Habari

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimesema kuwa kimekwenda visiwani Zanzibar, kuwapelekea wananchi serikali ya tatu.

Kauli hiyo imetolewa jana visiwani humo na Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe, alipokuwa akizungumza na wazee wa jimbo la Uzini kabla ya kuzindua kampeni za kuwania ujumbe wa Baraza la Wakilishi.

Alisema CHADEMA inawataka Wanzanzibari waamue aina ya Muungano wanaoutaka tofauti na huu wa sasa ambao umezusha manung’uniko makubwa.

Aliongeza kuwa chama hicho kinaamini muundo wa serikali tatu yaani ile ya Tanganyika, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na Serikali ya Muungano.

Mbowe alisema wakazi wa Uzini wana kila sababu ya kukichagua CHADEMA kiwe chama mbadala kuwaletea maendeleo kwa kuwa tayari kwa sasa Chama cha Wananchi (CUF) na Chama cha Mapinduzi (CCM), vimefunga ndoa.

Alitolea mfano kuwa ajali ya meli iliyotokea Oktoba mwaka jana, wahusika wameshindwa kuchukuliwa hatua ikiwemo kufukuzwa kazi kutokana na vyama vyote hivyo viwili kulindana.

Alibainisha kuwa CHADEMA kimekwenda visiwani humo baada ya kubaini kuwa hakikuwekeza nguvu zake na matokeo yake ni kukosekana siasa za ushindani.

Kiongozi huyo wa kambi rasmi ya upinzani bungeni aliwataka wananchi kupuuza maneno na siasa chafu zinazosambazwa kuwa chama hicho ni cha dini fulani.

Aliongeza kuwa siasa hizo chafu zinatolewa kwa lengo la kuwatenganisha na chama hicho pamoja na kupandikiza mbegu za chuki.

Alibainisha kuwa malengo ya CHADEMA ni siasa na jamii si udini kama propaganda zinavyoenezwa kwa lengo la kuwasahaulisha wananchi madai yao ya kupatiwa huduma muhimu zikiwemo afya, elimu, maji na miundombinu.

“Nimekuja hapa kumuombea mtoto wenu kura na mtakapomchagua si kwamba ni kiongozi wangu bali ni wa kwenu na atawawakilisha na kuwatetea nyie atakapokuwepo kwenye Baraza la Uwakilishi,” alisema.

Naye, Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk. Willibrod Slaa awaligusia sakata la kuongezwa eneo la bahari linaloonekana kugonga vichwa vya vigogo wa pande mbili za Jamuhuri ya Muungano, akisema kuwa hata Bunge halikushirikishwa.

Kuhusu umaskini unaowakabili wananchi wa visiwa hivyo, Dk. Slaa alisema pamoja na Shirika la Maendeleo ya Mafuta nchini (TPDC), kugundua kuwa chini ya mikarafuu kuna uwezekano wa kupatikana mafuta, ugomvi mkubwa uliopo sasa ni kwamba nani atafaidika na mafuta hayo.

Alisema kiuhalisia Wazanzibari wanapaswa kufaidika na mafuta hayo kwa kuwa ni mali yao na izingatiwe kwamba yakiuzwa nje ya nchi yatawaletea maendeleo.

Kwa upande wake, mgombea ujumbe wa Baraza la Uwakilishi katika jimbo hilo kwa tiketi ya chama hicho, Ali Mbarouk Mshimba, aliahidi kuleta mabadiliko katika sekta ya elimu, huduma za afya na maji pindi akichaguliwa.

Mshimba alisema inasikitisha kuona kwamba lengo la hayati Abeid Karume, lililokuwa na lengo la kuwapatia elimu bure Wazanzibari, halijafikiwa na badala yake elimu imekuwa ni gharama na nyumba za gharama nafuu alizoahidi hawana uhakika kuzipata.

Uchaguzi wa jimbo la Uzini unakuja baada ya kifo cha aliyekuwa mbunge wake, Musa Khamis Silima (CCM).

Share: