Habari

DPP apiga chenga maandishi, aibuka na rufani mara dufu!

Salma Said,

Mahakama Kuu ya Zanzibar imesema haitasikiliza kesi inayowakabili viongozi wa Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu Zanzibar (JUMIKI) hadi pale Mahakama ya Rufani itakapotoa maamuzi juu ya rufani zilizokatwa huko.

Upande wa mashitaka wa serikali umekata rufani Mahakama ya Rufani ukipinga maamuzi ya Jaji Fatma Himid Mahmoud anayesikiliza kesi hiyo aliyoutaka upeleke kwa maandishi sababu za kuzuia dhamana ya washitakiwa hao.

Mwanasheria wa serikali, Raya Issa Mselem aliiambia Mahakama jana kuwa Mkurugenzi wa Mshitaka (DPP), Ibrahim Mzee Ibrahim hakuridhishwa na maamuzi hayo ya Mahakama hasa ya kuwasilisha kwa maandishi sababu za kupinga dhamana kwa washitakiwa hao.

Alidai kuwa kutokana na hali hiyo DPP ameamua kukata rufani Mahakama ya Rufani. Kwa mfumo wa Mahakama Tanzania Mahakama ya Rufani ni suala la Muungano.

Hiyo itakuwa rufani ya pili kukatwa na upande wa mashitaka katika kesi hiyo baada ya awali kupinga maamizi ya Jaji Abraham Mwampashi wa Mahakama Kuu Zanzibar aliyefuta maagizo ya Mrajis wa Mahakama Kuu ya Zanzibar, George Kazi likiwemo la kuwanyima dhamana washitakiwa hao.

Wakili wa utetezi, Salum Toufiq ameiomba Mahakama kutokubaliana na uamuzi huo kwani upande wa mashtaka unahalifu amri ya Mahakama kama kulikuwa na sababu za msingi ilikuwa waeleze mapema .

Jaji Fatma alisema amesikia maombi ya pande zote mbili hivyo upande wa mashitaka unayo haki ya kukata rufani na atasikiliza kesi hiyo baada ya maamuzi ya Mahakama ya Rufani au zikipita siku 60 bila ya maamuzi.

Washitakiwa hao ambao wataendelea kusota rumande ni Farid Hadi Ahmed (41) mkaazi wa Mbuyuni,Mselem Ali Mselem (52) mkaazi wa Kwamtipura, Mussa Juma Mussa (47) mkaazi wa Makadara na Azan Khalid (48) mkaazi wa Mfenesini.

Wengine ni Suleiman Juma Suleiman (66), mkaazi wa Makadara, Khamis Ali Suleiman (59) mkaazi wa Mwanakwerekwe, Hassan Bakar Suleiman (39) mkaazi wa Tomondo, Ghalib Ahmada Juma (39) mkaazi wa Mwanakwerekwe na Abdallah Said (48) mkaazi wa Misufini

Washitakiwa hao wamefikishwa mahakamani kwa madai ya kuharibu mali, uchochezi, ushawishi na kuhamasisha fujo na kuhatarisha usalama.

Tagsslider
Share: