Habari

DC aagiza barabara mashimo ya mchanga itengenezwe

January 21, 2019

MASANJA MABULA, PEMBA

MKUU wa Wilaya ya Micheweni, Salama Mbarouk Khatib, amezishauri wizara ya kilimo, halmashauri ya wilaya hiyo na wizara ya fedha, kuifanyia matengenezo barabara inayokwenda kwenye mashimo ya mchanga ya Shumba Vyamboni, ili iweze kupitika.

Alisema ubovu wa barabara hiyo umesababisha kupungua mapato ya serikali baada ya baadhi ya gari za mizigo kusitisha kuchukua mchanga.

Akizungumza baada ya kufanya ziara ya kuitembelea barabara hiyo, alielezea kutoridhishwa na hali ya barabara hiyo na kuzipa siku saba taasisi hizo kuifanyia matengenezo ya haraka ili kudhibiti mapato ya serikali.

“Natoa muda wa siku saba barabara hii iwe imefanyiwa matengenezo ili iweze kupitika vyema na kuondosha usumbufu wanaoupata madereva kwani wanachangia mapato ya serikali,”alisema.

Aidha katika hatua nyenegine, aliziagiza taasisi hizo kushirikiana na wizara mawasiliano, kuangalia uwezekano wa kutoa zana kwa ajili ya matengenezo hayo.

Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Micheweni, Suleiman Juma Pandu, aliziomba taasisi hiyo kushirikiana kuifanyia matengenezo kwani fedha zinazokusanywa katika mashimo hayo ni nyingi ikilinganishwa na gharama ambazo zinahitajika kuifanyia matengenezo.

Alisema kila taasisi ambayo inaguswa na mapato yatokanayo na mashimo hayo, inapaswa kuchangia ili kufanikisha matengenezo ya barabara hiyo.

Mwakilishi wa Ofisa Mdhamini Wizara ya Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi, Hamad Omar, alisema mapato yanayokusanywa katika mashimo hayo yanapelekwa wizara ya fedha na sio wizara ya kilimo.

Kwa upande wao, madereva wa gari za mizigo, waliziomba taasisi husika kuitengeneza haraka barabara hiyo kwani ni moja ya sehemu ambayo inaingiza mapato.

Mmoja wa madereva hao, Mustafa Saleh, anayeendesha gari Z150 GT, alisema yuko tayari kutoa gari lake kwa ajili ya kubeba kifusi ili kutengeneza barabara hiyo.

Nae dereva Ali Suleiman, aliahidi kushirikiana na serikali kuwahamasisha wenzake kuchangia ili kufanikisha matengenezo ya barabara hiyo.

Barabara hiyo ambayo imechimbuka wakati wa mvua ni kero kwa madereva kwani imesababisha baadhi ya gari kuharibika.

Zanzibarleo

Share: