Habari

DK Shein awaalika wafanyabiasha na wawekezaji wa Indonesia

Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein akisalimiana na Meya wa Jimbo la Gorontalo, Indonesia Profesa Nelson Pamalingo. Mazungumzo yao yalihusu ushirikiano wa kilimo cha minazi walipokutana katika Hoteli ya Borobudur, mjini Jakarta.

Jakarta, Indonesia
Jumatano,Agosti 1, 2018

RAIS wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein amewaalika wafanyabiashara na wawekezaji kutoka nchini Indonesia, kwend Zanzibar, ili kufungua makampuni ya biashara na kuwekeza kwa kuangalia fursa zilizopo.

Dk Shein alitoa mwaliko huo leo Jumatano, Agosti 1, 2018 wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na jumuiya ya wafanyabiashara na wenyeviwanda wa nchini Indonesia (KADIN), katika ukumbi wa Ofisi ya Jumuiya hiyo iliyopo mjini Jakarta.

Dk Shein akizungumza katika mkutano huo na wafanyabiashara wa nchi hiyo, aliwaeleza kuwa kuna sababu mbali mbali ambazo wawekezaji wanaweza kuichagua Zanzibar kama ni sehemu pekee ya kuekeza ikiwa ni pamoja na kuwepo mazingira mazuri ya uwekezaji.

Alisema Zanzibar, ina soko kubwa la biashara linalojumuisha nchi za Afrika Mashariki na Jumuiya ya nchi za kusini mwa Afrika (SADC).

Rais wa Zanzibar, aliwaeleza wafanyabiashara hao kuwa miongoni mwa sababu kubwa ambayo Zanzibar pamoja Tanzania Bara, zinajivunia kuwepo kwa amani, usalama na utulivu.

Dk Shein alisema kuwa kunaweza kuimarishwa uhusiano imara kati ya nchi hizo mbili katika maeneo ya biashara na uwekezaji.

Aidha alisema uendelezaji wa miundombinu ambapo uhusiano kama huo pia, unaweza kuanzishwa kati ya Zanzibar na kampuni binafsi za Indonesia.

Akitangaza fursa za uwekezaji zilizopo Zanzibar katika sekta mbali mbali za uchumi, katika mkutano huo Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Uwekezaji Vitega Uchumi Zanzibar (ZIPA) Salum Khamis Nassor alisema kuwa Zanzibar ni eneo la pekee lenye matumaini katika kuekeza katika sekta kadhaa za uchumi.

Nao viongozi na Wanajumuiya ya Wafanyabiashara na Wenyeviwanda ya Indonesia (KADIN), walisema mafanikio waliyoyapata katika Jumuiya yao hiyo na kuahidi kuitumia fursa ya kwenda kuekeza na kufanya biashara Zanzibar, kamahatua ya kukubali mwaliko wa Rais wa Zanzibar.

Pia, Dk Shein alikutana na uongozi wa Kampuni ya mafuta na gesi ya Pertamina ya nchini humo ambao ulimueleza mafanikio iliyoyapata katika shughuli zake za sekta hiyo na kueleza kuwa tayari imeshaanza kufanya shughuli zake Tanzania Bara katika mikoa ya Lindi na Mafia.

Hivyo, kutokana na mazungumzo hayo kampuni hiyo ilivutika na kuahidi kuitumia fursa hiyo ili kuangalia uwezekano wa kuanzisha mashirikiano na Zanzibar, hasa wakizingatia uzoefu na mafanikio waliyoyapata katika sekta hiyo.

Mapema Dk Shein alikutana na kufanya mazungumzo na Meya wa Jimbo la Gorontalo, Profesa Nelson Pomalingo na kukubaliana haja ya kuimarisha ushirikiano kati ya Zanzibar na Indonesia katika sekta ya kilimo hasa kilimo cha minazi.

Naye, Meya wa Jimbo la Gorontala alimueleza Dk Shein kuwa Indonesia na Zanzibar ni maeneo yanayofanana kijiografia hivyo kushirikiana katika sekta ya kilimo kuna weza kukapelekea mafanikio kwa nchi zote mbili.

Hata hivyo, Meya huyo alisema katika kilimo cha minazi licha ya kuwa changamoto zilizopo katika kilimo hicho kwa upande wa Indonesia zinafanana na zile za Zanzibar, lakini nchi hiyo imeweza kupata mafanikio makubwa kutokana na zao hilo.

Katika mazunguzo hayo, kiongozi huyo Profesa Nelson aliahidi kuanzisha na kuendeleza uhusiano na ushirikiano na kusisitiza kuwa atahakikisha mashirikiano yanaanzishwa na kusimamiwa katika kuhakikisha kilimo hicho kinaimarishwa katika Zanzibar.

Mazungumzo kama ya Rais wa Zanzibar, pia yalifanywa viongozi wanaoungana na Dk Shein katika ziara hiyo amabo walipata fursa ya kukutana na kufanya mazungumzo na wenzao wa Indonesia katika ukumbi wa Hoteli ya Borobudur, mjini Jakarta.

Katika mikutano hiyo iliyofanyika kwa nyakati tofauti, viongozi hao wa pande zote mbili walieleza haja ya kuwepo kwa mashirikiano ya pamoja sambamba na kubadilishana uzoefu na utaalamu katika kuimarisha sekta za maendeleo hususan sekta ya utalii, uvuvi na kilimo.

Kadhalika, Dk Shein leo Jumatano, Agosti 1, 2018 amefanya mazungumzo na mwenyeji wake, Makamu wa Rais wa Indonesia, Muhammad Jusuf Kalla ambapo katika mazungumzo hayo viongozi hao walisisitiza haja ya kuzidisha ushirikiano katika sekta za maendeleo.

Mazungumzo ya viongozi hao yafanyika katika Ofisi ya Makamu wa Rais wa Indonesia, mjini Jakarta, ambako mkutano huo pia ulihudhuriwa na mawaziri wa nchi zote mbili.

Katika mazungumzo hayo Dk Shein alimpongeza mwenyeji wake kwa muwaliko wa ziara yake hiyo ambayo inaimarisha uhusiano na ushirikiano wa kihistoria uliyopo baina ya Indonesia na Zanzibar.

Share: