Habari

CUF – WAMNG’ANG’ANIA RAZA

Talib Ussi – Zanzibar.

MGOMBEA wa Chama  Cha Wananchi (CUF) katika uchaguzi mdogo wa Jimbo la Uzini, Unguja Salma Hussein Zarali, amekata rufaa katika Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) kupinga uamuzi uliotolewa na ofisi ya tume ya wilaya hiyo kuhusu mgombea wa CCM Mohamed Raza.

Mgombea huyo wa CUF alikuwa amewasilisha katika ofisi hiyo, pingamizi la kutaka Raza  aondolewe katika kinyang’anyiro hicho kwa madai kuwa amekosa sifa za kumwezesha kugombea. Salma alitoa msimamo huo jana, alipokuwa akizungumza na mwandishi wa habari hii, huko  Uzini.

Mgombea huyo wa CUF alisisitiza kuwa Raza amevunja sheria ya  uchaguzi namba 46  kifungu kidogo 3 (a) na kuitaka tume itumie kifungu cha 44 (4) kumwengua.

Alidai kuwa mgombea yeyote wa nafasi ya uwakilishi wa jimbo, anapaswa kula kiapo mbele ya hakimu wa mkoa, lakini Raza amekula kiapo chake mbele ya hakimu wa wilaya. “Sisi  tunaenda mbele zaidi kudai haki yetu ya msingi dhidi ya mgombea huyu ambaye kimsingi  hastahiki kugombea kwa kuwa amekiuka sheria,” alisema  Salma.

Jana ofisi ya Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar katika Wilaya ya Kati ilitupilia mbali pingamizi zilizowasilishwa na  CUF na Chadema dhidi ya Raza, kwa maelezo kwamba kisheria madai yao hayana msingi.

Lakini Salma alisema ikiwa NEC itaendelea kumbeba Raza, CUF watakwenda mahakamani kuomba uchaguzi usitishwe hadi sheria zitakapofuatwa.“ Kama tume wataendelea na msimamo wa wao, sisi tutakwenda kudai haki mahakamani,” alisisitiza Salma..

Share: