Habari

Dk. Mabodi: Tushindae kwa sera sio vituko

February 11, 2018

NA ABDI SULEIMAN, PEMBA

WANANCHI wa kisiwani Pemba, wametakiwa kufahamu kuwa serikali iliyopo madarakani inayoongozwa na Dk. Ali Mohamed Shein ni halali kwani imechaguliwa na kupata baraka kamili za wananchi na hakuna uchaguzi mwengine hadi 2020.

Uchaguzi wa marudio ulivishirikisha vyama mbalimbali vya siasa, hivyo haiwezekani mtu mmoja kususia kwake kubadilishe mchakato na matokeo ya uchaguzi.

Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Dk. Abdulla Juma Saadalla, aliyaeleza hayo wakati alipokuwa akizungumza na wanachama wa CCM wa Tawi la Mwambe na Kendwa jimbo la Kiwani, ikiwa ni ziara yake ya kuangalia utekelezaji wa ilani ya CCM ya 2015/2020.

“Kwa miaka hii sahauni kuhusu uchaguzi hapa mpaka 2020, CCM mbele kwa mbele na sio mguu mbele mguu nyuma kama wanavyosema wao. Uchaguzi mkuu kwa Zanzibar ni 2020 panapo majaaliwa” alisema.

Aliwataka viongozi wa matawi kushuka chini kwa wananchama na wananchi, kuwaelezea maendeleo mbalimbali yaliyofanywa na serikali iliyopo madarakani.

Mabodi alifahamisha umuhimu wa vyama vya siasa ni kushindana kwa sera na sio kushindana kwa vituko, kwani bado wazanzibari wanahitaji kuishi kwa amani na utulivu.

Hata hivyo aliwataka makatibu na wenyekiti wa matawi, kuwapokea wanachama wapya watakaojiunga na CCM, kutoka vyama vya upinzani kwani tayari kuna idadi kubwa ya wapinzani wanatarajiwa kujiunga na CCM kwa upande wa Zanzibar.

Hata hivyo alisema wakati umefika wa kurudisha madarasa ya itakadi ya CCM, kama ilivyokuwa miaka ya nyuma ambayo ni muhimu kwa CCM.

“Wajumbe wa NEC wajibu wenu kupita kwa wananchi na sio kukaa ofisi, sasa kazi ya kwenda vijijini imewadia kuhakikisha wanachama wapya wanapatikana”, alisema.

Hata hivyo aliwataka wanaCCM kujitokeza kwa wingi kujiandikisha katika daftari la wapiga kura wakati utakapofika, ili CCM iweze kurudi tena madarakani.

Zanzibarleo

Share: