Habari

Dk Bashiru Ally, anavaa viatu vya Gorbachev

Al Nofli
Jumamosi, Aprili 20, 2019

Ninamfananisha kwa mbali Katibu Mkuu wa CCM Dk Bashiru Ally na aliyekuwa Rais wa iliyokuwa Soviet Union, Mikhail Gorbachev aliyefanikiwa kuisambaratisha ‘USSR.’ Lakini, alifanya hivyo kwa nia njema, hakukurupuka.

Gorbachev baada ya kufanikiwa kuiporomosha chini USSR, nchi za Ulaya Mashariki zilizokuwa makoloni ya Urusi kuanza kutoka kwenye ulimwengu wa giza na mwisho wa vita baridi, alimaliza kazi.

Gorbachev, alikuwa Rais wa Soviet Union kuanzia March 15, 1990 mpaka Desemba 25, 1991 baada ya dunia kumuona kuwa ni mtu shujaa, mwaka 1990 alishinda tuzo ya Nobel – ‘Nobel Peace Prize.’

Sababu ya kumlinganisha Dk Bashiru na Gorbachev ni kutokana na uwazi na misimamo ya kisiasa ya Gorbachev, ambaye ndiyo chanzo kwa mataifa kandamizi ya Afrika kurudisha tena mfumo wa kisiasa wa vyama vingi.

Tanzania ni moja ya nchi za Afrika, zilizoamua kuridhia kwa shingo upande uwepo wa siasa za mfumo huo ambao inaelezwa uliridhiwa na wananchi kwa asilimia ishirini (20%) kwa mujibu wa ripoti ya ‘Tume ya Jaji Nyalali.’

Hata hivyo, Tanzania hadi leo bado, imeshindwa kuukubali mfumo huo wa siasa kwa asilimia 100 moja. Hili linathibitishwa katika kipindi cha uchaguzi ambacho kinagubikwa na vitisho, kupelekea maafa mengi na mauti ya watu.

Tume za uchaguzi ni taasisi za kubabaisha na kuibeba CCM kulinda serikali zake kuendelea kubaki kwenye madaraka kwa kutumia Jeshi la Polisi.

Dalili za wazi zipo kuwa Watanzania, Bara na Zanzibar, wameichoka CCM, na sasa wanahitaji njia ya kujing’ang’anua kutoka katika makucha ya kiharamia ya chama hicho.

Serikali za kiharamia na kidikteta zinapokaribia kuanguka hutumia Polisi na Jeshi la kulinda mipaka kupambana na upinzani ili kubaki madarakani. Hazikubali kutoka kwenye madaraka kwa sanduku la kura. Na hiyo ndiyo kauli ya baadhi ya viongozi wa CCM.

Dk Bashiru Ally, anajaribu kuifumbua macho CCM na serikali zake, kutahadhari kabla athari. Watanzania si wajinga kila siku wanajifunza kupitia matukio ya dunia ya nguvu ya umma.

Kwa sasa joto la wananchi limepanda sana kushinikiza serikali za CCM kufanya mabadiliko ya katiba ya nchi na tume huru za uchaguzi. Tanzania kwa sasa hakuna matumizi sahihi ya katiba na sheria za nchi, utawala unaendeshwa kwa matamko.

Katika Gazeti la Mwananchi la siku ya Jumatano, Aprili 17, 2019 lilikuwa na MAKALA iliyomuhusu Katibu Mkuu wa CCM, iliyokuwa na kichwa cha maneno: ‘Kauli ya Bashiru inamulika haki ya kufanya siasa.’

Please, soma makala

Kauli ya Katibu Mkuu wa CCM ya kutahadharisha kuhusu uwezekano wa kutokea machafuko ikiwa haki na usawa havitazingatiwa imekuja kwa wakati wake.

Kauli hiyo aliyoitoa hivi karibuni wakati akihutubia katika kongamano la kumbukumbu ya waziri mkuu wa zamani, hayati Edward Sokoine mjini Morogoro, inamulika uhalisia katika suala la haki na usawa wa binadamu hapa nchini.

Dk Bashiru Ally ambaye ni mwanataaluma wa sayansi ya siasa ni kama vile aliweka pembeni cheo chake cha ukatibu mkuu wa chama na kuzungumzia hali hiyo huku akieleza ugumu wa kuwaaminisha wananchi kile ambacho CCM inakihubiri.

Kwa mfano, anaeleza jinsi madereva wa bodaboda wanavyonyanyaswa na polisi, jinsi wakulima na wazalishaji wadogo wanavyokandamizwa na mamlaka za serikali, huku akirejea misimamo ya Sokoine (Edward) katika kusimamia usawa wa binadamu.

Hata hivyo, pamoja na hisia hizo, bado nachelea kusema Dk Bashiru ana kazi kubwa ya kuyasogeza mawazo hayo kwa viongozi wenzake wa CCM hadi wamwelewe.

Sina uhakika kama viongozi wa juu wa CCM wanakubaliana naye kuhusu ukandamizwaji wa haki za wanyonge.

Nasema hivyo kutokana na malalamiko ya muda mrefu kuwa upo ukandamizaji wa haki za wananchi katika kushiriki siasa wakati katiba inaitambua haki hiyo na Tanzania ni nchi inayofuata mfumo wa vyama vingi.

Katiba pia inatoa haki na uhuru wa watu kujiunga na vyama, kujumuika na kutoa maoni yao hadharani. Lakini
vyama vya upinzani na wafuasi wao wanapata taabu kufanya siasa, utafikiri ni kosa la jinai.

Siku hizi imekuwa kawaida kwa viongozi wa vyama vya upinzani kunyimwa haki ya kufanya mikutano ya hadhara kwa visingizio vya kuvunjika kwa amani wakati CCM haipati kikwazo hicho.

Tumeona watu wakiandamana kwa ajili ya kupongeza utendaji wa ngazi fulani za serikali, lakini wale wanaoandamana kuikosoa serikali hawaruhusiwi.

Siku hizi imekuwa kawaida kusikia kauli za viongozi wa Jeshi la Polisi kama vile, ‘watapata taabu sana’ watapigwa mpaka wachakae’ wakati si katiba wala sheria zinazoruhusu watu kuhukumiwa wala kuadhibiwa na vyombo vya dola badala ya mahakama.

Iko wapi haki ya kufanya siasa hapo? Uko wapi uhuru wa maoni unaotolewa na katiba? Je, huku siyo kupandikiza chuki kwa wananchi?

Kwa sababu kama ingekuwa ni tishio la amani, basi katazo hilo livihusu vyama vyote, lakini kwa nini inteljensia ya Jeshi la Polisi ikandamize upande mmoja tu wa wapinzani?

Yalianza matamko ya kukataza mikutano ya hadhara na maandamano ambayo hata hayaeleweki yalitolewa kwa misingi ya katiba na sheria zipi, lakini sasa inakwenda hadi kwenye mikutano ya ndani nako inavunjwa.

Kauli ya Dk Bashiru inapaswa kuchukuliwa kwa uzito wa kipekee na haikutakiwa ipotee hivi hivi, bali itupeleke kwenye kudai upya mabadiliko ya katiba yatakayowapa wananchi nguvu ya kurasimisha haki na usawa.

Mabadiliko ya katiba yatawaongezea nguvu wananchi kudai haki zao, tofauti na sasa tunaona viongozi wa serikali wamekuwa na nguvu kuliko hata sheria na katiba zenyewe.

Hata wale wasioutaka mfumo wa vyama vingi wajitolee kwenye mabadiliko ya katiba waseme. Sijui kwa nini mchakato wa katiba unaogopwa kiasi hiki, lakini ndiyo mwarobaini wa usawa na haki za binadamu nchini.

Katika hatua nyingine, Gazeti hilohilo la Mwnanchi la Jumamosi, Aprili 20, 2019 kupitia Mwandishi wake, Kalunde Jamal liliandika habari kumuhusu Katibu Mkuu wa CCM na Wabunge, likiwa na kichwa cha maneno: ‘Bashiru, mjadala katiba mpya ni demokarasia.’

Please, soma habari

Katibu Mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally amesema mjadala kuhusu katiba mpya ulioibuka bungeni mjini Dodoma wiki hii ni afya ya demokrasia.

Amesema mjadala huo unafungua fursa ya malumbano ya hoja kwa hoja kuhusiana na suala hilo, na ni mawanda mapana ya demokrasia.

Kauli ya Dk Bashiru imekuja baada ya baadhi ya wabunge wa upinzani Jumatano, Aprili 17, wakiwa bungeni kutumia Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015 kudai katiba mpya kwa maelezo kuwa chama hicho tawala kiliwaahidi Watanzania wakati kikiomba ridhaa ya kuwaongoza.

Madai hayo yaliibuka wakati bunge lilipokaa kama kamati kupitisha bajeti ya Wizara ya Katiba na Sheria ya 2019/2020 na aliyeanzisha hoja hiyo alikuwa mbunge wa viti maalumu (Chadema), Salome Makamba baada ya kushika shilingi ya waziri, akitaka majibu ya serikali ni lini itaendeleza mchakato wa katiba mpya.

Hoja yake iliungwa mkono na hivyo kutolewa fursa ya kuchangiwa.

Wakati ikiungwa mkono na wenzake wa upinzani, wabunge wa CCM walipinga wakikumbushia jinsi vyama vya upinzani vilivyosusia vikao vya Bunge Maalumu la Katiba pamoja na kuipinga katiba Inayopendekezwa kwa madai kuwa imechakachuliwa.

Dk Bashiru akizungumzia hilo, Jumatano (Aprili 17) mjini Dodoma alisema:

“Ninafuatilia mijadala inayoendelea bungeni na wanavyojadili kuhusu katiba mpya, hoja kwa hoja, malumbano bila kutukanana ndiyo afya ya demokrasia, nachelea kujibu kuhusu suala hilo kwa sababu nitaufunga mjadala huo.”

Alisema kinachoulizwa bungeni kinajibiwa bungeni kwenye maswali na majibu na ndiyo kazi ya bunge.

Bunge la Katiba lilikamilisha kazi yake ya kuandika katiba mpya kwa upigaji kura za kupitisha Rasimu ya Katiba ambayo ilitakiwa ipitishwe kwa kura ya maoni ya theluthi mbili ya kura kutoka kila upande wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, lakini mchakato huo ulisimama kabla ya Uchaguzi Mkuu wa 2015.

Katika hoja yake, Salome alisema kuwa licha ya Rais John Magufuli kunukuliwa akisema kuwa suala la katiba mpya siyo kipaumbele chake kwa sasa, limo katika Ilani ya CCM.

“Lakini ukurasa wa 206 na 207 wa Ilani ya CCM inasema wazi, ili kuendeleza utawala bora, demokrasia na uwajibikaji katika kipindi cha miaka mitano ijayo CCM itahakikisha inatekeleza kukamilisha mchakato wa kutunga katiba mpya na kuanza kuutekeleza kwa mujibu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba,” alisema mbunge huyo.

Mbunge huyo aliitaka serikali kuwaeleza wananchi ni lini watapata katiba mpya.

Akijibu hoja hiyo, Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Profesa Adelardus Kilangi alisema, “Katiba ni dira na ndio mwongozo ila mchakato wa katiba utaendelea kulingana na mazingira na mahitaji yatakavyoruhusu.”

Salome hakuridhika na maelezo ya Profesa Kilangi, na badala yake alishika shilingi kuruhusu wabunge kuchangia hoja hiyo.

Katika mchango wake, mbunge wa Moshi Vijijini (Chadema), Anthony Komu alisema ili kulinda utulivu na amani suala hilo limalizwe.

Naye mbunge wa Konde (CUF), Khatib Said Haji alisema anashangazwa na CCM wasivyotaka kuendeleza mchakato huo wakati walifanya sherehe na kupeana nishani wakati wakipitisha ‘Katiba Inayopendekezwa.’

Mbunge wa viti maalumu (Chadema), Susan Lyimo alichangia madai hayo kwa kusema kuwa, “Dk Bashiru (Ally, katibu mkuu wa CCM) anapita sehemu mbalimbali akisema wanatekeleza ilani ya chama hicho, ni kama mnawalaghai wananchi na mnasema tunaishi katika katiba, ni katiba ipi hiyo?”

Mbunge wa Mbeya Mjini (Chadema), Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ alisema kama suala la katiba mpya haliwezekani, serikali ifanye marekebisho ya katiba na sheria ili ipatikane tume huru ya uchaguzi.

Sugu alisema: “mtu yeyote anayekataa kufanya jambo jema ujue ni muovu. Kama hawaibi katika uchaguzi kwa nini hawataki kuondoa shari, tufanye mchakato wa kuwa na tume ambayo kila mtu akishindwa kunakuwa hakuna malalamiko.”

“Inatakiwa iwepo tume huru ambayo mfumo wa uundwaji wake tutautengeneza sisi, mfano tume inaweza kuwa na wawakilishi kutoka kila chama.”

Mbunge wa Tarime Mjini (Chadema), John Heche alisema kuwa wakurugenzi wa halmashauri walielezwa hadharani kuwa hawatarajiwi kumtangaza mpinzani kushinda, jambo linaloashiria uporaji wa kura.

“Kwa uzoefu wa chaguzi zilizofanyika huko nyuma hatukuwahi kuona hali tunayoiona sasa. Hivi sasa ni kawaida mnaweza kukusanya matokeo yenu na mkaona mmeshinda ila msimamizi wa uchaguzi anataja mshindi mwingine,” alisema Heche.

“Hivi sasa wapiga kura wanaweza kuwa wengi kuliko waliojiandikisha kupiga kura. Mawakala wanazuiwa vituoni.”

Aliongeza: “Haya mambo yanaweza kufanyika katika chaguzi ndogo ila yakifanyika uchaguzi mkuu hali itakuwa mbaya sana.

“Suluhisho ni kuleta mabadiliko ya katiba bungeni ili turekebishe kifungu kuhusu tume ya uchaguzi ili twende katika uchaguzi kwa amani,” alisema Heche.

Katika hoja ya kutaka mabadiliko ya Katiba, yameibuka mambo mawili; ama kuendeleza mchakato wa Katiba Mpya kwa kupigwa kura ya maoni ya Katiba Inayopendekezwa au kufanya marekebisho ya Katiba ya sasa ili kupata Tume huru ya uchaguzi kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa na Uchaguzi Mkuu 2020.

Katika mjadala wa bajeti hizo, kati ya wabunge watatu wa upinzani waliosimama kuzungumza, mmoja kati yao aligusia suala la Katiba Mpya na vitendo vya wakuu wa mikoa na wilaya kuwasweka watu ndani.

Katika Katiba suala linaloonekana kupata uzito ni tume huru ya uchaguzi ambapo wabunge wamebainisha kuwa haki inaonekana kutotendeka chini ya tume ya sasa.

Wametoa mifano lukuki, ikiwemo mawakala wa upinzani kuzuiwa kuingia vituoni wakati wa chaguzi ndogo, madai kuwa wasimamizi wa uchaguzi hutangaza watu ambao hawakushinda na masanduku ya kura kuporwa.

Mathalan, kiongozi wa kambi hiyo Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa Chadema, ilipendekeza kuundwa kwa tume huru itakayoondoa mamlaka ya rais ya kuteua mwenyekiti, makamu mwenyekiti na wajumbe wengine au wakurugenzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi.

Badala yake, kambi hiyo ilishauri wajumbe hao wateuliwe kwa utaratibu mwingine maalumu utakaowekwa kwa mujibu wa katiba hiyo.

Hata hivyo, uongozi wa tume ya uchaguzi umezungumzia suala hilo mara nyingi, ikisema iko huru na inafuata sheria, kanuni, taratibu na miongozo katika kusimamia uchaguzi.

Hata hivyo, mahitaji ya tume huru hayakuanza leo, hata Tume ya Jaji Francis Nyalali iliwahi kueleza kuwa “mwenyekiti na wajumbe wa tume ya uchaguzi sharti wachaguliwe na Bunge na Baraza la Wawakilishi”.

Rasimu ya Katiba ya Jaji Warioba na Katiba inayopendekezwa kwenye ibara za 190 na 211 zimetaja kuhusu kuundwa kwa Tume Huru ya Uchaguzi na jinsi tume hiyo itakavyopatikana.

Pia, Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Profesa Adelardus Kilangi alisema, “Katiba ni dira na ndio mwongozo ila mchakato wa Katiba utaendelea kulingana na mazingira na mahitaji yatakavyoruhusu.”

Salome hakuridhika na maelezo hayo lakini hata wabunge walipochangia hoja hiyo na kupigiwa kura za sauti haikupita baada ya mwenyekiti kuridhika na kura zilizosema hapana.

Tagsslider
Share: