Habari

Dr Sheini Mazalio ya Ubaguzi yako Kisonge lakini Umeufyata kuwambia.

Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein, ameitahadharisha jamii juu ya vitendo vya ubaguzi, bugudha na manyanyaso kwa misingi ya kisiasa na kueleza kuwa vinaiangamiza jamii.

Akizungumza na wananchi wa kijiji cha Maziwang’ombe, wilaya ya Micheweni, mkoa Kaskazini Pemba jana, Dk. Shein alisema wananchi ni lazima wazingatie sheria ya kuanzishwa vyama vingi, ambayo inaeleza wazi kuwa kila mwananchi ana haki na uhuru wa kujiunga na chama chochote cha siasa na kushiriki siasa bila kubaguliwa.

“Tusiwarithishe chuki wala ugomvi watoto wetu kwani tukiendelea kufanya hivyo tutakuwa tunaiangamiza jamii yetu ambayo tangu mapinduzi ya mwaka 1964 ilikuwa ikiishi kwa amani na upendo,” alisema Dk. Shein.

Aliwaeleza wananchi hao kuwa tofauti za itikadi za kisiasa isiwe kisingizio cha kufanyiana chuki, kubaguana na kubugudhiana au kutengana, kwani watu wote ni ndugu na wanahitaji kuishi pamoja kwa upendo na kusaidiana.

“Mzazi atabaki kuwa mzazi, mtoto atabaki kuwa mtoto, ndugu atabaki kuwa ndugu; inakuwaje tunafanyiana visa na kuhasimiana kwa kuwa tu mwenzetu mmoja ametoka chama hiki kwenda chama kingine?” aliuliza Dk. Shein.

Dk. Shein alifika kijijini hapo kukabidhi boti na mashine ya kisasa yenye injini ya uwezo wa nguvufarasi 40 kwa kikundi cha Heri ya Moyo Mmoja kinachoundwa na vijana waliohama chama cha CUF na kujiunga na CCM.

Vijana hao walifanyiwa visa vya kunyimwa huduma muhimu na hata kuondolewa katika kazi za pamoja ikiwamo kutengwa katika shughuli za ushirika ndani ya kijiji hicho.

Katika mkutano huo uliohudhuriwa na mamia ya wananchi wa kijiji hicho na vijiji vya jirani, Dk. Shein aliwakumbusha wananchi kuzingatia historia yao na kuwahimiza kudumisha amani na utulivu na kuwaonya kutoshiriki vitendo vya uvunjifu wa amani kwa kuwa vyombo vinavyohusika na ulinzi na usalama havitawavumilia.
IMG_6750
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein akimkabidhi Boti na Mashine Bw.Shamte Hamadi Juma wa Kijiji cha Maziwa Ng’ombe Wilaya ya Micheweni kwa niaba ya kikundi cha Wavuvi Kheri Moyo Mmoja Pemba hafla ya makabidhiano hayo ilifanyika jana kijijini hapo

Chanzo (Nipashe)

Share: