Habari

Dk Shein awatunishia misuli CCM wenzake Zanzibar

Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein akizungumza na viongozi wa CCM na SMZ katika mkutano wa majumuisho baada ya ziara yake katika Wilaya ya Kusini Unguja, Jumatano Februari 20, 2019

Na Khadija Khamis – Maelezo Zanzibar
Tarehe 20/2/2019

Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar Dk, Ali Mohamed Shein ameweka msimamo wa chama hicho kwamba kitawapitisha kugombea katika nafasi za uongozi wanachama wenye mapenzi ya dhati na moyo wa kukitumikia chama hicho.

Dk Shein ametoa msimamo huo wakati akihutubia wanachama na wanachi katika Ukumbi wa Hoteli ya Residence, Kizimkazi Jumatano, Februari 20, 2019 akiwa katika mfululizo wa ziara yake ya kukagua shughuli za Chama na Serikali katika Mkoa wa Kusini Unguja.

Amesisitiza kwamba chama kitawapitisha wanachama wataaobainika kufuata vyema taratibu na miongozo ya chama na wanachama wasiokuwa na sifa amesema wasipoteze muda kugombea.

“Nasema wazi asiyekitumikia chama fomu za kugombea hapewi, asigombee bure” alitahadharisha Dk Shein.

Amesisitiza kwa viongozi wa chama na serikali kufuata vyema maadili ya kazi zao ili kuwaletea wananchi maendeleo kama walivyoahidi.

“Chama kina maadili yake na serikali ina maadili yake asiyeweza kufuata maadili aache” amesema Dk Shein.

Aidha, amewataka viongozi hasa Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kutumia lugha nzuri wakati wa kuchangia hoja mbalimbali ili kuepuka kuichafua serikali na CCM.

Hata hivyo amesema kuwa wajumbe wa baraza hilo hawakatazwi kuihoji serikali kwa kuwa ndio wajibu wao wa msingi lakini wanapaswa kuzingatia matumizi mazuri ya lugha katika kuchangia mijadala.

“Serikali zote duniani zinahojiwa wajumbe wanapaswa pia kuhoji lakini kwa kuzingatia kauli nzuri” amesema Dk Shein

Kuhusu utekelezaji wa Ilani ya CCM Dk Shein amesema serikali yake imeendelea kutekeleza ahadi zake alizoahidi kupitia Ilani ya CCM ya mwaka 2015 – 2020.

Ameongeza kuwa ipo miradi mbalimbali ya maendeleo inayoendelea kutekelezwa na serikali yake ambayo haipo katika Ilani ya CCM.

Ameitaja miradi hiyo kuwa: “Ni ujenzi wa Daraja la Kibonde Mzungu na Barabara ya Mwanakwerekwe ambazo zinajengwa kwa gharama kubwa lakini hazipo katika Ilani ya CCM.”

Dk Sheini aliwahimiza viongozi kwenda katika majimbo yao ya uchaguzi kwa lengo la kujua changamoto zinazowakabili na kuzipatia ufumbuzi.

“Wakati ni sasa, sisi tunapita kusikiliza changamoto na kuzipatia ufumbuzi viongozi nanyi mwende majimboni kwenu kutekeleza kile mlichoakiahidi,” aliwasihi.

Dk Shein ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar, leo Alhamisi, Februari 21 anatarajiwa kuanza ziara kwa wilaya nne za Pemba.

Share: