Habari

Dk Shein: WanaCCM endelezeni vuguvugu la ushindi hadi 2020

Monday, May 30, 2016
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi ambaye pia ni Makamu mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein amewataka wanachama na wapenzi wa chama hicho kisiwani Pemba kuendeleza vuguvugu la ushindi wa chama hicho hadi uchaguzi mkuu ujao mwaka 2020.

Dk. Shein amesema vuguvugu hilo halina budi kwenda sambamba na usimamizi makini wa utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama hicho ya 2015/2020 ambayo ndio chachu ya ushindi wa CCM katika uchaguzi wa marudio uliofanyika mwezi Machi 2016.

Dk. Shein amesema hayo leo wakati alipokuwa akizungumza na viongozi wa chama hicho kuanzia ngazi ya mashina hadi wilaya wa wilaya ya Wete Mkoa wa Kaskazini Pemba.

“Kazi ya chama cha siasa wakati wote ni kuendeleza vuguvugu la kisiasa mbalo litawaweka wanachama na wapenzi wake pamoja kwa lengo la kuimarisha uhai wake na kujipambanua katika kutekeleza malengo yake kwa jamii” Dk. Shein alisisitiza.

Aliwaeleza viongozi hao kuwa kazi kubwa inayowakabili wana CCM na wananchi ni “kutekeleza Ilani” na kuangalia namna gani serikali itafanya kazi kwa kutekeleza Ilani hiyo.

Dk. Shein aliwapongeza na kuwashukuru viongozi hao kwa kusimama imara na kwa ujasiri mkubwa hadi CCM ikaibuka na ushindi wa kishindo kwa mgombea wake wa urais huku ikikomba viti vyote vya uwakilishi na udiwani Unguja na Pemba.

Makamu Mwenyekiti huyo wa CCM Zanzibar aliwakumbusha viongozi hao kuwa mwaka ujao chama hicho kitafanya uchaguzi wake kuwapata viongozi hivyo hawana budi kuanza kujiandaa.

“Ni uchaguzi utakaoimarisha chama chetu kwa kupata viongozi makini na wenye uwezo wa kukiongoza chama chetu na kutuletea ushindi katika uchaguzi wa 20202” Dk. Shein alieleza na kuwasisitizia viongozi hao kuwa sasa ni kazi tu hakuna kulala.

Katika hatua nyingine Makamu Mwenyekiti huyo wa CCM aliwaeleza viongozi hao kuwa chama hakitawavumilia viongozi ambao hawatatimiza majukumu yao hivyo kuwatanabahisha viongozi katika chama hicho kuepuka ubabaishaji.

Dk. Shein yuko kisiwani Pemba wa ziara ya siku tatu kuwashukuru wanachama na wapenzi wa chama hicho kwa ushindi mkubwa walioupata katika uchaguzi mkuu uliopita.

Zanzinews

Share: