Habari

Dk. Shein: Tibirinzi soko la wananchi wote

January 7, 2018

NA RAJAB MKASABA

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, amesema kuwa miongoni mwa malengo ya mapinduzi matukufu ya mwaka 1964, ni kuzifanya hali za maisha ya wazanzibari kuwa bora.

Dk. Shein alieleza hayo huko Tibirinzi Chakechake, mara baada ya kulizindua soko jipya la Tibirinzi, ikiwa ni miongoni mwa shamra shamra za kutimia miaka 54 ya mapinduzi.

Alisema ujenzi wa soko la Tibirinzi, umelenga kuinua maisha ya wananchi sambamba na kujipatia mahitaji yao na kamwe lisitumike kama kichocheo cha kubaguana misingi ya vyama, dini, jinsia au mahala mtu anapotokea.

Alisisitiza kuwa jengo soko hilo jipya ni ukombozi kwa wakulima, wafanyabiashara, wafugaji, wavuvi, wajasiriamali na wananchi wote kwa jumla kwa kuwaongezea kipato chao kitakachoimarisha maisha yao.

Alisema si vyema soko hilo likahusishwa na masuala ya kisiasa kwani ni soko la watu wote wa vyama vyote, dini zote na jinsia zote huku akiwataka wafanyabiashara watakaolitumia soko hilo kuleta bidhaa zenye ubora zitakazolingana na hadhi ya soko hilo.

Alisema kuwa ujenzi wa soko hilo ni katika hatua za kutafsiri mapinduzi ya mwaka 1964 kwa vitendo kwa kuwaletea wananchi maendeleo zaidi bila ya ubaguzi.

Alitumia fursa hiyo kueleza mafanikio sambamba na azma ya mapinduzi matukufu ya Januri 12, 1964 ambayo yamewakomboa wananchi wa Zanzibar na kukata minyororo ya chuki, udhalimu na manyanyaso.

Alieleza madhumuni ya mapinduzi ya Zanzibar ni kuwa huru hatua ambayo imepekea kupanga mambo bila ya kuingiliwa na mtu na kuweza kuongoza nchi sambamba na kuandaa mipango ya muda mrefu na muda mfupi na wakati.

Alieleza kuwa Zanzibar imepata maendeleo makubwa katika kukuza uchumi wake ndani ya kipindi cha miaka 54 huku akieleza kuwa mabadiliko makubwa ya kiuchumi, sera ya serikali maisha ya watu ambayo yote hayo ni maendeleo.

Zanzibar leo

Share: