Habari

CCM Nyang’anyang’a Bunge la Katiba

Dar es Salaam/Moshi. Chama Cha Mapinduzi (CCM), kimeanza kumeguka baada ya baadhi ya wabunge wake ambao ni Wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba, kuunga mkono kauli ya Naibu Katibu Mkuu wake, Mwigulu Nchemba.

Nchemba ambaye pia ni Naibu Waziri wa Fedha, Jumanne iliyopita akichangia wakati wa mjadala wa mabadiliko ya kanuni, alilitaka Bunge Maalumu la Katiba lijitathmini kama lina ulazima wa kuendelea wakati hakuna uhakika wa kupatikana kwa theluthi mbili.

Alisema kitendo cha Bunge hilo kukaa kwa siku 84 bila uhakika wa kupatikana kwa theluthi mbili kwa pande zote mbili inayohitajika kupitisha Rasimu ya Katiba Mpya, hakiwezi kueleweka kwa Watanzania.

Nchemba alisema ni vyema kujua idadi ya wanaoshiriki awamu ya pili ya Bunge hilo ili kutoa uthibitisho kimahesabu kama uamuzi wa kuendelea kwa Bunge unaweza kuwa na maana.

Jana Mwigulu Nchemba alizidi kusisitiza kauli aliyoitoa akisema ni msimamo wake binafsi kama mtoto wa maskini. Alisema anatambua jinsi walipa kodi watakavyoumia, rasimu hiyo itakapokwama kupita kutokana na kukosekana kwa theluthi mbili ya pande zote.

Bunge la Katiba limepanga kutumia Sh20 bilioni huku wajumbe wake wakilipwa posho ya Sh300,000 kwa siku lakini hali halisi inaonyesha kwamba hata waketi siku 90 na watumie mabilioni yote hayo ya fedha, mwisho wa siku, theluthi mbili haitapatikana.

Hata hivyo, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye juzi alijibu akisema kauli ya Nchemba ni mtazamo wake binafsi na hakuongea kama kiongozi wa chama hicho.

Lakini jana wabunge mbalimbali wa CCM walijitokeza hadharani wakisema wanaunga mkono kauli ya Nchemba ili hesabu ijulikane badala ya kuendelea kutafuna fedha za wananchi bila tija.

Ali Keissy

Mbunge wa Nkasi Kaskazini, Ali Keissy, alisema msimamo wa Nchemba ndiyo msimamo sahihi ambao unapaswa kufuatwa kuliko kuendelea na Bunge wakati wakijua kuwa theluthi mbili haitapatikana.

Lembeli

Mbunge wa Kahama, James Lembeli aliliambia gazeti hili jana kuwa alichokisema Nchemba ni ukweli ambao haupingiki.

Mbunge wa Viti Maalumu, Esther Bulaya alisema: “Kiukweli kutoka moyoni mwangu namuunga mkono Mwigulu Nchemba. Tusijisahau, sisi ndiyo tumepewa dhamana ya kulinda umoja wa kitaifa”.

Uamuzi wa CCM kuamua kuendelea na vikao vya Bunge hilo unalalamikiwa na wananchi kuwa ni matumizi mabaya ya fedha za Watanzania maskini na wengine kumsihi Rais Jakaya Kikwete alivunje Bunge hilo mara moja.

Kuendelea kwa Bunge hilo kunaonekana kuigawa nchi katika makundi yanayohasimiana, hali inayotafsiriwa kuwa hata kama katiba itapitishwa, itakuwa vigumu kupigiwa kura ya ndiyo.

(Mwananchi)

Share: