Habari

DC avunja ndoa ya mwanafunzi

AUGUST 11, 2018 BY ZANZIBARIYETU

KAMATI ya ulinzi na usalama ya wilaya ya Micheweni kwa kushirikiana na Wizara Kazi, Uwezeshaji, Wazee, Wanawake na Watoto, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, imeivunja ndoa ya mwanafunzi wa kidatu cha tatu, iliyotarajiwa kufanyika wiki ijayo.

Kamati hiyo iliokuwa ikiongozwa na Mkuu wa wilaya ya hiyo, Salama Mbarouk Khatib, ilifika kijiji cha Mishelishelini shehia ya Makangale na kuonana na wazazi na walezi wa binti huyo na kisha kuwaweka chini ya ulinzi kwa mahijiano.

Kamati hiyo awali ilipata taarifa ya mwanafunzi huyo kutaka kuolewa na kisha kuwaita wazazi hao ofisini kwa mkuu wa wilaya kwa mazungumzo, lakini wakipinga.

Mwanafunzi huyo anaesoma kidato cha cha tatu katika skuli ya Makangale, alikiri mbele ya viongozi hao kwamba kwa sasa hataki tena kusoma kutokana na ufahamu wake kuwa mdogo.

“Mbona wewe ulifaulu mwaka jana wakati ulipofanya mtihani wa kidato cha pili au aliekufanyia mtihani ni huyu anaetaka kukuoa,” alimuuliza Mkuu wa wilaya ya Micheweni.

Salama alisema kwa kuwa alikuwa na taarifa juu ya harusi hiyo, ndipo alipoamua kuchukua hatua hizo kabla haijafanyika.

“Mtoto huyu arudi skuli kupata haki yake ya elimu, ni kosa kisheria kumuoza mume mwanafunzi,” alisema.

Nae Mratibu wa idara ya elimu uendeshaji na utumishi, Mussa Khamis Mussa, alieleza kuwa, serikali imeondoa michango yote kwa wanafunzi, ili watoto wote waweze kupata haki yao ya elimu, hivyo watahakikisha ni kosa kisheria.

Ofisa Mdhamini Wizara ya Kazi, Uwezeshaji, Wazee, Wanawake na Watoto, Khadija Khamis Rajab, aliwaomba wazazi wa mwanafunzi huyo kufuata maagizo yaliyotolewa na wamsimamie ili kuhakikisha anamaliza masomo yake.

Nao wazazi wa binti huyo walisema wamekuwa wakimnasihi amalize masomo yake, lakini mwenyewe hataki tena kwenda skuli na chanzo cha kufanya hivyo sio kuolewa.

Mume aliyetaka kumuoa binti huyo, Othman Hassan Kulili, mkaazi wa Makangale, alisema alipanga kumuoa baada ya kumaliza masomo yake na sio sasa.

“Mimi nilipeleka posa lakini niliwambia wazazi wake kuwa nitamsubiri mpaka amalize kusoma, pia kila siku namsisitiza aende skuli kusoma hadi atakapomaliza,” alisema Bwana Harusi.

Zanzibar Yetu

Share: