Habari

CUF yatangaza wagombea majimbo 50 Zanzibar

Zanzibar. CUF imetangaza majina ya wagombea waliopendekezwa kuwania ubunge na uwakilishi Zanzibar katika majimbo 50, likiwamo jina la kada wa CCM, Mohamed Hashim Ismail.

Wakati Ismail akitangazwa kuwania nafasi ya uwakilishi wa Jimbo la Dimani kwa tiketi ya CUF, Chadema imepewa jimbo moja.

Kuondoka kwa Ismail ni pigo jingine kwa CCM ambayo katika siku za karibuni imekuwa ikipoteza wanachama wake waandamizi, akiwamo Hassan Nassor Moyo ambaye alivuliwa uanachama kwa madai ya kukiuka taratibu za chama.

Kupitishwa kwa majina ya majimbo 50 ya Unguja na Pemba, ni baada ya kikao cha Kamati ya Utendaji ya Taifa ya CUF kilichofanyika chini ya mwenyekiti wake, Maalim Seif Sharif Hamad.

Kwa mujibu wa mapendekezo hayo, majina matatu yamependekezwa kupigiwa kura ya maoni ngazi ya jimbo kwa kila jimbo na wilaya kwa wagombea wa nafasi za viti maalumu, ili kupata mgombea mmoja kabla ya kufanyika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.

Mkurugenzi wa mipango na uchaguzi wa CUF, Omar Ali Shehe aliwaambia waandishi wa habari katika mkutano uliofanyika ofisini kwake Vuga jana, kuwa wanachama 517 walijitokeza kuwania ubunge, wakati 242 wanataka uwakilishi na 67 ni viti maalumu, huku waandishi wa habari wanne wakifanikiwa kupenya katika hatua ya kwanza ya mchujo ya kutafuta wagombea.

Waandishi hao wa habari, ni aliyekuwa mtangazi wa BBC, Ali Saleh ‘Alberto’ (Mji Mkongwe), Maua Mohamed Mussa (Tanzania Daima) ambaye anawania nafasi za viti maalumu Wilaya ya Mjini, Talib Ussi (Mwananchi) anawania ubunge wa Jimbo la Mgogoni na Mwajuma Juma Kombo (Majira) anayewania uwakilishi wa jimbo la Amani.

Mkurugenzi huyo alisema mchakato huo umefanyika kwa umakini wa hali ya juu, ili kuhakikisha wanapatikani watu wenye sifa na uwezo wa kuingia katika vyombo hivyo viwili vya kutunga sheria.

“Tumeamua kutangaza majina ya wagombea kabla ya Tume ya Uchaguzi kumaliza kazi ya kukata mipaka mipya ya majimbo ya uchaguzi. Hii inatokana na wenzetu (Tume ya Uchaguzi, Zec) kupoteza mwelekeo. Wameshindwa kutangaza mipaka tangu Machi mwaka huu,” alisema Omar Ali Shehe.

Alisema mabadiliko yoyote yatakayotokea, chama hicho kitaamua kulingana na mazingira halisi, lakini CUF ni chama cha siasa kina ratiba yake na lazima itekelezwe kwa wakati mwafaka na kama mtu hayupo tayari kuendelea na safari ni bora kutangulia kuliko kumngoja.

Wakati hayo yakitokea, wagombea watatu wa CUF wamepita bila ya kuwa na wapinzani. Wagombea hao ni Ismail Jussa (uwakilishi Mji Mkongwe), Mansour Yusuph Himid (uwakilishi Kiembesamaki) na Khamis Msabah Mzee (ubunge Jimbo la Dole).

Pia, CUF haijasimamisha mgombea ubunge katika Jimbo la Kikwajuni na badala yake imekiachia Chadema ambayo itamsimamisha naibu katibu mkuu wake upande wa Zanzibar, Salum Mwalimu ikiwa ni utekelezaji wa makubaliano ya vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) ya kuachiana majimbo.

Mbali ya CUF na Chadema, vyama vingine ni NCCR-Mageuzi na NLD.

“Kwa upande wa urais (wa Zanzibar), tumekubaliana Maalim Seif Sharif Hamad ndiye atakayesimama kwa tiketi ya Ukawa. Jimbo la Kikwajuni tumewaachia Chadema,” alisema Omar Ali Shehe.

Mawaziri wa CUF wanakabiliwa na upinzani mkubwa katika majimbo yao, baada ya kupitishwa watu wanaowapinga kabla ya kwenda kupigiwa kura ya maoni na wanachama katika majimbo husika.

Waziri wa Katiba na Sheria, Abubakar Khamis Bakari anachuana na Amour Said Mohamed na Suleiman Mohamed Khalfan wanaowania Jimbo la Mgogoni, wakati waziri asiyekuwa na wizara maalumu, Haji Faki Shaali anachuana na Mohamed Khatib Mikidadi na Tahir Aweis mohamed katika Jimbo la Mkanyageni kisiwani Pemba.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, Fatma Abdulhabib Ferej amepata upinzani katika viti maalumu Wilaya ya Mjini akichuana na Nunuu Salim Rashid na Rahma Mohamed Ibrahim Sanya.

Pia, Waziri wa Viwanda, Biashara na Masoko, Nassor Ahmed Mazrui anatarajiwa kuchuana vikali na Mussa Haji Jadi katika Jimbo la Mtoni, huku Waziri wa Mifugo na Uvuvi Abdillahi Hassan Jihad akipata upinzani kutoka kwa Said Abdallah Juma na Mohamed Ali Amour katika Jimbo la Magogoni kisiwani Unguja.

Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo, Said Ali Mbarouk naye amepata upinzani kutoka kwa Ali Yusuph Abdallah na Kassim Hamad Nassor wanaowania Uwakilishi katika Jimbo la Gando, wilayani Wete, Pemba.

Waziri wa Miundombinu na Mawasiliano na Makamu Mwenyekiti wa CUF Zanzibar, Juma Duni Haji ameamua kujitokeza katika Jimbo la Bububu akiwania nafasi ya uwakilishi na atachuana na Ali Juma Khamis.

Naibu Waziri wa Ardhi, Maji, Makazi na Nishati, Haji Mwadini Makame atapambana na Hassan Jani Masoud na Haji Maulid Machano katika Jimbo la Nungwi, Pemba wakati Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Zahra Ali Hamad akichuana na Lutfiya Kassim Juma na Hassina Ali Matar katika nafasi za viti maalumu Wilaya ya Magharibi, Unguja.

Jina la mwanasiasa mkongwe, Mussa Haji Kombo limekatwa katika kinyang’anyiro cha ubunge wa Jimbo la Chakechake, Pemba wakati Waziri wa Afya, Rashid Suleiman Seif ameamua kupumzika na nafasi yake ya uwakilishi wa Jimbo la Ziwani inawaniwa na mtangazaji wa zamani wa Sauti ya Tanzania Zanzibar (STZ) Najma Khalfan Juma ambaye pia anawania nafasi ya viti maalumu wilayani ChakeChake pemba.

Mkurugenzi wa ZEC, Salim Ali Kassim alisema tume hiyo itaendelea na utaratibu wa kukata mipaka ya majimbo licha ya CUF kutangaza majina ya wagombea wake katika majimbo ya sasa.

“Kwa mujibu wa sheria, tume imepewa mamlaka ya kutangaza majimbo, maeneo ya uchaguzi na vituo vya kupigia kura kabla ya Uchaguzi Mkuu na kutangaza katika gazeti rasmi la Serikali. Uchaguzi wa 2005 tulitangaza majimbo Juni, mwaka huu ndiyo kwanza mwezi wa tano, hivyo bado hatujachelewa,” alisema mkurugenzi huyo.

mwananchi

Tagsslider
Share: