Habari

CCM imara inahitaji Upinzani madhubuti – Julius Nyerere (1990s)

Na Gululi Kashinde – Raia mwema

March 14, 2018

DESEMBA 13 mwaka 1991 Mwalimu Julius Nyerere alizungumza na waandishi wa habari nyumbani kwake Msasani, Dar es Salaam, juu ya kuwepo kwa mfumo wa vyama vingi vya siasa nchini.

Siku iliyofuata, Desemba 14, waandishi wa habari mashuhuri na waandamizi, Salva Rweyemamu (aliyewahi kuwa Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu utawala wa Kikwete) na mwenzake Lukas Kisasa, kwa pamoja walichapisha habari katika Gazeti la Uhuru (Gazeti la CCM) likiwekewa kichwa cha habari: “Hali inaruhusu vyama vingi nchini – Nyerere.”

Katika mkutano huo na wanahabari, pamoja na mambo mengi mtawanyiko yaliyozungumzwa, Mwalimu Nyerere alishangaza wengi aliposema; “ubovu wa uongozi ndani ya CCM ndiyo ulionifanya nikapendekeza tuanzishe mfumo wa vyama vingi.”

“Nilitumaini kuwa tunaweza kupata chama kingine kizuri ambacho kingeweza kuiongoza nchi yetu badala ya CCM, au ambacho kingekilazimisha CCM kujisafisha uongozi wake, kwa kuhofia kuwa bila kufanya hivyo, kitashindwa katika uchaguzi ujao.”

Huo ndiyo ulikuwa mtizamo wa Mwalimu Nyerere kuhusu uwepo wa vyama vingi na siasa za ushindani hapa nchini. Mwalimu aliamini kuwa, CCM imara inahitaji upinzani madhubuti.

Ukubwa na ukongwe wa CCM ulikifanya kuanza kubweteka na kushindwa kujibu changamoto mtambuka. Mserereko huo ulimfanya Mwalimu Nyerere kuwa mkosoaji mkubwa wa sera za chama chake.

Mwalimu Nyerere, alikosoa hadharani pasipo woga wala hofu. Huyu ndiye alianza kuasisi dhana ya “chukia makosa, penda wakosoaji” ndani ya chama chake.

Nimelazimika kurejea haya yote mara baada ya kuanza kunusa harufu mbaya ya kuturejesha tulikotoka. Mjadala sasa ni mkali hususan kwenye mitandao ya kijamii.

Watu wanaanza kuhoji iwapo kuna umuhimu wa kurejea kwenye mfumo wa chama kimoja. Mjadala huu unakolezwa na ukweli halisi juu ya hali ya kisiasa hapa nchini.

Malalamiko kwa vyama vya siasa yameongezeka kwa madai kuwa, mazingira ya kufanya siasa kwa sasa ni magumu sana na hatarishi. Orodha ya matukio ya kuzuia shughuli za siasa ni ndefu.

Kuzuia mikutano ya hadhara kwa vyama vya upinzani ni miongoni mwa matamko hatarishi kwa ustawi wa demokrasi yetu changa.

Pamoja na ukweli huo, si sahihi hata kidogo kutamani kurejea au kurejeshwa kwenye mfumo wa chama kimoja. Zipo sababu kadhaa.

Mosi, dunia inahama kwa kasi sana kutoka mfumo wa Chama kimoja kwenda siasa za ushindani. Yeyote anayetamani kurejea huko tulikotoka ni sawa na kutamani kufuta historia ya nchi hii.

Pili, tafiti zote zinaonesha wazi kwamba, maendeleo na demokrasia ni chanda na pete. Huwezi kutenganisha uwepo wa demokrasia na maendeleo.

Uhuru wa watu kuzungumza mambo yao kwa uhuru na uwazi pasipo hofu yoyote ndio injini na kichocheo cha maendeleo.

Hakuna serikali yoyote inayoweza kuwaletea maendeleo wananchi wake pekee yake pasipo ushiriki wa wananchi wake weyewe. Hii ni dhana ya kitafiti.

Kujificha katikati ya dhana kuwa, uchumi na maendeleo ndiyo huzaa demokrasia ni kujidanganya na kujiliwaza kwa kutumia dhana mfu. Ukweli ni kwamba, msingi mzuri wa ujenzi wa maendeleo na ukuaji wa mitaji na uchumi ni uwepo wa demokrasia.

Kujaribu kutenganisha demokrasia na maendeleo ni kutokujua dhana pana ya maendeleo. Hii ni dhana pana inayohitaji mjadala mahususi kwa siku zijazo.

Lakini itoshe tu kusema, kamwe tusitumie kigezo cha maendeleo na ujenzi wa uchumi kwa kuminya uhuru wa watu kutoa maoni na hata kufikiri tofauti.

Wapo baadhi ya makada watiifu wa CCM walau waliobakia na chembechembe za Mwalimu Nyerere, wengi wao walikuwepo Msasani kwenye mkutano wa Mwalimu Nyerere na wanahabari mwaka 1991.

Hawa wanakerwa sana na makatazo ya kuzuia shughuli za kisiasa. Tofauti yao na Mwalimu Nyerere ni moja; Mwalimu alikemea hadharani bila uoga, lakini wao wamebakia kunong’ona chini kwa chini kwenye makorido ya ofisi ndogo ya CCM Lumumba, Dar es Salaam.

Ni vema ikaeleweka kwamba, mnufaikaji muhimu wa uwepo wa siasa za vyama vingi ni CCM yenyewe. Na ni busara kutambua kuwa, kazi ya vyama vya upinzani ni kutafuta makosa ya serikali iliyoko madarakani na kuyaanika hadharani. Vyama vya siasa kusifia serikali iliyopo madarakani ni hiyari si sharti.

Mifano ya CCM kunufaika na ukosoaji wa vyama vya upinzani ipo mingi. Mathalan, tangu serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais John Pombe Magufuli iingie madarakani imeweza kujipambanua kwa mambo makuu mawili:

Mosi, ikisema inatenda. Hii ni tofauti kidogo na awamu ya nne iliyoongozwa na Jakaya Kikwete, ilikuwa ikisema haitendi na ikitenda haisemi. Pili, awamu ya tano inashughulika na yote yaliyosemwa na wapinzani katka awamu zilizopita.

Mambo yaliyoibuliwa na wapinzani huko siku za nyuma hususan masuala ya ufisadi na rushwa, ndiyo hayohayo yanayoshughulikiwa na serikali ya awamu ya tano hivi sasa.

Vyama vya upinzani ni sawa na kioo. Kazi ya kioo ni kuonesha kasoro. Huwezi kulaumu au kuvunja kioo baada ya kukuonesha kuwa hujanawa uso vizuri kwa sababu waliokuzunguka hawataki kukwambia ukweli. Tafakari.

gululig@yahoo.com – Simu: 0753 270 441

Share:

1 comment

 1. zamko 14 Aprili, 2018 at 19:24 Jibu

  @ Muandishi,
  nakupa hongera sana kaka kwa makala yako nzuri sana yenye Ukweli Mtupu. Na nibora Hii habari Imeandikwa na Nyinyi Wenyewe Watanganyika ambao Munamuona Nyerere kafanya la Maana kutaka mfumo Wa Vyama Vingi. Naam hivo ndivo ilivozaniwa na Wengi sana Hadharani.

  Lakini Nyuma ya Pazia Nyerere alikuwa ana maana Nyengine ya Kuwa na Mfumo wa Vyama vingi, .. Mtazamo Wake nikutaka Kuwagawa Wazanzibari katika Uhizbu na Uafrica.. Na inasemekana Huko Nyuma ya Pazia Aliwahi Kusema tufanye Vyama vingi Watakaoanza kupigana wenyewe kwa Wenyewe na Kubaguwana ni Wao Wanaoutaka Vyama Vingi Yaani Wazanzibari.

  Kama Nyerere alikuwa na Nia safi ya Vyama vingi na aliamini kama Msemo huo unaosema kwamba …. Nanunukuu “Nilitumaini kuwa tunaweza kupata chama kingine kizuri ambacho kingeweza kuiongoza nchi yetu badala ya CCM, au ambacho kingekilazimisha CCM kujisafisha uongozi wake, kwa kuhofia kuwa bila kufanya hivyo, kitashindwa katika uchaguzi ujao.”… Mwisho wakunukuu maneno ya Nyerere.

  Kwanini 1995, CUF iliposhinda kule Zanzibar na CCM kubadilisha Matokeo na kumtangaza Salimini hali ya Kuwa CCM Ilishindwa Vibaya sana licha Ya Wizi Wao, Kuroga na Wengine Kukobea Bwawa la Maji Uchi ( Akina Amina Salimu Ali).. Nyerere hakuingilia na Kumwambia Salimini Amour Amuache Sefu Achukue Nchi kwasababu chama chake kilishinda???

  Badala yake Wao ndio walio shangiria Uamuzi wakubadilisha matokeo ya CUF kupewa CCM na Yale ya CCM kupachikwa CUF.. ?…

  Baada ya Hapo Nyerere huyo huyo alipendekeza nafasi ya Makamo wa 1 wa Raisi wa Muungano ambayo ilikuwa ni Raisi wa Zanzibar inbadilishwe kwani alishaingiwa na Hofu kwamba CCM haitafanya vizuri hasa kwa upande wa Zanzibar…

  Nyerere alikuwa na Nia yakuisambaratisha Zanzibar katika Mfumo wa Vyama vingi kwakutumia Sera zake za Waweke CCM katika Madaraka na Uwalinde kwa njia yoyote ile. Hatimaye Ndoto Yake yakuviburuza Visiwa vya Zanzibar katika Bahari ya Hindi na Kuvitupa ingetimia.. Na sasa tunayaona hayo ya Kuburuzwa Ki Sycologia na Kiuchumi sio Ki Geographical, kwani uwezo huo hata huyo Raisi wenu Wa Malaika alieletwa na Mungu hawezi.

Leave a reply