Habari

Dk Shein aagana na gavana wa BOT

January 8, 2018

STATE HOUSE ZANZIBAR

OFFICE OF THE PRESS SECRETARY

PRESS RELEASE

Zanzibar 08.01.2018

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein ameagana na Gavana wa Benki ya Tanzania (BOT) anayemaliza muda wake Profesa Benno Ndulu ambaye ameeleza furaha yake ya kuuona uchumi wa Zanzibar ukiwa umeimarika kwa kiasi kikubwa chini ya uongozi wa Dk. Shein.

Katika mazungumzo hayo ya kuagana yaliyofanyika Ikulu mjini Zanzibar, Profesa Ndulu alimueleza Dk. Shein kuwa kazi ya kuimarisha uchumi iliyofanywa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar chini ya uongozi wa Dk. Shein ni kubwa sana na kuna haja ya kupongezwa.

Profesa Ndulu alieleza kuwa uchumi wa Zanzibar ni mkubwa sana hatua ambayo inatokana na kasi kubwa ya kuimarisha uchumi huo ilivyofanywa huku akisisitiza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iko vizuri kifedha.

Alieleza kuwa sekta ya utalii nayo kwa upande wake imeweza kuchangia kwa kiasi kikubwa kuimarisha uchumi wa Zanzibar sekta ambayo imeweza kusaidia kukuza uchumi huo badala ya kutegemea zao moja la karafuu peke yake.

Aliongeza kuwa uchumi wa Zanzibar umeweza kuimarika kwa kiasi kikubwa kutokana na kukua kwa sekta hiyo ya utalii hapa nchini hatua ambayo imepelekea kuimarika kwa huduma mbali mbali za kimaendeleo na kijamii huku ikiendelea kuwa kivutio duniani.

“Nuru ya Zanzibar inaendelea kungara na maendeleo yanazidi kuimarika siku hadi siku…hongera sana kwa hatua ya kiuchumi iliyofikiwa hapa Zanzibar, pongezi hizi nazitoa kwa dhati ya moyo wangu kabisa”, alisisitiza Profesa Ndulu.

Aidha, Profesa Ndulu alimueleza Dk. Shein kuwa kuimarika kwa uchumi wa Zanzibar hivi sasa kunatokana na uongozi imara wa Rais Dk. Shein pamoja na utaalamu na uzoefu wake mkubwa wa uongozi alionao kwa muda mrefu.

Pamoja na hayo, Profesa Ndulu alitumia fursa hiyo kumueleza Dk. Shein mashirikiano mazuri yaliopo kati ya uongozi wa Wizara ya Fedha Zanzibar na Benki hiyo hatua ambayo imeweza kuleta mafanikio makubwa ndani ya uongozi wa miaka kumi akiwa Gavana wa BOT na matarajio aliyonayo ya kuendeleza zaidi mafanikio hayo miaka kwa ijayo.

Sambamba na hayo, Profesa Ndulu alimueleza Dk. Shein majukumu yake mengine atakayoyafanya katika masuala mazima ya kiuchumi na kifedha kitaifa na kimataifa mara baada ya kumaliza muda wake wa kazi ya Gavana wa (BOT).

Nae Rais Dk. Shein kwa upande wake alimpongeza Gavana wa Benki ya Tanzania (BOT) anaemaliza muda wake Profesa Benno Ndulu kutokana na mchango wake mkubwa alioutoa katika kuiimarisha na kuiendeleza sambamba na kusimamia fedha za Tanzania katika Benki hiyo.

Dk. Shein alitumia fursa hiyo kumpongeza Profesa Ndulu kwa kufanya kazi kwa mashirikiano makubwa kati yake na uongozi wa Wizara ya Fedha wa Zanzibar sambamba na michango yake katika kuimarisha kada ya fedha hapa nchini.

Katika mazungumzo hayo, Dk. Shein alieleza kufurahishwa na maelezo ya Profesa Ndulu kuhusiana na kuimarika kwa uchumi wa Zanzibar ambapo alisisitiza kuwa juhudi zake zimeweza kuendeleza juhudi za kuimarisha uchumi kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Pamoja na hayo, Dk. Shein alieleza kuwa (BOT), ni Benki ya Muungano ambayo imekuwa ikifanya vyema shughuli zake kwa pande zote mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzani.

Aidha, Dk. Shein Shein alieleza kuwa ipo haja ya kujivunia mafanikio hayo makubwa ya kiuchumi yaliofikiwa hapa Zanzibar huku akieleza matumaini yake ya kuendelea Benki hiyo kufanya vizuri chini ya uongozi mpya wa Profesa Florens Luoga.

Rais Dk. Shein alimueleza Gavana huyo anaemaliza muda wake kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar chini ya uongozi wake itaendelea kutoa ushirikiano mkubwa na Benki hiyo kupitia Tawi lake lililopo Zanzibar.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

Pemba Today

Share: