Habari

Chadema yajiandaa kutekeleza ‘Azimio la Zanzibar’

Dar es Salaam, Tz
Jumamosi, Februari 16, 2019

Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Vicent Mashinji amesema chama hicho sasa kinafanya uratibu na kupanga ratiba kwa ajili ya kuanza mikutano ya hadhara kama walivyoazimia katika ‘Azimio la Zanzibar.’

Dk Mashinji amesema hayo jana Februari 15 wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maazimio ya kikao cha kamati kuu ya chama hicho kilichoketi Februari 9 na 10 katika Hoteli ya Bahari Beach.

Rais John Magufuli, kiongozi mkuu wa nchi alipiga marufuku mikutano ya hadhara kwa vyama vya siasa na kuruhusu viongozi wa kuchaguliwa tu katika maeneo yao husika.

Rais Magufuli alitoa agizo hilo mwaka 2016 miezi michache baada ya kuingia madarakani ili katika kipindi chake ajikite zaidi kutimiza ahadi zake kwa maendeleo ya Watanzania wote.

Hata hivyo, agizo hilo limekuwa likipigiwa kelele na vyama vya upinzani na wadau wa demokrasia kote nchini wakidai kuwa ni agizo linalopingana na katiba na sheria, inagwa baadaye walilazimika kuliheshimu.

Mikutano ya hadhara iliyoruhusiwa ni ya wabunge katika majimbo yao ya uchaguzi na viongozi wa kitaifa wasiokuwa na majimbo wamejikuta njiapanda.

Ilifika hatua hata mikutano ya ndani ya wapinzani ikawa inavunjwa na polisi chini ya agizo hilo. Lakini, polisi hao hao wanaruhusu na kutoa ulinzi kwa mikutano ya ndani na ya hadhara ya viongozi wa CCM.

Kwa kawaida kiongozi wa nchi anaposema jambo linatakiwa kutekelezwa. Inawezekana likawa ni agizo linaloonekana kuwa kinyume cha sheria, lakini kwa busara hutakiwa kutekelezwa na ndiyo maana hata vyombo vya dola vinalazimika kusimamia agizo hilo.

Baada ya agizo hilo baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa waliachana na mikutano ya hadhara na kuhamia katika mikutano ya ndani na wale ambao walijaribu kwenda kinyume na agizo hilo waliingia matatizoni.

Hata hivyo, katika siku za karibuni wameonekana baadhi ya wanasiasa hasa kutoka chama tawala, ambao wameanza kukiuka agizo la rais na kufanya mikutano hadharani.

Hatua hii imeanza kuzua mjadala ni kwa jinsi gani viongozi hao wameamua kupuuza agizo hilo na hakuna hatua zinazochukuliwa tofauti na inapotokea kwa upande wa upinzani.

Mfano mdogo tu ni kitendo cha Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole kufanya mkutano wa hadhara mkoani Arusha mwishoni mwa wiki iliyopita.

Chadema kimesema kinafanya uratibu na kupanga ratiba ili kufanya mikutano ya hadhara nchi nzima kama walivyoazimia katika ‘Azimio la Zanzibar.’

Dk Mashinji amesema: “Tulikuwa na shughuli za kuimarisha chama na mambo mengine ya ndani ndiyo maana hatukufanya mikutano lakini sasa tunafanya maandalizi.”

“Mikutano ni haki ya kikatiba hata aliyeizuia alifanya utashi wake binafsi si kwa msukumo wa kisheria,” anasema Dk Mashinji.

Anasema vyama vya siasa vilijikuta vikitii amri isiyo halali kisheria na serikali ilijificha katika kichaka kuwa wapinzani wanatumia mikutano hiyo kuwatukana na kuwakashifu wakati hawafanyi hivyo kwa kuwa chama kina sera ambazo kinataka kuzieleza kwa wananchi.

Dk Mashinji ameongeza kuwa viongozi wa CCM sasa wanafanya mikutano ambayo serikali yao iliizuia lakini mikutano yenyewe imejikita katika kukejeli na kukashifu watu.

Share: