Habari

CUF INALAANI NA KUPINGA KUFUNGIWA

CUF INALAANI NA KUPINGA KUFUNGIWA
KWA GAZETI LA THE CITIZEN;

THE CIVIC UNITED FRONT
(CUF –Chama Cha Wananchi)

TAARIFA KWA UMMA

THE CIVIC UNITED FRONT (CUF-Chama Cha wananchi) kinalaani na kupinga kufungiwa/kusimamisha leseni ya uchapishaji na usambazaji pamoja na mtandao wa gazeti hilo kwa siku saba kuanzia Tarehe 27/2/2019 kwa gazeti la THE CITIZEN, linalotolewa kila siku na kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL). Uamuzi huo uliotolewa na Idara ya Habari (Maelezo) unatokana na madai ya gazeti hilo la Kiingereza kuandika habari iliyohusu maoni ya wataalamu walioelezea kuporomoka kwa shilingi ya Tanzania na kuchapishwa Februari 23, 2019.

“Uamuzi wa kusimamisha kwa muda leseni hiyo unatokana na mwenendo na mtindo wa habari na makala ambao kwa kiasi kikubwa unakiuka misingi ya maadili ya taalamu ya habari kwa upotoshaji wa mara kwa mara wa taarifa zinazohusu Serikali na uchochezi bayana unaokiuka masharti ya leseni,” imeeleza sehemu ya aya katika barua hiyo kutoka Idara ya Habari Maelezo.

THE CIVIC UNITED FRONT (CUF-Chama Cha Wananchi), kimesikitishwa na kulaani mwenendo wa serikali ya awamu ya tano kuingilia na kubana uhuru wa habari ambazo ni ukweli usiopingika kuwa SHILINGI YA TANZANIA imezidi kuporomoko siku hadi siku kutokana na kuharibiwa kwa mfumo wa uchumi nchini.

CUF inaungana na watanzania wote wapenda HAKI, AMANI, UHURU, DEMOKRASIA, NA USTAWI WA WANANCHI kulaani na kupinga vitendo na mwenendo huu usiofaa wa serikali kuingilia uhuru, kuwatisha na kujenga jamii yenye hofu na woga dhidi ya serikali yao isiyotaka kupokea fikra mbadala katika kuleta ustawi mwema wa Taifa. Tunaitaka Serikali ilifungulie Gazeti hilo na iwache mtindo wa kufungia vyombo vya habari kama njia ya kutaka kunyamazisha maoni yasiyowafurahisha watawala.

HAKI SAWA KWA WOTE

MBARALA MAHARAGANDE
NAIBU MKURUGENZI WA HABARI

maharagande@gmail.com
+225 715062577 / +255 767062577

Imetolewa Leo Tarehe 28/2/2019

Share: