Habari

Dk Bashiru Ally na Wallace Karia, Tundu Lissu kawakosea nini?

Picha ni Rais wa Tanzania Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi alipofika hospitali, Nairobi, Kenya kumjulia na kumfariji Tundu Lissu alikokuwa anapatiwa matibabu baada ya kushambuli kwa risasi zaidi ya 30 Septemba 7, 2017 area D nje ya makazi yake Dodoma. Picha kutoka kwenye mitandao.

Al Nofli

Jumapili, Februari 3, 2019

Tundu Lissu Mwanasheria Mkuu wa CHADEMA amebobea kwenye masuala ya siasa na amekuwa akisifika ndani na nje ya Tanzania kuwa ni mpigania haki wakati Michael Wambura amekuwa akisaka haki yake kwenye vyombo vya kisheria, lakini wanatofauti kubwa sana.

Lissu ni mtetezi wa haki na demokrasia na suala tata kuhusu Muungano wa Tanganyika na Zanzibar. Wambura anapigania haki yake tu, wala si mtetezi wa haki za Watanzania au masuala mengine yanayogusa jamii.

Naanza na Dk Bashiru Ally

Leo Jumapili, Februari 3, 2019 nilimsikiliza Katibu Mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally kupitia clip inayotambaa mitandaoni nikawa nalijiuliza mbona huyu ‘Doctor’ akili zake na za mtoto wa darasa la tano (STD V) hawana tofauti!. Nikaamini kuwa ukishakuwa CCM unanuia kuwa mjinga.

Kusema kweli kauli ya Dk Bashiru msomi wa ‘PhD’ imenishangaza sana, amejipambanua na taaluma yake na amerejea kwenye ujinga wa kupigiwa mfano.

Kwa ufupi, haiwezekani kulifananisha tukio la ajali ya Edward Sokoine na shambulizi la risasi zaidi ya 30 alizomiminiwa Tundu Lissu ni matukio mawili ambayo hayawezi kulinganishwa. Sokoine alipata ajali ya gari Lissu alishambuliwa kwa risasi na watu wasiyojuilikana.

Labda, angalau Dk Bashiru, engeweze kuchukuwa mfano wa kushambuliwa kwa risasi kwa Tundu Lissu na tukioa la kuuwawa kwa kushambuliwa kwa risasa Mzee Abeid Aman Karume, Rais wa Zanziabr wa Serikali ya Mapinduzi. Lakini, si Sokoine.

Kama alivyosema Nape Mnauye, kuwa CCM imevamiwa na wasaka tonge ndiyo watu jumla ya Dk Bashiru Ally, msomi lakini mjinga. Hata mwanafunzi wa darasa la 5 asingeweza kutoa mfano wa tukio la Lissu na ajali ya gari ya Sokoine.

Hapa nakumbusha: Edward Sokoine alifariki dunia kwa ajali ya gari Aprili 12, 1984 wakati akitokea Morogoro kuelekea Dar es Salaam.

Sokoine, alikuwa Waziri Mkuu wa Tanzania kwa vipindi viwili kuanzia Februari 13, 1977 hadi Novemba 7, 1980 na baadaye kuanzia Februari 23, 1983 hadi Aprili 12, 1984 alipofariki dunia kwa ajali ya gari. Dk Salim Ahmed Salim ambaye alikuwa Waziri Mkuu kuanzia Aprili 24, 1984 hadi Novemba 5, 1985. Dk Salim alimrithi Sokoine.

Narejea tena kidogo kwa Dk Bashiru. Viongozi wa nchi aina ya Dk Bashiru Ally ni hatari sana, viongozi wa kujikweza na kujipendekeza kwa fitina. Leo aseme fitina hii kesho aseme fitina ile ili kumfurahisha Magufuli. Ujinga mtupu.

Wakati Tundu Lissu aliposhambuliwa kwa risasi aliufyata hata ‘tweety’ yake hatukuiona, angalau mfalme wao alitumia njia hiyo kutoa salamu za pole.

Inasikitisha kuwa wakati Lissu, amepigwa risasi hakupaza sauti kulaani shambulizi lile jambo ambalo lina harufu ya tukio la kupangwa na kutengenezwa kwa maslahi maalumu.

Dk Bashiru, anapaswa kujuwa kuwa Mwenyezi Mungu pekee ndiye mwenye nguvu za uzima/uhai wa kila kiumbe. Dk Bashiru, aache kujisuka na kujipendekeza, tumeshamgunduwa kuwa kichwani ni mweupe, upepo mtupu.

Narudi kwenye habari inayo fanana na ya Dk Bashiru Ally.

Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wallace Karia amesema amemfananisha Mbunge wa Singida Mashariki (CHADEMA), Tundu Lissu na aliyekuwa Makamu wa Rais wa TFF, Michael Wambura kutokana na mambo wanayoyafanya kwenye vyombo vya habari na majukwaa mbalimbali.

Jumamosi, Februari 2, 2019 akihutubia wajumbe wa Mkutano Mkuu wa TFF uliofanyika mjini Arusha, Karia alisema watu wanaofanya U-Tundu Lissu kwenye mpira hawatapewa nafasi.

Kauli hiyo ilichukuliwa kwa hisia tofauti huku baadhi ya watu wakihoji sababu za mkuu huyo wa TFF kumtaja Lissu, kwenye masuala ya michezo, inahusu nini? Lissu yuko nje ya nchi akipatiwa matibabu.

Maoni yangu

Baadhi ya watu hususan CCM au wanaoshabikia utawala wa Magufuli, wanachanganya baina ya serikali na nchi wanashindwa kutambua kuwa ni vitu viwili tofauti. Kuhusu suala la Lissu nchi haihusiki, serikali ndiyo iliyojichafua. Serikali si nchi. Serikali ni Magufuli na gengi lake.

Narudia, serikali si nchi kwa kuwa Tundu Lissu alishambuliwa kwa risasi zaidi ya 30 watu wengi walisikitika, walihuzunika na walimuombea dua apone haraka.

Lakini, serikali ilipigamarufuku na kuzuia watu hata kuvaa fulana zilizokuwa na picha yake na maandishi ‘get better soon LISSU’. Hilo linatosha kusema serikali si nchi. Nchi na Serikali ni vitu viwili tofauti.

Kadhalika, Watanzania wengi walichangia matibabu yake kwa kutoa fedha kupitia namba za simu zilizotengwa maalumu kupitishia michango hiyo. Uongozi wa CHADEMA, hatimaye ulitangaza idadi ya fedha zilizochangwa na Watanzania. Lengo la michango hiyo ni kusaidia matibabu ya Lissu.

Serikali ya Tanzania, mbali ya kuwashangaza wananchi wake kuhusu maafa ya Lissu, lakini dunia nzima inaendelea kuaacha midomo wazi kufuatia tukio la kushambuliwa Tundu Lissu.

Hapa ndiyo tunaposema kuwa Serikali ya Tanzania ni ya mtu si ya watu. Lissu ni mbunge wa wananchi wa kuchaguliwa anashambuliwa kwa risasi, hadi sasa hakuna watu wanaotuhumiwa kuhusika na uhalifu huo.

Kiongozi wa Bunge kwa maana ya spika na naibu wake hadi leo hawakuonesha kusikitishwa na shambulizi dhidi ya Lissu. Siku chache zilizopita amenukuliwa akitoa kauli za vitisho dhidi ya ubunge wa Lissu.

Tunapouliza maswali kwa serikali ya Tanzania, spika wa bunge/naibu wake na watu aina ya Dk Bashiru Ally na Paul Makonda, kuwa hivi mtu akieleza dunia maovu yanayofanywa na viongozi wa nchi yake, ataambiwa “anachafua nchi”?.

Ifahamike kuwa watawala na madikteta watapita lakini nchi itakuwepo.

Nirudi kwa Rais wa TFF Karia, ambaye amethibitisha ni jinsi gani hajui lengo na umuhimu wa kuendeleza taasisi anayoiongoza, taasisi inayounganisha jamii wenye misimamo tofauti ya kisiasa na wasiokuwa na itikadi za vyama vya siasa.

Karia alisahau kuwa lengo la kuendeleza taasisi hiyo ni kuwaweka watu pamoja bila kujali itikadi zao, imani zao na hisia zao. Karia, anapaswa kufahamu kuwa Tundu Lissu siyo ‘size’ yake, Lissu ni namba nyingine katika dunia.

Pia Karia anapaswa kufahamu kuwa taasisi yoyote ya michezo ni starehe inayowaunganisha watu wote haipendezi kuingiza ushabiki wa kisiasa kwa kutoa mifano ya kubeza na dharau.

Lissu hakufanya kosa la kupelekea kupigwa risasi mchana kweupe. Kwa nini anapohojiwa na kujibu au kueleza maafa yaliyomfika; CCM na serikali wanalalamika kuwa anaikashifu nchi?

Lissu hatukani mtu, anachoeleza kupitia dunia ni ukweli na hali halisi ya uongozi wa sasa wa serikali ya Tanzania na bunge. Na hiyo ni moja ya kazi ya viongozi wa upinzani kote duniani, licha ya yeye kuwa anazo sababu za kueleza yaliyompata.

Nchi zinazoongozwa kwa misingi ya kidemokrasia na utawala unaoheshimu sheria ziko upande wa Lissu na wapinzani. Kwa sababu Karia ni miongoni mwa wanaCCM wenye akili finyu za samaki wanaona Lissu, anachafua nchi. Awasifu kwa lipi?

Viongozi wengi wa Tanzania, hasa wale wenye wasiwasi na nafasi zao za kazi kama Karia, Makonda na wasomi uchwara, wanasoma doti washagundua ili wasitumbuliwe na Magufuli ni kuwadhalilisha wapinzani aina ya akina Tundu Lissu.

Hoja ya Tundu Lissu kushambuliwa kwa risasa kunusurika kifo ni maajaliwa ya Mwenyezi Mungu. Mtu anaeona shambulio la risasi dhidi ya Lissu, linastahili. Huyo si mtu ni adui hata kwa mama yake mzazi.

Lissu ni mtu wa kupewa upendo na kufarijiwa kila dakika. Lissu ameonewa na bado kuna watu wanaendelea kumuonea, kumdhalilisha na kumsimanga, akina Spika Job Ndugai, Dk Bashiru Ally, Paul Makonda, Wallace Karia na wenzao wengine wote hawana tofauti na nyoka…wananiudhi sana.

Haikuwa Rais wa Tanzania wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi alifunga safari ya Nairobi kwa mintarafu ya kwenda kumliwaza na kumfariji Tundu Lissu, lakini ‘mburu matari’ washabiki wa Magufuli wanafurahiya kwa yaliyomkuta Lissu. Watanzania na Dunia wanamjuwa mchawi wa Lissu. Ipo siku atabainika hadharani.

Lakini, kwa sababu mtu anahitaji cheo kutoka kwa Magufuli, anafanya aonekane kuwa ni adui na hampendi Lissu. Na yaliyomkuta ni stahili yake, yanamfurahisha. Hivi kutetea haki ni haramu?.

Ukiona mtu anajaribu kujiweka (kujikweza) karibu sana na watawala ujue mtu huyo ni mchafu ananuka uvundo. Chunguzeni sana!. Lissu anatetea haki, kosa liko wapi?.

Rais wa TFF Karia ni vizuri akafahamu kuwa sehemu pekee ambayo inawaweka pamoja watu wa dini, itikadi za kisiasa, makabila, jinsia, umri, wenye vipato, rangi na kadhalika ni maeneo ya michezo.

Unapokuwa kiongozi ni vizuri kulifahamu hilo na siku zote kiongozi bora huhakikisha anawaweka pamoja watu anaowaongoza bila kujali tofauti zao. Karia ni vizuri sana haya mambo ya siasa akajiepusha nayo na kuhakikisha hayaingii kwenye TFF.

Kwenye viwanja vya michezo popote watu huweka kando tafauti zao na itikadi zao za kisiasa kwa sababu ni eneo la starehe tu.

Tunaona Uwanja Taifa kwenye soka, Januari Makamba na Zitto Kabwe wanaketi pamoja na kujadili mikakati ya namna Simba inavyoweza kushinda.

Mwigulu Nchemba na Freeman Mbowe wanajifaragua kivyao na kupanga mikakati ya ushindi bila kujali tofauti zao za kisiasa. Hivyo ndiyo inavyotakiwa.

Kila nikifanya utafiti nimegundua wapinzani wa Lissu kisiasa wameshindwa kwa hoja ndiyo maana wanawatumia wajinga wasiyojitambua kumchafua, pasipo kuelewa.

Nadhani ni makosa ya utaalamu katika ‘Public Speaking’ kwa mtu kama Wallace Karia hana ujuzi wa kuzungumza kwenye hadhira. Anadhani kukonga nyoyo za watu ni kuwadhalilisha wengine.

Inawezekana kalitumia neno la ‘Ma-Tundu Lissu wa kwenye Soka’ akidhani ni kauli rahisi na nyepesi. Hili ni doa kwa taasisi na mashirikisho mengine ya michezo duniani.

Viongozi wa Mashirika ya Michezo ya Dunia, hawakuwa wajinga kukataza alama, ishara, nembo na kauli za kisiasa kuingizwa katika michezo, wanajua hisia ya siasa inavyoweza kuwasambaratisha watu hata waliyotimu moja.

Kwa nchi zenye kuheshimu ‘title’ za watu Karia muda huu hana tena kazi, iwe kwa hiari kwa kujiuzulu au kwa lazima tena kupitia vyombo vya habari tu. Nafasi ya Tundu Lissu kisiasa, kibunge na kitaaluma ni mtu mkubwa sana. Tundu Lissu anaheshimika kwa uwezo wake.

Linapofananishwa jina la Lissu katika hotuba ya kumsema au kumkemea Wambura, ni kuonyesha kuwa Lissu ni kama Wambura. Kitu ambacho si sahihi au niseme ni kosa.

Kuna msemo: ‘bora kujikwaa kidole kuliko kujikwaa ulimi’:

Karia alieleza kuwa, alimfananisha Lissu na Wambura kutokana na yanayoendelea kwa sasa, ambapo wamekuwa wakitumia vyombo vya habari kufanya upotoshaji.

“Nilisema kuwa hatutaki mambo ya kina Tundu Lissu kwenye mpira, nadhani mnajua kwa sasa Lissu anahaingaika kwenye vyombo vya habari kuikashifu serikali yetu na Wambura naye anazunguka kwenye vyombo vya habari kuikashifu TFF na viongozi wake.”

“Kwa hiyo nikamlinganisha Wambura na Lissu, lakini kama hii kauli imewakera wengine naomba samahani ila nimewalinganisha kutokana na kuhama hama kwenye vyombo vya habari kutoa kauli za kuwadhalilisha viongozi waliochaguliwa kihalali,” alisema Karia.

Hata hivyo, licha ya Karia kuomba radhi kwa kauli yake hiyo, CHADEMA kupitia Idara yake ya Uenezi imemtaka kiongozi huyo wa TFF kuomba radhi kwa kuwa, alitumia jina la Lissu kwa lengo la kumchafua.

Taarifa hiyo imesema kuwa CHADEMA haina mpango wa kuingia kwenye ugomvi na TFF wala wadau wa michezo hivyo, ni vyema akatekeleza agizo hilo la kumuomba radhi Lissu kabla ya hawajachukua hatua za kisheria.

Binafsi naamini Karia, hakukosea ni dhamira yake ndiyo maana kwenye kauli yake ya kuomba msamaha kasema alichomaanisha kuwa; “Lisu anahangaika na kuikashifu serikali na Wambura anafanya hivyo hivyo kwa serikali.”

Kwa maana hiyo alitamka kauli hiyo akiwa amelenga shebaha na madhumuni maalumu hasa katika nafasi yake ya kazi yake u-Rais wa TFF, ili kumfurahisha Magufuli..

Share: