Habari

CUF: Ahadi ya JK ‘changa la macho’

Na Julius Mathias, Mwananchi

Alhamisi,Januari15 2015

Dar es Salaam. Chama cha Wananchi (CUF) kimekosoa ahadi ya Serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya kuanza kutoa elimu bure nchi nzima kuwa ni propaganda za kuelekea Uchaguzi Mkuu.

Katika waraka uliotumwa kwa vyombo vya habari na Naibu Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa chama hicho, Abdual Kambaya unaeleza kuwa haiwezekani Rais atoe ahadi ambayo haijajadiliwa na kupitishwa na chama chake kama sehemu ya malengo yatakayotekelezwa.

“Kitendo cha CCM kutangaza kufuta ada ya elimu ya msingi na sekondari ni changa la macho kwa Watanzania. Hii siyo mara ya kwanza kwa CCM kutoa ahadi ya elimu bure.

Alifafanua kuwa michango iliyoshindwa kuondolewa imeendelea kuwapo hadi leo bila ya dalili yoyote ya utekelezaji. Alisema licha ya kushindwa kufuta ada, michango inayoendelea kutozwa ni mingi na inazidi kwa kiasi kikubwa ada inayotozwa.

Rais Kikwete alitoa ahadi hiyo mwishoni mwa wiki iliyopita mbele ya mabalozi wa nchi mbalimbali katika karamu aliyoindaa Ikulu kwa ajili ya kuukaribisha mwaka 2015, huku Rais wa Zanzibar, Dk Mohammed Shein naye akitangaza mpango huo wakati wa sherehe za Mapinduzi ya Zanzibar.

Rais Kikwete alisema hatua hiyo inakuja baada ya Serikali kukamilisha Sera ya Elimu na Ufundi ili kuboresha sekta hiyo ambayo imepitishwa na Baraza la Mawaziri katika mkakati wa kuhakikisha kila Mtanzania anapata elimu kwa gharama itakayobebwa na Serikali.

Chama tawala kimetangaza azma hiyo ikiwa ni miaka 10 baada ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kubainisha kuwa hiyo ni moja ya mikakati yao ifikapo mwaka huu kama wangechaguliwa kuongoza dola.

“Bado kuna michango mbalimbali kama vile ya taaaluma, rim za karatasi, ulinzi, madawati, tahadhari, mtihani, mafunzo ya ziada, vitabu na nyingine nyingi. Ukijumlisha michango yote inazidi laki nne na bado pamoja na hali hii Serikali ya CCM inaibuka na kusema elimu itakuwa bure wakati utekelezaji wa kufuta michango hiyo shuleni bado ni kizungumkuti,” alisema Kambaya.

Chama hicho kimesema kilitegemea suala la elimu bure lingejadiliwa na kuwekwa kwenye maadhimio yaliyojadiliwa na kikao cha Kamati Kuu ya CCM kilichohitimishwa mjini Unguja jana ili kuonyesha kuwa ni huo mkakati wa kichama.

Mwananchi

Share: