Habari

CHADEMA: Zanzibar Imedhalilishwa

Na Janet Josiah – TanzaniaDaima

03/10/2014

CHAMA CHA Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimesema kilichofanyika katika Bunge Maalum la Katiba (BMK) jana, kimewadhalilisha Wazanzibari.

Wakati CHADEMA ikisema hivyo, Chama Kikuu cha Upinzani Zanzibar, CUF, nacho kimesema CCM imejidhalilisha na kwamba hiyo itakuwa hukumu yao katika uchaguzi mkuu mwakani na ule wa serikali za mitaa.

Akizungumza na Tanzania Daima jana, Naibu Katibu Mkuu CHADEMA-Zanzibar, Salum Mwalim alisema baada ya wajumbe wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuandaa katiba yao, amepanga kushirikiana na viongozi wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), kuzunguka Unguja na Pemba kwa ajili ya kuwaambia Wazanzibari waikatae Katiba iliyopendekezwa utakapofika wakati wa kura za maoni.

Mwalim alisema Katiba iliyopendekezwa haikuja na mapendekezo ya Wazanzibari, hivyo wanapaswa kuikataa.

“Katika mapendekezo hayo ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hakuna hata pendekezo moja la Wazanzibari lililowekwa…nawataka Wazanzibari wayakatae mapendekezo hayo katika kura za maoni zitakazoitishwa,” alisema Mwalim.

Alisema kwa kuwa Katiba ya Zanzibar ya mwaka 2010 iliyofanyiwa marekebisho inatambua kuwa sheria yoyote inayopendekezwa katika Katiba lazima ipigiwe kura za maoni, sasa watazungumza kupitia kura za maoni na si vinginevyo.

Naibu Katibu Mkuu huyo, aliwataka watanzania bara kushirikiana na Wazanzibari kuikataa Katiba iliyopendekezwa kwa sababu imependekezwa na wajumbe wa CCM na siyo wawakilishi wa makundi na vyama vyote.

Na katika hatua nyingine, Naibu Katibu Mkuu huyo, alimpongeza Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar, Othman Masoud Othman kwa kuitumia taaluma yake vizuri kukataa vifungu vyote vya Katiba iliyopendekezwa.

“Natumia fursa hii kwa moyo wa shukrani kumpongeza Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar…si tu kwa kuitumia vizuri taaluma yake…bali ameonyesha kujali maslahi ya kwao…ujasiri wa hali ya juu wa kiongozi aliyejitambua na kujua mahitaji ya nchi yake,” alisema Mwalim.

Mwalim alisema kitendo kilichofanywa na Mwanasheria Mkuu huyo cha kusimama kidete kwa maslahi ya Zanzibari, kinapaswa kuigwa na Wazanzibari wote hasa vijana, bila kujali umri, dini na itikadi kwa ajili ya maslahi mapana ya nchi yao.

Alisema CHADEMA Zanzibar, iko upande wake na itaendelea kutangaza ujasiri na utashi wa nchi yake popote watakapokwenda, ili aendelee kuwa mfano wa kuigwa kwa Wazanzibari wengine walioko upande wa CCM, lakini hawana maslahi na nchi yao.

Pamoja na hayo, Mwalim alisema chama chake sasa kinajipanga kuzunguka nchi nzima ili kuwaeleza wananchi kilichotokea bungeni, lakini pia kuwaeleza nini wafanye katika kura ya maoni ya Katiba iliyopendekezwa.

Kwa upande wake, Naye Mkurugenzi wa Habari na Mahusiano ya Umma wa CUF, Salim Bimani alisema walichokifanya CCM ni kujidhalilisha na kwamba hiyo itakuwa ndio hukumu yao kwa kuadhibiwa mwaka 2015 katika Uchaguzi Mkuu na hata Serikali za Mitaa.

Alisema CCM imethubutu kutumia nguvu kubwa na mabavu katika kufanikisha agenda yao ya kuwavuruga wananchi kwa kuitupa rasimu ya Jaji Warioba na kuingiza wanayoitaka wao, kitendo ambacho hakitakubalika hata siku moja.

Bimani alisema kuwa wao waligundua tangu awali na ndio maana wakatoka ndani ya bunge hilo na kwamba baada ya CCM kupitisha rasimu wanayoitaka, wao hawaitambui na wanawangoja kuwahukumu kwa wananchi.

“Sisi tunawataka wananchi watulie…lakini wawaadhibu CCM kwenye uchaguzi mkuu na hata kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa…kwa kuwa wamefanya kitu kinyume na makubaliano na wamevunja sheria ya kuandaa katiba hiyo kama ilivyokuwa imepangwa hapo awali,” alisema Bimani.

Aliongeza: “CCM inatufanya sisi hatuna akili kabisa na kwamba walichokifanya hukumu yake ni mwaka 2015 na watakosa kura kwa wananchi…hivyo sasa wamejipalia makaa ya moto kwa kuwa watadharauliwa kwa wananchi na mataifa yote kwa kile walichokifanya.”..

Share: