Habari

Dk. Shein apata mapokezi makubwa

NA RAHMA SULEIMAN
14th July 2015

Mgombea urais wa Zanzibar kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Ali Mohamed Shein.
Mgombea urais wa Zanzibar kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Ali Mohamed Shein, jana alipata mapokezi makubwa Zanzibar akitokea Dodoma, baada ya kuteuliwa kuwa mgombea.

Pia, alimpongeza mgombea wa urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Magufuli, akisema kiongozi huyo ni mwadilifu na hana kashfa zozote zinazohusiana na ufisadi.

Dk. Shein aliyasema hayo wakati akizungumza na wanachama wa CCM katika Ofisi Kuu ya CCM Kisiwandui, baada ya kupokelewa.

Alisema anamfahamu Magufuli na kuwa ni mchapaka kazi na mwadilifu hivyo hana shaka yoyote na uongozi wake.

“Magufuli hana doa wala hana skendo za kashfa, mimi namfahamu sana, ni kiongozi mzuri na hodari nimefanya kazi naye miaka tisa na nusu, namjua uwezo wake, ufanyaji kazi zake, heshima yake na ana sifa kubwa sana ya kuingoza nchi hii, ”alisema Dk. Shein.

Aidha, alimpongeza kwa kumteua mgombea wake mwenza mwanamke, Samia Suluhu, na kusema kuwa ndani na nje ya chama hicho itakuwa historia kubwa ya wanawake kupewa nafasi za juu za ungozi.

Alisema katika uongozi wake endapo atapata ridhaa ya wananchi ataendelea kuwapa kipaumbele wanawake katika kuwapa nafasi mbalimbali za uongozi ili asilimia50 kwa 50 ipatikane.

Alitumia nafasi hiyo kuwataka waangalizi wa uchaguzi kutoka ndani na nje ya nchi wafuate sheria za nchi na sheria za uchaguzi badala ya kuchokonoa mambo ambayo hayawahusu.

Dk. Shein aliwasili jana na kupokelewa na wananchi na wafuasi wa CCM katika uwanja wa ndege wa Abeid Amani Karume akitokea Dodoma na kusindikizwa na magari na mapikipiki hadi makao makuu ya CCM Kisiwanduwai na kuzungumza na wanachama hao.

CHANZO: NIPASHE

Share: