Habari

Dk. Shein: Sikukurupuka kufuta michango ya elimu

May 20, 2018

Azindua mpango wa utoaji ruzuku
Serikali kuendelea kuwekeza katika elimu
NA KHAMISUU ABDALLAH

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, amesema suala la kuondosha michango kwa wanafunzi wa skuli za serikali linalenga kukuza elimu na kuhakikisha watoto wa Zanzibar wanapata haki na fursa ya elimu bila ya ubaguzi.

Dk. Shein alieleza hayo jana katika uzinduzi wa utoaji ruzuku kwa skuli 202 za sekondari za Zanzibar iliyofanyika katika ukumbi wa Shekh Idrisa Abdul-wakil Kikwajuni mjini Unguja.

Alisema, uzinduzi wa utoaji ruzuku una umuhimu mkubwa katika historia na malengo ya Mapinduzi matukufu ya mwaka 1964 ya utoaji wa elimu bure iliyotolewa na Mzee Karume, Septemba 23 mwaka huo.

Alisema kitendo cha kutangaza kufuta michango kwa wanafunzi wa skuli za sekondari ifikapo mwezi Julai hajalitoa kwa kushtukiza au jazba bali alilitoa kwa malengo na madhumuni sawa na agizo alilolitoa marehemu Karume la kuwapatia watoto wa wanyonge elimu bila ya malipo.

Alibainisha kuwa elimu ina historia kubwa hapa nchini tangu kwenye harakati za ukombozi kwani kuna miongoni mwa madhila ambayo yaliwapata wazee kabla ya Mapinduzi ikiwemo kunyimwa haki ya msingi ya kupata elimu, huku huduma za elimu na afya ambazo zilikuwa zikitolewa kwa misingi ya kikabila na ubaguzi.

Alifamisha kuwa, tamko la utoaji wa elimu bure lilotolewa na marehemu Karume lilikuwa na lengo la kuhakikisha watoto wa wanyonge wanapata fursa ya kupata elimu.

Alisema wasisi wa nchi walikumbwa na ugumu wa kuweza kutoa elimu bure kwa wananchi wote wa Zanzibar baada ya Mapinduzi matukufu ya mwaka 1964 lakini walitekeleza jambo hilo kwa vitendo.

“Kwa nini viongozi wetu walikuwa na ugumu kulikuwa na idadi kubwa ya wanyonge waliokuwa wakitaka fursa ya elimu, ufinyu wa nyezo kwa wakati ule pamoja na kuwepo walimu ambao hawakuwa tayari kuwasaidia wanyonge”, alisema Dk. Shein.

Alibainisha kuwa, hadi Mapinduzi ya mwaka 1964 yanafanyika, Zanzibar ilikuwa na skuli za msingi 62 za serikali zenye wanafunzi 19,106 na skuli nne za sekondari kwa Unguja na Pemba zilizokuwa na wanafunzi 734 huku watoto wa wafanyakazi na wakulima hawakupata fursa ya kusoma elimu ya juu na kumaliza darasa la nane au la sita.

Dk. Shein, alisema hivi sasa Zanzibar ina jumla ya skuli za maandalizi 348 zenye wanafunzi 72,151, ambapo mpaka mwaka 1964, ilikuwepo skuli moja ya Saateni.

Kwa upande wa skuli za msingi alisema, zipo skuli 442 kutoka skuli nne zenye wanafunzi 276,858 ambapo ni tofauti na mwaka 64 zilikuwa na wanafunzi 19,000 huku skuli za sekondari zipo 202 zenye wanafunzi 129,91 kutoka wanafunzi 734 mwaka 1964.

Mbali na hayo, alisema serikali imejidhatiti katika mabadiliko ya elimu nchini na haioni hasara kuwezeka katika elimu kwa kutoa elimu bure na kuipa umuhimu wa kipekee bajeti ya elimu kila mwaka kwa kuhakikisha dhamira hiyo inafikiwa.

“Tumeamua kutoa fedha za kutosha katika bajeti ya wizara ya elimu mwaka hadi mwaka ambapo kwa mwaka 2017/2018 serikali imechanga bilioni 197.29 ikilinganishwa na bajeti ya 2016/2017 ya bilioni 140.19 huku ikiahidi katika bajeti ya mwaka huu kutenga zaidi ya fedha hizo.

Zanzibarleo

Share: