Habari

CUF, Msajili vitani

Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi

***Upande wa Maalim Seif waahidi kumpeleka mahakamani
***Mutungi asema huko ndiko haswa mahali pake

Rahma Suleiman – Nipashe
04 Oktoba 2016

WAKATI Bodi ya Wadhamini ya Chama cha Wananchi (CUF), jana ilikutana Zanzibar na kutoa maazimio sita likiwemo la kukusudia kumshtaki mahakamani Msajili wa Vyama vya Siasa kwa kuingilia maamuzi halali ya CUF.

Jaji Francis Mutungi amesema wanaweza kuchukua hatua hiyo kama hawakuridhika na maamuzi yake ya kumtambua mwenyekiti Profesa Ibrahim Lipumba.

Bodi hiyo ilisema itamshtaki Jaji Mutungi kwa sababu alichokifanya ni sawa na kukichagulia chama hicho mwenyekiti kinyume na hukumu iliyowahi kutolewa na Mahakama Kuu.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, mwenyekiti wa bodi ya CUF, Abdallah Said Hatau alisema bodi hiyo imepuuza wito wa Prof. Lipumba ambaye alitaka kuitishwa kwa kikao cha bodi ya wadhamini wa chama hicho.

Jaji Francis Mutungi jana aliwataka viongozi na wanachama wa CUF kwenda mahakamani kama hawakubaliani na uamuzi wake wa kumrudisha ofisini Lipumba.

Profesa Lipumba alijiuzulu Agosti 5, mwaka jana akidai dhamira yake inamsuta kuendelea kukalia kiti baada ya chama hicho kukubali kumpitisha Waziri Mkuu wa zamani Edward Lowassa kuwa mgombea wake wa urais chini ya mwamvuli wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).

“Bodi itaendelea kuheshimu maamuzi ya baraza kuu la uongozi taifa likiwa ndiyo chombo chenye dhamana ya kusimamia uongozi na uendeshaji wa chama,” alisema Hatua akirejea maamuzi ya baraza hilo ya kumfukuza uanachama Lipumba mwishoni mwa mwezi uliopita.

CUF ilidai kumfukuza Lipumba kwa tuhuma za kufanya fujo katika ofisi kuu ya chama Buguruni, Dar es Salaam ambako aliingia ofisini kwa nguvu baada ya mashabiki wake kuvunja geti na milango.

Bodi hiyo imewahakikishia wanachama wote wa CUF wa Tanzania Bara na Zanzibar kwamba ipo makini na itasimama pamoja nao kulinda mali za chama.

Aidha, chama hicho kimemtaka msajili wa vyama vya siasa aache kuingilia mambo ya ndani ya uongozi na uendeshaji wa chama hicho.

Azimio lingine la bodi hiyo ni kumtaka Prof. Lipumba kulipa gharama za hasara zote zilizosababishwa na kuvamia mkutano mkuu maalumu wa taifa wa chama hicho uliofanyika Agosti 21 mwaka huu Dar es Salaam. CUF ilidai kupata hasara ya Sh. milioni 650 kwa tukio hilo.

MSIJE OFISINI
Licha ya Baraza Kuu la Uongozi Taifa la CUF kutangaza kumfuta uanachama, Jaji Mutungi alimrejeshea uenyekiti Prof. Lipumba kwa sababu barua yake ya kujiuzulu haikujadiliwa katika kikao sahihi.

Akizungumza na Nipashe kwa simu jana, Jaji Mutungi alisema kama viongozi na wanachama wa CUF wanaona hajawatendea haki kutokana na uamuzi wake huo, wanapaswa kwenda kudai haki hiyo mahakamani badala ya kukimbilia kwenye vyombo vya habari.

“Siwezi kufanya kazi kwa shinikizo la media (vyombo vya habari) wala msije ofisini kwangu, tuhuma zote za CUF nazijua, kama wanaona wanaonewa waende mahakamani,” alisema Mutungi.

Jaji Mutungi alitoa kauli hiyo baada ya kuulizwa na gazeti la nipashe kuhusu tuhuma zilizoelekezwa kwake jana na Mwenyekiti wa Uongozi wa CUF, Julius Mtatiro, aliyedai kuwa Jaji huyo anatumika kukivuruga chama hicho.

Katika mkutano huo na waandishi wa habari uliofanyika jana Dar es Salaam, Mtatiro alisema msajili wa vyama vya siasa na Prof. Lipumba wamekuwa wakifanya vikao vikiwa na lengo la kuivuruga CUF.

Mtatiro alisema kumekuwapo na vikao vya mara kwa mara kati ya Jaji Mtungi na Lipumba, lakini uongozi wa CUF umekuwa ukipata taarifa zote za vikao hivyo.

Alisema Septemba 15 wabunge wa CUF wakiwa mjini Dodoma walizungumza na waandishi wa habari juu ya mikakati ya Jaji Mutungi kutaka kumrejeshea Prof. Lipumba uenyekiti, jambo ambalo lilitokea siku chache mbele.

Mtatiro alisema utafanyika utaratibu wa kumwondoa Prof. Lipumba katika ofisi za CUF kwa utaratibu uliostaharabika.

Alisema Katibu Mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad atakwenda katika ofisi hizo pindi hali ya usalama itakapotengemaa.

“Muda mwafaka ukifika tutakwenda ofisini, ofisi kuu ya chama imetekwa, lakini makao makuu ya chama yako salama, kwa sasa operesheni za chama zinaendelea kama kawaida ingawa hatupo ofisini,” alisema Mtatiro.

Share: