BarazaniHabari

CUF wamtege Lipumba kwa maswali 8

Profesa Ibrahim Lipumba

Mary Geofrey – Nipashe
18 June 2016

SIKU Chache baada ya aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba kuandika barua ya kutengua uwamuzi wake kujiengua nafasi hiyo, uongozi wa CUF umemtaka atoe ufafanuzi wa maswali manane.

Lipumba aliandika barua ya kujiengua nafasi hiyo Agosti 5, mwaka jana ambapo Juni 13, mwaka huu pia alitangaza kutengua uamuzi huo ambao umepingwa vikali na uongozi wa chama hicho akiwamo Katibu Mkuu, Maalim Seif Sharif Hamad.

Akizungumza na waandishi wa habari jana Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi ya CUF, Twaha Taslima alisema baada ya Lipumba kutaka kurudi kwenye nafasi yake wafuasi na wanachama wamekuwa wakijiuliza maswali ambayo wanayaelekeza kwake.

Alitaja moja ya swali kuwa ni kutaka kufahamu sababu ya msingi iliyomsababisha Profesa Lipumba aandike barua ya kujiuzulu nafasi ya uongozi Agosti 5, 2015.

Taslima alisema pia wanachama wanataka kufahamu sababu zilizomuondoa kwenye nafasi yake na kama zimeshapatiwa ufumbuzi na ikiwa bado, je hazitatokea tena ndani ya chama hicho.

Swali la tatu lililoelekezwa kwa Profesa Lipumba ni kuwa, kama sababu hizo hazipo kwa sasa, na kama zikijitokeza tena, atachukua tena uamuzi wa kujiuzulu kama alivyofanya awali ama la?.

Taslima alisema swali lingine wanalotaka kupata majibu kutoka kwa Profesa Lipumba ni kwa nini alikaa nje ya chama kwa miezi kumi na kuamua kurudi kipindi hiki.

Taslima alitaja swali la tano lililoelekezwa kwa Lipumba kuwa ni je, kama anadhani madai ya kutojibiwa kwa barua yake ya kujiengua nafasi yake, aliyompelekea Maalim Seif (Katibu Mkuu) ndiyo msingi wa hoja yake ya kurudi katika nafasi ya uenyekiti au la, na je, hajui kama Mkutano Mkuu wa Taifa haukuhitajika kufanyika kwa ajili ya jambo hilo?.

Alisema vilevile kuwa uongozi huo, haukuacha kuhoji kwamba, wajumbe walioteuliwa na Baraza Kuu la Uongozi la Taifa kuunda Kamati ya Uongozi wataenda wapi, baada ya yeye kuamua kujirudishia uongozi.

Pia, walihoji kuwa Lipumba anadhani kuwa yeye ni mkubwa kimamlaka kuliko Baraza Kuu hadi afikie hatua kutoheshimu uwamuzi wa Baraza.

Swali la nane ambalo lilielekezwa kwa Lipumba, ni je ametumia kipengele kipi cha katiba katika Ibara 117 kufanya uamuzi wa kujirudishia uenyekiti wa taifa.

“Maswali haya tumeshindwa kuyajibu kwa ufasaha. CUF inapenda kuchukua nafasi hii kumuomba Lipumba asijaribu kukiyumbisha Chama katika kipindi hiki ambacho nchi ina matatizo makubwa na Watanzania wanahitaji kuwekwa pamoja na kupewa matumaini,” alisema Taslima.

Profesa Lipumba ‘kibarua kigumu’ CUF..
Wakati huo huo, Fidelis Butahe na Sharon Sauwa wa Gazeti la Mwananchi wameandika kwamba, Chama cha Wananchi kimemtaka Profesa Lipumba kutojaribu kukiyumbisha chama katika kipindi hichi ambacho nchi ina matatizo lukuki.

Kauli hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi CUF Taifa, Twaha Taslima imekuja baada ya Profesa Lipumba ambaye alijiuzulu Agusti 5, mwaka jana kutengua uwamuzi wake wa kung’atuka na kuomba kurejea kuendelea kuwa Mwenyekiti wa CUF.

Taslima ambaye amethibitisha kuwa atagombea uwenyekiti wa CUF katika uchaguzi unaotarajiwa kufanyika Agosti 21 mwaka huu, amesema wanachama wa chama hicho wanajiuliza maswali mengi baada ya uamuzi huo wa Lipumba.

Amesema hakuna kipengele cha Katiba ya CUF kinachosema, Mwenyekiti akijiuzulu anaweza kusitisha mpango huo na kurejea tena katika wadhifa wake.

“Hakuna kipengele cha Katiba ya CUF kinachosema Mwenyekiti akijiuzulu anaweza kusitisha mpango huo na kurejea katika wadhifa wake…Ombi la Lipumba halitekelezeki,” alisisitiza Taslima..

Share: