Habari

Dr Shein atakutana na Wazanzibar waliopo Emirates?

Dr Ali Mohamed Shein, Rais wa Zanzibar akiwa na mwenyeji wake Sheikh Mohammed Bin Rashid Al Maktoum, Mkuu wa Dubai wakinywa qahwa huku wakiendelea na mazungumzo ya kuimarisha ushiriakiano wa kiuchumi baina ya nchi mbili hizi

Kawaida ya viongozi wa nchi wanapotembelea nchi nyengine kwa ajili ya kujenga urafiki, umoja, na mashirikiano baina ya nchi hizo, pia hupata fursa ya kukutana na wananchi wake wanaoishi nchi hiyo. Ili kujiweka karibu , kubadilishana fikra na uzowefu waliopata, pia kuhamasisha michango yao kwa nchi yao ya asili.

Niliposoma taarifa ya ziara ya Dr Shein, Rais wa Zanzibar inayoendelea nchini Emirates, sikuona sehemu (kwenye ratiba) inayoonyesha mbali ya kukutana na wakuu wa nchi ya Emirates, Dr Shein atakuwa na mkutano na Wazanzibar wanaoishi nchi humo.

Nchini Emirates kuna idadi kubwa ya Wazanzibar wanaoishi, kufanyakazi pia ni kituo kikubwa cha Wafanya biashara wa Zanzibar ambao kila leo hupanda ndege kwenda Dubai, Sharja kuchukuwa mizigo. Mchango wao kwa Zanzibar katika eneo la ushuru na mapato ni mkubwa sana.

Pia kwa vile wengi wa Wazanzibar waliokwenda Dubai ilikuwa bado haijaendelea walikuwa ni miongoni mwa walioshiriki na kuchangia maendeleo ya Emirates. Hivyo Dr Shein angepata fursa ya kukutana na Wazanzibar hao ingekuwa thamani kubwa ya ziara yake kwa wananchi wake waliopo Zanzibar na wale waliopo Emirates.

Ikumbukwe kuwa ni azma ya Dr Shein kuwatambua na kuwajumuisha Wazanzibar walioko nje za nje, kushiriki kikamilifu harakati za kuleta maendeleo nchi mwao. Katika hatua hio Dr Shein aliunda idara maalum ya Mambo ya Nje na Shughuli za Wazanzibar waliopo Nje (Wazanje). Idara hii ipo kwa muda wa miaka 7 sasa, mwanzo ilikuwa chini ya unaibu Katibu Mkuu Said Abdalla Natepe (Marehemu) na Mkurugenzi Khamis Ali Khamis (Marehemu)

Sasa hivi idara hii ipo chini ya unaibu Katibu Mkuu Bi Rahma na Mkurugenzi Bi Adila. Tukiamini kuwa kuundwa kwa idara hii sio tu kutengeneza kitengo cha kupata ajira na watu kupata mishahara bali kufanya kazi kwa uweledi na ufanisi kufikia malengo na madhumuni ya kuundwa kwake. Pia kuendeleza yale yote yaliasisiwa na wale waliotangulia kuiongoza idara hii. Hivyo lilikuwa jukumu lao kuratibu mkutano huo baina ya Dr Shein na Wazanzibar waliopo Emirates.

Faida ni nyingi hakuna haja ya kuzitaja, nikumbushe moja tu, wakati wa utawala wa Dr Salmin Amour Juma kulikuwa na kampuni ikiitwa Zanzibar State Engineering ambayo wamiliki wake ni Wazanzibar wanaoishi Emirates.

Ni imani yangu kuwa mkutano huu umefanyika au utafanyika kwa maslah ya maendeleo ya watu wetu na nchi yetu. Ziara ya wiki moja haikoseshi muda wa kufanya kikao kima hiki ikiwa imepangaliwa ipasavyo.

Share: