Habari

CUF yasema itakapo ingia ikulu haitolipiza kisasi kwa CCM

Zanzibar,

Chama cha wananchi CUF kimesema kuwa iwapo kitaingia ikulu ya Zanzibar mwezi oktoba mwaka huu hakitolipiza kisasi kwa CCM na badala yake kitatoa fursa kwa wananchi kufanya shughuli zao bila ya kubaguliwa nakupewa usumbufu wowote.

Hayo yameelezwa na katibu mkuu wa chama hicho Maalim Seif hamah alipokuwa akizungumza na wazee wa chama hicho kutoka wilaya sita za unguja huko hoteli ya bwawani Zanzibar, ambapo pia mwenyekiti wa kamati ya maridhiano, Mzee Hassan Nassor Moyo wa CCM alihudhuria.

Maalim Seif ambaye pia ni makamu wa kwanza wa rais wa Zanzibar amesema kuwa binafsi neno ‘kisasi’ amelifuta kabisa, na amewataka wana CUF wenye mawazo kwamba chama hicho kikiingia ikulu itakuwa zamu yao ya kutesa kusahau hilo.

Ameongeza kuwa CUF kitaangalia mbele na wala hakitafukua makaburi, kitasimamia usawa hakutakuwa na ubaguzi katika ajira kwa misingi yoyote ile, na kila mmoja atatembea kifua mbele ili ajione ni mzanzibari sawa na mwengine.

Amesema kuwa ni jukumu la wazee wa chama hicho kuwaongoza vijana katika kuhakikisha CUF inapata ushindi mkubwa usiopungua asilimia 75 katika uchaguzi mkuu ujao, kutokana na chama hicho kuwa tegemeo la wazanzibari katika kuwaletea ukombozi.

Katibu mkuu huyo amesema kuwa mwaka 2015 ni mwaka wa uamuzi kwa wazanzibari kuhusu musatakabali wa nchi yao, hivyo amewataka wananchi kujipanga kukipa ushindi wa kihistoria chama hicho ili kiweze kushika dola bila ya kikwazo chochote na kisimamie matarajio yao.

Amesema kuwa dalili za ushindi wa kihistoria kwa CUF 2015 zinaonekana wazi kwa namna wazanzibari wanavyokikubali chama hicho siku hadi siku, baada ya kujidhihirisha ndicho pekee chenye nguvu na uwezo wa kupigania maslahi ya wazanzibari na nchi yao.

Alieleza kuwa wananchi wengi wa Zanzibar hivi sasa wamekielewa na wanakikubali CUF, na hata katika yale maeneo ambayo kilikuwa na upinzani mkubwa, kufikia hatua ya viongozi wa CUF kupigwa mawe na kuzomewa, hivi sasa viongozi hao wakipita wanalindwa na wananchi wa maeneo hayo.

Wakizungumza katika mkutano huo waasisi wa chama hicho, Mzee Ali Haji Pandu na Mzee Machano Khamis Ali wametoa wito kwa wananchi wa Zanzibar kumpa nguvu na kuzidi kumuunga mkono katibu wa CUF Maalim Seif Sharif Hamad katika kutetea hadhi na heshima ya Zanzibar.

Kwa upande wake, Mzee Hassan Nassor Moyo amesema kuwa Maalim Seif ni kiongozi jasiri mwenye azma ya dhati isiyotetereka katika kuhakikisha Zanzibar inabaki katika utulivu na wananchi wake wanakuwa wamoja.

Mzee Moyo amesema kuwa kamati ya maridhiano pamoja na wananchi wote wa Zanzibar hawawezi kukubali kuiona Zanzibar iliyotulia inaingizwa katika matatizo mengine ya mifarakano na baadhi ya viongozi wanaopigania maslahi binafsi ambao wanatamani serikali ya umoja wa kitaifa kuvunjika.

Share: