Habari

Dk Shein : Watanzania walioko nje wana nafasi kuchangia maendeleo ya taifa

Thursday, September 18, 2014

STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar 18 Septemba, 2014

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesema mpango wa serikali wa kuwa na mawasiliano ya karibu na watanzania wanaoishi ughaibuni (Diaspora) lengo lake ni kuwashajiisha watanzania hao kushiriki kikamilifu katika kujenga nchi yao kama wanavyofanya raia wa nchi nyingine duniani.

Amesema Serikali imejiandaa vyema katika kutekeleza mpango huo tangu ulipoanza rasmi kwa kufanya mkutano wa kwanza wa watanzania wanaoishi ng’ambo mjini London, Uingereza mwaka 2008.

Akizungumza na watanzania wanaioshi nchini Comoro wakati wa ziara yake nchni humo, Dk. Shein aliwaambia watanzania hao kuwa wana nafasi nzuri ya kuchangia maendeleo ya nchi yao kwa namna mbalimbali ikiwemo kuwekeza wao binafsi, kutafuta wawekezaji na pia kutumia utaalamu wanaoupata wakiwa nje.

Katika mkutano huo uliofanyika katika Ofisi za Ubalozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Comoro, Dk. Shein aliwahakikishia watanzania hao kuwa nyumbani ni shwari huku watanzania wenzao wakiendelea na jitihada za kujiletea maendeleo.

Alitumia fursa hiyo pia kuwaeleza jitihada mbalimbali zinazofanywa na Serikali katika kuimarisha uchumi ikiwemo mipango ya kuwawezesha wananchi kiuchumi ikiwa ni sehemu ya jihada za kupambana na tatizo la ajira.

Dk. Shein aliwataka watanzania hao kuunga mkono jitihada za viongozi wa Tanzania na Comoro za kuimarisha uhusiano mzuri na wa kindugu uliopo kati ya Comoro na Tanzania.

Alisema uhusiano huo si wa kupita wala wa kupanga bali ni matokeo ya historia karne nyingi ya maingiliano kati ya watu wa visiwa vya Comoro na Tanzania.

Kwa hivyo aliwaeleza watanzania hao kuwa ziara yake nchini humo ni sehemu ya jitihada hizo na kufafanua kuwa dhamira ya sasa ni kutaka ushirikiano huo uwe na nguvu zaidi na kuendelezwa kwa kasi zaidi kwa yale watu wa nchi hizo walioyokuwa wakisaidiana kwa sababu ya udugu wao lakini pia kuweka utaratibu rasmi wa kiserikali kwa maeneo mapya ya ushirikiano.

Hivyo alieleza matumaini yake kuwa mwishoni mwa ziara yake makubaliano ya ushirikiano yatasainiwa kwa manufaa ya watu wa wa Comoro, Zanzibar na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ujumla.

Katika risala yao kwa Mhe Rais watanzania hao walieleza kuridhishwa na hatua za serikali katika kuimarisha uchumi na kuleta maendeleo huko nyumbani.

Katika risala hiyo iliyosomwa na Bi Maimuna Yusuf, watanzania hao ambao wengi wao ni wafanyabiashara waliiomba Serikali kurejesha safari za moja kwa kwa moja za meli kati ya Zanzibar na Comoro.

Watanzania hao waliiomba pia Serikali kuzungumza na Serikali ya Muungano wa Comoro kuangalia uwezekano wa kupunguza kodi mbalimbali wanazotozwa wafanya biashara wakati wanapoingiza bidhaa kutoka nje kwa kuwa kodi hizo ni kubwa sana na zinaathiri biashara.

Kabla ya kuzungumza na watanzania hao, Dk. Shein alikagua sehemu sehemu mbalimbali za ubalozi huo na pia kuzindua tovuti ya ubalozi na baadae kukabidhi muhuri rasmi kwa ajili ya kuanzisha huduma za utoaji viza kwa wananchi wa Comoro wanaofanya safari kuja Tanzania.

Kabla ya kuanza huduma hizo raia wa Comoro walikuwa wakipatiwa viza mara wanapowasili nchini na kusababisha malalamiko kuwa wanachelewa kutokana na misululu mirefu wanapowasii viwanja vya ndege.

Akizungumza katika uzinduzi wa Tovuti hiyo, Balozi wa Tanzania nchini Comoro, Balozi Chabaka Kilumanga alieleza umuhimu wa tovuti katika mazingira ya sasa ya upashanaji na usambazaji habari ambapo alisema hivi sasa tovuti ndio mlango ya wa nchi na taasisi kwa kuwa watu wengi wanapohitaji taarifa kuanzia kwenye tovuti za nchi au taasisi husika.

Kuhusu huduma za viza, Balozi Kilumanga alieleza kuwa raia wa Comoro wamekuwa wakipatiwa viza wanapowasili nchini Tanzania lakini wamekuwa wakilalamikia misongomano hivyo serikali imeamua kuondosha kero hiyo kwa kutoa huduma hiyo nchini Comoro.
Akitoa maelezo kuhusu tovuti hiyo, Afisa wa Ubalozi huo Jabir Ali Mwadini alisema tovuti hiyo imenzishwa ili kurahisisha mawasiliano kati ya ubalozi na wadau mbalimbali.

Alisema miongoni mwa taarifa zitakazopatikana katika tovuti ni zote zinazohusu Tanzania ikiwemo historia na maendeleo katika nyanja zote. Aidha kutakuwa na kurasa maalum zikiwemo za uhusiano kati ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Muungano wa Comoro, ukurasa wa watanzania wanaoishi Comoro ambao wataweza kujisajili moja kwa moja kupitia ukurasa huo na ukurasa wa masuala ya utalii.

Katika ziara hiyo Mheshimiwa Rais amefuatana na mke wake Mama Mwanamwema, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Ikulu na Utawala Bora Dk. Mwinyihaji Makame Mwadini, Naibu wa Waziri wa Kilimo na Maliasili Bibi Mtumwa Kheir Mbarak na Mshauri wa Rais Ushirikiano wa Kimataifa, Uwezeshaji na Uchumi Balozi Mohamed Ramia Abdiwawa.

Wengine ni Kadhi Mkuu wa Zanzibar Sheikh Khamis Haji, Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo Bwana Ali Saleh Mwinyikai, Katibu Mkuu Wizara ya Uwezeshaji, Ustawi wa Jamii, Vijana, Wanawake na Watoto Bibi Asha Ali Abdulla na Kaimu Mkurugenzi Idara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Zanzibar Bwana Kombo Abdulhamid Khamis.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi na ujumbe wake wamerejea nchini leo mchana ambapo alilakiwa na viongozi mbalimbali wakiongozwa na Makamu wa Pili wa Rais Balozi Seif Ali Iddi.

Zanzinews

Share: