Habari

Dk Shein atembelea kisiwa cha Bali nchini Indonesia

Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein akisalimiana na Gavana wa mji wa Bali, Indonesia, IMade Mangku Pastka walipokutana kwa  mazungumzo katika Hoteli ya Discovery Kartika Plaza siku ya Ijumaa, Agosti 3, 2018.

Bali, Indonesia
Agosti 4, 2018

RAIS wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein amefurahishwa na fursa iliyotolewa na Gavana wa kisiwa cha Bali nchini Indonesia, itakayowezesha vijana wa Zanzibar kwenda kujifunza uendeshaji wa shughuli za utalii kwenye kisiwa hicho.

Dk Shein alionyesha furaha yake hiyo wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Gavana wa Jimbo la kisiwa cha Bali, IMade Mangku Pastka mazungumzo yaliyofanyika Ijumaa, Agosti 3, 2018 katika Hoteli ya Kartika Plaza iliyopo mjini Bali.

Rais wa Zanzibar alimueleza kiongozi huyo kuwa fursa hiyo ni ya pekee na inajenga imani kubwa kutokana na uhusiano wa kihistoria uliopo kati ya Zanzibar na Indonesia.

Alisema kuwa fursa hiyo itasaidia kwa wanafunzi wa fani ya utalii katika Chuo Kikuu cha Zanzibar (SUZA) kupata taaluma zaidi ya kujifunza namna ya uendeshaji shughuli za hoteli na utalii katika kisiwa hicho ambacho kimepata mafanikio makubwa kutokana na sekta hiyo kuimarika.

Pia, Dk Shein alitumia fursa hiyo kutoa shukurani kwa Gavana huyo kwa mapokezi makubwa aliyopata katika ziara ya kisiwa hicho kidogo cha Bali, kilichopo Kusini Mashariki mwa Jakarta.

Dk Shein alisema kwa muda mrefu Zanzibar imeanza biashara ya utalii kwa lengo la kukuza uchumi na kwa sasa sekta hiyo imekuwa ikichangia fedha za kigeni kwa asilimia 80 ya pato lake.

Alisema lengo kubwa katika kukuza sekta hiyo ni kuhakikisha kwamba ifikapo mwaka 2020 idadi ya watalii wanaotembelea Zanzibar iweze kuvuuka lengo lililokusudiwa hadi watalii laki tano kwa mwaka.

Alisema sababu nyingi kwa Zanzibar kutaka kushirikiana na Kisiwa cha Bali ni katika kuendeleza sekta ya uvuvi ambayo nayo imeweza kupata mafanikio makubwa katika kisiwa hicho.

Awali, Gavana wa Kisiwa cha Bali, IMade Mangku Pastka akimkaribisha Rais wa Zanzibar, alieleza ni kwa kiasi gani alivyofarajika pamoja na wakazi wa kisiwa hicho kutokana na ziara wa Rais wa Zanzibar na ujumbe wake ambayo imeimarisha uhusiano kati ya Indonesia na Zanzibar.

Alisema kutokana na kisiwa hicho kubeba shughuli za kitalii na kupelekea kuwa na hoteli nyingi za kitalii, vyuo vya kitalii pamoja na huduma za kiwango cha juu kwa watalii, hivyo wako tayari kuwapokea wanafuzi wa Zanzibar kujifunza ili kupata utaalamu wa kuimarika sekta hiyo.

Alisema Bali, iko tayari kutoa nafasi za masomo kwa vijana wa Zanzibar wa fani ya utalii kwenda kujifunza zaidi kisiwani Bali, hata kuwapo kwa ziara fupifupi za kubadilishana uzoefu na utaalamu.

Pia, Gavana huyo alimueleza Dk Shein mafanikio waliyoyapata wakazi wa Bali katika kuimarisha sekta ya uvuvi na kuunga mkono kuwepo kwa mashirikiano baina ya Indonesia na Zanzibar kwa muda mfupi ujao.

Akiwa katika Hoteli ya Kartika Plaza iliyopo mjini Bali, Dk Shein alikutana na Uongozi wa Kampuni ya Utalii ya Bali, ukiongozwa na Mkurugenzi Mkuu wake Abdulbakar Mansoer ambaye alieleza mafanikio yaliopatikana katika sekta ya utalii kisiwani humo huku akiahidi mashirikiano kati ya Bali na Zanzibar.

Wakati huo huo, Dk Shein alitembelea Chuo Kikuu cha Udayana kiliopo Jambaran Kisiwani Bali na aliweza kuzungumza na walimu pamoja na wananfunzi wa chuo hicho katika jengo la Ruang Bangsa.

Dk Shein alitoa pongezi na shukurani kwa uongozi wa Chuo Kikuu cha Udayana kwa mapokezi mazuri waliyopata pamoja na kusisitiza haja ya kuwepo kwa mashirikiano kati ya Chuo Kikuu cha cha Zanzibar (SUZA) na chuo hicho.

Akizungumza na wananfunzi wa chou hicho, Dk Shein alisisitiza kusoma kwa bidii na hasa ikizingatiwa kuwa nchi yao ya Indonesia inawategemea kuwa viongozi na watendaji wazuri kwa siku zijazo.

Dk Shein ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa Chuo Kikuu cha Zanzibar (SUZA), alitoa mwaliko kwa wanafunzi wa Udayana, kutembelea Zanzibar kujifunza pamoja na kubadilishana uzoefu na taaluma na wenzao wa Chuo Kikuu cha SUZA.

Aidha, Dk Shein alitembelea ofisi za kampuni ya mafuta ya nazi ya ‘Samani Island Virgin Coconut Oil’. Uongozi wa kampuni hiyo ulimueleza Dk Shein, pamoja na mafanikio ulioyapata kutokana na kuwa na soko la uhakika la kuuza mafuta ya nazi la ndani na nje ya nchi zikiwemo nchi za Ujerumani, Australia, Bulgaria na Japan.

Akizungumza na Uongozi wa Kampuni hiyo, Dk Shein alisema lengo la ziara yake katika ofisi hizo ni kuangalia uwezekano wa kushirikiana pamoja katika kufufua biashara ya mafuta ya nazi pamoja na kilimo cha minazi, zao lililoipatia sifa kubwa Zanzibar, hapo miaka ya nyuma.

Dk Shein alihitimisha ziara yake katika kisiwa hicho cha Bali kwa kuungana na Waislamu katika ibada ya sala ya Ijumaa, iliyosaliwa katika Masjid Huda Islamiya Mjini Bali.

Share: