Habari

Dk. Shein atoa sadaka ya chakula

May 27, 2018

NA MWINYIMVUA NZUKWI

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj, Dk. Ali Mohamed Shein amekabidhi sadaka ya vyakula kwa wananchi wa mikoa mitano ya Zanzibar ikiwa ni miongoni mwa utaratibu aliojiwekea unaolenga kupunguza ukali wa maisha kwa wananchi katika kipindi hiki cha mwezi mtukufu wa Ramadhani.

Akikabidhi sadaka hiyo kwa niaba ya Rais, Mwenyekiti wa Kamati ya zaka na sadaka ya Rais wa Zanzibar, Haji Nassib Nyanya sadaka hiyo pia imekusudiwa na kukuza moyo wa kusaidiana miongoni mwa jamii ambapo jumla ya pakti 2,500 za mchele, unga wa ngano na sukari zitakabidhiwa kwa wakuu wa Mikoa na wakuu wa wilaya ili kugaiwa kwa wananchi.

Alifafanua kuwa jumla ya shilingi milioni 105 zimetumika kununulia vyakula hivyo ambapo ambavyo ni mchele pakti 1,000, unga wa ngano pakti 1,000 na sukari pacti 500 za kilo 50 kila moja na kueleza kuwa kila wilaya itakabidhiwa pakti 60 za unga, pakti 60 za mchele na pakti 30 za sukari.

“Kila mwaka Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein amekuwa akitoa sadaka hii kupitia kamati katika mwezi wa Ramadhani au karibu na sikukuu hivyo ipo haja na kila mwenye uwezo kufuata nyayo za Rais kwa kuwajali watu wenye mahitaji”, alisema Nyanya.

Akipokea sadaka hiyo kwa niaba ya wakuu mikoa mingine na wananchi wa Zanzibar kwa ujumla, Mkuu wa mkoa wa Mjini Magharibi Ayoub Mohammed Mahmoud amemshukuru Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein kwa kuendeleza jambo hilo jema analolifanya kila mwaka ambalo linatoa mfano mzuri wa viongozi wanaowajali wananchi wao.

Zanzibarleo

Share: