Habari

Dk. Shein: Vyombo vya habari macho ya serikali

January 10, 2018

. Afungua studio ya kisasa ZBC
. Aahidi kushughulikia changamoto za wafanyakazi

NA HAFSA GOLO

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk.Ali Mohamed Shein, amesema, Wizara ya Habari, Utalii, Utamaduni na Michezo ndio uti wa mgongo na macho ya serikali, hivyo ni vyema watendaji wakafuata utaratibu na maadili ya kazi zao ili kuwapa taarifa sahihi wananchi.

Aliyasema hayo wakati wa uzinduzi wa studio za kisasa za Shirika la Utangazaji Zanzibar (ZBC) katika muendelezo wa shamrashamra za miaka 54 ya mapinduzi.

Alisema, wizara hiyo kupitia vyombo vyake vyake vya habari ikiwemo Serikali la Magazeti ya Serikali (Zanzibar Leo),ni sehemu muhimu ya kutoa taarifa za kweli na zinazoelimisha jamii katika miradi ya maendeleo na kiuchumi.

“Sekta ya Habari ndio kichocheo cha maisha ya binaadamu,” alisema.

Aidha alisema, katika kuhakikisha vyombo hivyo vinatekeleza majukumu yake kwa ufanisi, serikali imefanya jitihada ya kuimarisha vitendea kazi vya kisasa ili viweze kuendana na ulimwengu wa sayansi na teknolojia.

Kuhusu ZBC alisema, serikali imetumia fedha nyingi kwa ajili ya ujenzi wa studio za kisasa ambazo zitatoa huduma bora na zinazoendana na wakati ndani na nje ya Zanzibar.

Alisema, mabadiliko hayo yatakayokwenda sambamba na teknolojia ya habari duniani na kurejesha heshima na historia ya Zanzibar ambayo ina mambo mengi muhimu ya kihistoria.

“Zanzibar sio wanagenzi wa tasina ya habari na ina historia kubwa, mwaka 1885 iliamzisha gazeti ambalo lilikuwa likisimulia habari za mjini Unguja,”alisema.

Akitilia mkazo zaidi eneo hilo, alisema Zanzibar pia ndio ya kwanza kuanzisha televisheni ya rangi ikiwa na lengo la kuelimisha wananchi kufuata mila na silka yao na kuwa eneo la kujifunzia wanafunzi.

Kuhusu gazeti la Zanzibar Leo, alisema hali ilikuwa halivutii na kwa kuona umuhimu wake hakusita kuleta mabadiliko kwa kuwapatia makaazi bora na vitendea kazi ili watendaji wafanye kazi kwa ufanisi zaidi.

Aliwataka wafanyakazi wa vyombo vya habari kuhakikisha wanatumia lugha ya Kiswahili fasaha kwani kufanya hivyo ni kuheshimu lugha ya taifa lao.

“Bado matamshi na maandishi ya Kiswahili yanayotumiwa sio Kiswahili fasaha,” alsiema.

Alisema yapo mabadiliko ya utekelezaji wa majukumu kwa wafanyakazi hivyo aliwataka kuendelea kufanyakazi kwa bidii na jitihada ziendelezwe ili malengo yafikiwe.

Akimnukuu Rais wa kwanza wa Zanzibar, marehemu Abeid Amani Karume, Dk. Shein alisema moja ya hambo muhimu kwa mfanyakazi ni kuheshimu kazi yake na akiwa haheshimu hana hamu ya kazi yake na haipendi.

Alisema ni jambo la msingi kwa watendaji kujifunza kwa watu wenye uzoefu kwani ndio njia sahihi ya kufanyakazi kwa ufanisi zaidi.

Aidha aliwahimiza wafanyakazi kushindana kwa kujituma na kusoma na huo ndio msingi wa maendeleo.

Aliitaka deni wanalodai wafanyakazi wa Shirika la Utangazaji lilipwe katika kipindi cha mwezi mmoja baada ya kupokea malalamiko kwamba wapo baadhi ya wafanyakazi fedha zao zimetumiwa kulipia umeme.

Alisema sio vizuri kwa kiongozi kutoa maamuzi binafsi bila ya kushirikisha serikali kuu hasa ikizingatiwa madeni ya umeme hulipwa na serikali.

Katibu Mkuu wizara hiyo, Omar Hassan King, alisema mradi wa matengenezo ya studio mpya ulihusisha moja kwa moja na uimarishaji wa kampuni ya ZMUX ambao unaenda sambamba na ufunguzi wa mitambo ya kusambaza maudhui ya ZMUX zilizopo Rahaleo.

Alisema miongoni mwa vifaa vilivyonunuliwa ni pamoja na microwave link yenye uwezo wa kurusha chaneli nane ambapo ziligharimu shilingi milioni 67, utengenezaji wa studio tatu pamoja na vifaa vyake kiwemo na chumba chenye mahitaji maalum ili kuweza kuunganisha mawasiliano kati ya maeneo yote ya studio hizo na mambo mengine ya kitaalamu, ambapo shilingi bilioni 1.1 zilitumika.

Aidha alisema gharama zote zilizotumika katika kuimarishia ZBC –TV na radio ni shilingi bilioni 4.7.

Nae Waziri wa wizara hiyo, Rashid Ali Juma, alisifu uamuzi wa serikali kwa kuimarisha vyombo vya habari.

Zanzibar leo

Share: