Habari

Dk Shein Ahutubia Baraza la Eid el Fitr Zanzibar

Zanzibar 26.06.2017

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk.Ali Mohamed Shein ametanabaisha na kusisitiza juu ya umakini mkubwa unaohitajika katika kuandaa, kusimamia na kufuatilia Mikataba ya Mafuta na Gesi ili kuepuka ubabaishaji kwani rasilimali hizo ni za Wazanzibari wote.

Alhaj Dk. Shein aliyasema hayo leo katika hotuba yake aliyoitoa katika Baraza la Idd El Fitri lililofanyika huko katika ukumbi wa zamani wa Baraza la Wawakilishi, Kikwajuni Mjini Zanzibar.

Alisisitiza kuwa mikataba ya Mafuta na Gesi Asilia isitoe mwanya wa kuwanufaisha watu wachache na makampuni yao kwa njia za kijanja, dhulma na mambo ya ubabaishaji na kutaka kujifunza kwa waliotangulia katika biashara ya aina hiyo.

Katika hotuba yake, Dk. Shein alisema kuwa baada ya kukamilika kwa kazi ya kutunga Sheria ya Mafuta na Gesi Asilia, kuanzisha Mamlaka ya Kusimamia na kuratibu shughuli za Mafuta na Gesi na kuanzisha Kampuni ya Mafuta, hatua muhimu inayofuatana ni kuandaa Mikataba ya Mafuta na Gesi Asilia.

Alisema kuwa uongozi wa Wizara ya Ardhi, Maji, Nishati na Mazingira, wataalamu na Taasisi zote zinazohusika katika kuandaa Mikataba hiyo, wafahamu kuwa rasiliamali ya Mafuta na Gesi Asilia ni ya Wazanzibari wote.

Hivyo, alisisitiza kuwa wote hao wana dhamana na jukumu kubwa la kuhakikisha kuwa maslahi ya Zanzibar na wananchi wake yanalindwa na vigezo vyote muhimu vinazingatiwa.

Alhaj Dk. Shein alitumia fursa hiyo kutoa pongezi kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Pombe Magufuli kwa juhudi anazoendelea kuzichukua katika kukuza uchumi, ikiwemo ufufuaji na uendelezaji wa sekta ya viwanda na uzuiaji wa usafirishaji wa mchanga wenye dhahabu nje ya nchi pamoja na kuzilinda rasilimali za Taifa.

Aidha, alisema kuwa Watanzania wote, bila ya kujali itikadi zao za kisiasa, hawana budi wamuunge mkono na kumpa moyo kwa kazi nzuri anayoifanya.

Alisema kuwa juhudi anazozichukua za kupambana na rushwa na uhujumu wa uchumi, ni katika kulitekeleza jukumu la Serikali la kuwatumikia wananchi kama ilivyoelekeza Ilani ya Uchaguzi Mkuu ya CCM ya mwaka 2015-2020.

Alhaj Dk. Shein pia, alieleza kuwa Serikali anayoiongoza itaendelea kuweka usimamizi madhubuti wa matumizi ya fedha zake kwa kuweka vipaumbele katika mambo muhimu yenye kuleta tija kwa maendeleo ya nchi.

Aliongeza kuwa Serikali itaongeza kasi kwenye vita vya kupambana na rushwa na uhujumu wa uchumi na kusimamia utekeleza wa misingi yote ya utawala bora huku akizipongeza TRA na ZRB kwa juhudi zao zilizopelekea kuvuka malengo ya ukusanyaji wa Mapato pamoja na kuupongeza uongozi wa Wizara ya Fedha na Mipango kwa usimamizi mzuri wa ukusanyaji wa mapato na udhibiti wa matumizi.

Pamoja na hayo, Alhaj Dk. Shein aliwata viongozi kushirikiana na wananchi kwani wanamategemeo makubwa kwa Serikali yao katika kuwatumikia kama walivyoahidi na kuwataka kila mmoja kutekeleza wajibu wake kwani viongozi wa dini, siasa na wa kijamii wana wajibu wa kuzitekeleza dhamana zao. Kadhalika watumishi wa umma nao wanapaswa kuwatumikia wananchi kwa uadilifu na kwa misingi ya usawa.

Alhaj Dk. Shein alitumia fursa hiyo kwa kutoa shukurani zake za dhati kwa Mashekh na Waalimu wote waliofanya kazi kubwa ya kutoa darsa mbali mbali, katika Mwezi Mtukufu wa Ramadhan kwa lengo la kukumbusha juu ya maamrisho ya Mola wa viumbe wote.

Alitoa pongezi maalum kwa wananchi na wageni ambao hawakuwa katika funga kwa ushirikiano waliouonesha kwa ndugu zao Waislamu jambo ambalo limeonesha kielelezo cha uhusiano mwema na kupevuka kwa utamaduni wa kuishi kwa kustahamiliana huku akiwatakia safari njema Waislamu watakaokwenda kutekeleza ibada ya Hijja mwaka huu.

Pia, aliwapongeza wananchi wote kwa kudumisha hali ya amani na utulivu nchini wakati wote khususan katika kipindi chote cha Mwezi Mtukufu wa Ramadhan na kuvipongeza vikosi vya ulinzi na usalama kwa kusimamia hali hiyo.

Aliwapongeza kwa dhati wafanyabiashara wote waliolizingatia ombi lake alilolitoa kwao kwa lengo la kuwahurumia ndugu zao na kutafuta radhi za Mola wao, pale walipoitikia wito wa Serikali wa kuwataka kutopandisha bei ya bidhaa zao katika Mwezi wa Ramadhan ili kuwapa unafuu wananchi.

Alhaj Dk. Shein aliwataka wananchi kuendelea kuchukua tahadhari katika kukabiliana na maradhi ya kipindupindu kwa kutekeleza maelekezo yote yanayotolewa na Serikali, ili ile hali iliyotokea mwaka 1978 na mwaka 1998 isitokee tena na kueleza kuwa iwapo kanuni za afya bora, usafi wa mazingira na vile vile ujenzi unaozingatia sheria za mipango miji na vijiji zitazingatiwa ugonjwa huo utatokomezwa.

Alieleza kuwa Serikali inachukua hatua ya kuandaa Mpango wa kinga dhidi ya maradhi ya kipindupindu kwa kushirikiana na Shirika la Afya Duniani (WHO) ambapo wataalamu wa Shirika hilo wanatarajia kufika hapa nchi ni hivi karibuni.

Katika Baraza hilo la Idd El-Fitri viongozi mbali mbali walihudhuria akiwemo Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama Samia Suluhu Hassan, Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idd, Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh Saleh Omar Kabi, Spika wa Baraza la Wawakilishi Zubeir Ali Maulid na wengineo.

Mapema asubuhi, Dk. Shein aliungana na waumini wa dini ya Kiislamu katika sala ya Idd el Fitri iliyofanyika katika viwanja vya Maisara mjini Unguja.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

Zanzinews

Share: