Habari

DR. SHEIN AKUTANA NA SHAMHUNA KUANGALIA MPANGO KAZI.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk. Ali Mohamed Shein, leo amenza vikao maalum vya muendelezo wa kukutana na Wizara za Serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika kuangalia mpango kazi wa Wizara hizo katika utekelezaji wa Bajeti ya mwaka 2011/2012 kwa kipindi cha robo ya pili.

Katika vikao hivyo vinavyofanyika Ikulu mjini Zanzibar, Rais Dk. Shein leo ameanza kukutana na Uongozi wa Wizara ya Ardhi, Makaazi, Maji, Nishati na baadae alikutana na Uongozi wa Wizara ya Afya.

Akizungumza na Uongozi wa Wizara hizo kwa nyakati tofauti, Dk. Shein alisema kuwa utaratibu huo utazisaidia kwa kiasi kikubwa Wizara zote kuweza kujitathmini wenyewe kwa kuangalia kila robo mwaka hatua iliyofikiwa pamoja na mambo waliyoyafanya.

Alieleza kuwa hatua hiyo pia, itasaidia kupata kujua mambo waliyoyapanga wanaweza kuyatekekeza vipi kutokana na nyenzo walizozipata sanjari na bajeti yao waliyoiandaa.

Kwa upande wa Wizara ya Ardhi, Makaazi, Maji na Nishati, uongozi wa Wizara hiyo ulieleza mafanikio yaliopatikana kutokana na vikao hivyo na kueleza kuwa kwa upande wa sekta ya maji lengo la kuongeza upatikanaji wa maji safi na salama kufikia asilimia 95 kwa watumiaji wa mjini na asilimia 75 kwa watumiaji wa vijijini ifikapo mwaka 2015 lipo pale pale.

Uongozi huo ulieleza kuwa utafiti wa maji katika Mkoa wa Mjini Magharibi bado unaendelea baada ya kumpata mshauri mwelekezi kutoka Kampuni ya NIRAS ya Denmark ambapo pia, ulieleza hatua inazozichukua ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma hiyo muhimu.

Aidha, uongozi huo ulieleza kuwa kazi ya uchimbaji wa visima viwili vya Chumbuni,ulazaji wa mambomba ya maji katika maeneeo ya Kijichi na Kinuni,uwekaji wa pampu na Mota katika maeneo ya Dimani pamoja na uchimbaji wa visima viwili vya Chokocho Michenzani Pemba vimekamilika.

Pia, uongozi huo ulieleza kuwa ujenzi wa tangi la maji Kizimkazi, Micheweni na Kama tayari umekamilika na wananchi wameshaanza kutumia huduma hiyo ambapo ujenzi wa tangi la Ziwani Pemba umo katika hatua za kumalizika.

Uongozi ulieleza kuwa ulazaji wa mabomba ya maji katika maeneo ya Kizimkazi tayari umekamilika na kwa upande wa Shumbavyamboni kazi bado inaendelea.

Kwa upande wa Sekta ya Nishati uongozi huo ulieleza kuwa tathmini na malipo ya fidia ya mali na mazao kwa waathirika wa mradi wa MCC imekamilika.

Aidha, uongozi huo ulieleza kuwa kupitia shirika lake la umeme Zanzibar ZECO, limo katika juhudi za kuzungumza na Benki za hapa nchini zikiwemo PBZ na NMB kwa ajili ya kuwasaidia wananchi kuungiwa huduma hiyo kwa njia ya mkopo.

Uongozi huo ulieleza kuwa kwa upande wao hivi sasa Shirika hilo limesitisha mkopo wa kuungiwa huduma hiyo kutokana na ukosefu wa fedha na inachofanya hivi sasa ni kuendelea kukusanya kile waliochowakopesha wananchi waliyowaungia huduma hiyo hapo siku za nyuma.

Pamoja na hayo, uongozi huo ulieleza kuwa hatua za ukamilishaji wa waya wa baharini wenye kilomita 39.5 kutoka Ras Kiromoni Dar-es-Salam hadi Ras Fumba Unguja zinaendelea na unatarajiwa kukamilika wakati wowote. Pia, umeeleza azma na mikakati iliyowekwa ya kuepeleka huduma ya umeme katika visiwa vidogo vidogo vya Pemba.

Kwa upande wa uongozi wa Wizara ya Afya, uongozi huo ulieleza mikakati na mipango yake katika kuendeleza huduma ya afya hapa nchini. Aidha, Wizara hiyo ilitoa shukurani kwa Dk. Shein kutokana na hatua yake hiyo ambayo wameielezea kuwa ni chachu ya utendaji wa kazi zao

CHANZO ZANZIBAR ISLAMIC NEWS

Share: