Habari

CCM ZANZIBAR WASHUTUMU TAASISI ZA DINI

CCM Zanzibar, kupitia Jumuiya zake, wameshutumu taasisi za Dini zinazofanya mihadhara kupinga mchakato wa Katiba na suala la mfumo wa Muungano.

Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Wazazi (CCM) Ame Mussa Silima, alisema taasisi hizo ambazo zimevaa ngozi ya chama kimoja cha siasa ambacho alikataa kukitaja jina, lengo lake kubwa ni kuleta chokochoko na kuhatarisha amani na utulivu.

Alisema taasisi hizo zinafahamika kwa muda mrefu, zina uhusiano na baadhi ya vyama vya siasa katika harakati zake za kupinga Muungano pamoja na Mapinduzi ya Zanzibar. Jumuiya hizo za CCM ni umoja wa vijana, Jumuiya ya wanawake na Jumuiya ya wazazi.

Aidha, amesema CCM wamechukizwa na kitendo cha taasisi hizo kwa kuandamana hadi Baraza la Wawakilishi kwa ajili ya kupeleka maombi kupinga Tume ya Rais ya mchakato wa kuundwa kwa Katiba mpya.

Silima, alisema wanafahamu muelekeo wa taasisi hizo ni wa vyama vya siasa, na ndio zinazolete chokochoko na kutaka kuona Serikali ya umoja wa Kitaifa, inasambaratika.

Mkutano huo wa viongozi wa CCM na waandishi wa habari, Naibu Katibu Mkuu Jumuiaya ya wanawake Zanzibar, Salama Aboud Talib, aliwataka wananchi kupuuza taasisi hizo za Dini pamoja na viongozi wake kwani wanataka kuwarudisha wananchi walikotoka, alisema na kuongeza:

“Hizi taasisi za dini viongozi wake ni wakorofi wanataka kuturudisha kule nyuma tunakotoka ambapo tulitawaliwa kwa vurugu na fujo za kisiasa,” alisema Salama.

Shutuma hizo zimekuja kufuatia hatua ya Kundi la Wazanzibari Asilia, kupeleka barua yao katika ofisi za Baraza la Wawakilishi kwa madai ya kutaka kufanyika kwanza kura ya maoni kuhusu mustakabali wa Zanzibar.

Akizungumza kwa ufupi baadae kiongozi wa kundi hilo Rashid Ali, alisema madai yao makubwa katika barua hiyo, wanataka iitishwe kura ya maoni katika suala la Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, alisema na kufafanua:

“kabla kuzungumzia kuwepo mjadala wa Katiba mpya, tunataka kwanza Wazanzibari, ipatikane ridhaa yetu kuhusu Muungano; Kura ya maoni ituulize Muungano tunautaka au laa, na kama ndio ni aina gani ya Muungano tunaoutaka, tuulizwe hivyo,” alifafanua Rashid.

Rashid alisema kundi lake linaungwa mkono na watu zaidi  300,000 na linasimamia madai ya kuwepo kwa taifa huru la Zanzibar.

Wakati huo huo imefahamika kuwa kesho Taasisi za Dini ya Kiislamu, zinazoongwa na Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu Zanzibar (JUMIKI) zitaendelea na Mihadhara yake kwenye uwanja wa Mpira wa Chukwani, karibu na Jengo jipya la Baraza la Wawakilishi.

Wazanzibari kutoka kila sehemu, waitikadi zote na dini zote, wanaombwa kufika kwa wingi, kunataarifa kuwa kesho kutakuwa na mambo makubwa na mazito yatakayo zungumzwa..

Share: