Zanzibar ni mali ya chama fulani pekee.

Uchaguzi wa Tanzania umefanyika Octoba 25 mwaka huu ambapo wazanzibari nao wamepiga kura tano ikiwemo ile ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mbunge ziliyosimamiwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi ya Tanzania (NEC) na kura tatu za kumchangua Rais wa Zanzibar, Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi na Diwani.

Wakati matokeo ya uchaguzi yameanza kutangazwa majimbo 32 na baadhi ya wagombea kukabidhiwa matokeo yao ambayo yalibandikwa vituoni na baadhi ya matokeo hayo kutangazwa kwenye kituo kikuu cha kutangazia matokeo katika Hoteli ya Bwawani ghafla zoezi hilo likasitishwa na kufutwa kabisa mnapo Octoba 28 ambapo Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) Jecha Salum Jecha alipojitokeza kwenye kituo cha televisheni cha taifa.

Jecha alisema kutokana na kasoro nyingi zilizojitokeza katika uchaguzi huo kwa mamlaka aliyopewa anafuta uchaguzi huo na Tume hiyo italazimika kufanya uchaguzi mengine upya, kauli hiyo imepigwa na baadhi ya wanasiasa na wanasheria mbali mbali nchini.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti wanasheria hao wamesema kwamba Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi hana mamlaka ya kisheria kufuta matokeo ya uchaguzi na hivyo zoezi liendelee pale liliposita na aliyeshinda atangazwe na hatimae kuapigwa kuwa Rais wa Zanzibar

Share: