Habari

Dk. Shein afanya uteuzi

May 17, 2018

Kumbi mashuri zapewa majina mapya

NA MWANDISHI WETU

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, amemteua Balozi Mohamed Ramia Abdiwawa kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Utumishi ya Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali.

Kwa mujibu wa taarifa iliyosambazwa kwa vyombo vya habari iliyosainiwa na Kaimu Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi, Salum M. Salum imeeleza kuwa uteuzi huo umeanza Mei 15 mwaka huu.

Taarifa hiyo ilieleza kuwa Dk. Shein amefanya uteuzi huo kwa mujibu wa uwezo aliopewa chini ya kifungu nambari 8(1), cha sheria ya uanzishwaji wa Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali yam waka 2003.

Aidha taarifa hiyo pia ilieleza kuwa Dk. Ali Mohamed Shein amemteua Dk. Mwinyi Talib Haji kuwa Mkurugenzi wa Chuo cha Utawala wa Umma (IPA), ambao ameufanya chini ya kifungo cha 9(1) cha sheria ya Chuo cha Utawala wa Umma ya mwaka 2007.

Katika taarifa nyengine iliyotolewa na Kaimu Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi, imeeleza kuwa katika kuwaenzi viongozi wa kitaifa, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein ameupatia jina jipya ukumbi wa zamani wa baraza la Wawakilishi.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo ukumbi huo hivi sasa rasmi utaitwa Ukumbi wa Sheikh Idrissa Abdul Wakil, ikiwa ni hatua ya kumuenzi aliyekuwa Rais wa awamu ya Nne wa Zanzibar na Spika wa Mwanzo wa Baraza la Wawakilishi.

Kadhalika kwa mujibu wa kifungu nambari 4(2), cha sheria ya kuwaenzi viongozi wa kitaifa nambari 10 ya mwaka 2002, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, ameruhusu ukumbi wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA), kuitwa ukumbi wa Dk. Ali Mohamed Shein.

Taarifa hiyo ilifahamisha kuwa lengo la kuupa jina hilo ukumbi huo ni kumuenzi na kutambua mchango wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi katika kukuza elimu.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo majina ya kumbi hizo yameanza kutumika rasmi Mei 11 mwaka huu.

Zanzibarleo

Share: