Habari

CCM yafanisha Uamsho na majambazi

Na Thobias Mwanakatwe

10th June 2012

Chama cha Mapinduzi (CCM) kimekishukia Kikundi cha Uamsho kuhusiana na vurugu zilizotokea Visiwani Zanzibar na kukifananisha na majambazi.

Katibu wa Itikadi, Siasa na Uenezi, Nape Nnauye, alitoa kauli hiyo jana kwenye mkutano wa hadhara wa chama hicho uliofanyika kwenye viwanja vya Jangwani Jijini Dar es Salaam, mahususi kujibu makombora yaliyorushwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) dhidi ya serikali.

“Uamsho ni majambazi, na kwa kuwa serikali hii ni ya CCM, tunataka iwashughulikie kama inavyofanya kwa majambazi wengine bila kuwaangalia sura,”alisema Nnauye.

Nnauye alisema kikundi hicho kinapaswa kushughulikiwa kwani kitendo cha kuchoma makanisa hakina uhusiano na madai ya muungano.

Alisema chadema walipofanya mkutano katika eneo hilo walichangisha fedha wananchi lakini serikali ya CCM haiwezi kufanya hivyo na badala yake inapeleka maendeleo kwa wananchi na kuwafananisha wanachama wa CCM wanaohamia upinzani sawa na oil chafu.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Dar es Salaam, John Guninita, alisema lengo la mkutano huo ni kutoa majibu kwa wananchi kuhusu utekelezaji wa kero zinazowakabili na utaratibu huu utaendelea kufanya hivyo katika wilaya zote za mkoa wa Dar es Salaam.

Alisema mwezi Machi mwaka huu viongozi wa CCM mkoa walifanya ziara katika matawi 600 ya CCM na kubaini kero lukuki zizanowakabili wananchi.

“CCM mkoa wa Dar es Salaam kuna wanachama zaidi ya 400,000, hivyo leo CCM na serikali yake imekuja kutoa majibu ya kero zenu na namna zinavyoshughulikiwa,”alisema Guninita.

Alizitaja baadhi ya kero hizo kuwa migogoro ya ardhi, maji,msongamano wa magari,wananchi kutolipwa fidia na hali ngumu ya maisha.

Katika mkutano huo wananchi walifurika kuanzia saa 8.00 mchana ambapo wengi wao walitumia usafiri maalum wa daladala zilizokodiwa huku wengi wao wakitumia usafiri binafsi.

Eneo la viwanja vya Jagwani mbali ya kufurika kwa watu, magari yalikuwa ni mengi huku vikundi kadhaa vya kutumbuiza vikiongoza na bendi ya TOT vikitumbuiza.

Pia vijana kadhaa wanaodaiwa kutoka vyama vya upinzani walidhibitiwa pale walipoonyesha alama ya vidole viwili inayotumiwa na Chadema.

CHANZO: NIPASHE JUMAPILI

Share: