Habari

Duni: Hivi, akina Warioba hawaoni katiba kuvunjwa?

Dar es Salaam. Aliyekuwa mgombea mwenza wa urais, Juma Duni Haji amewalaumu viongozi mbalimbali wastaafu na serikali kwa kutoa matamko kuwa kuna matatizo Zanzibar, lakini hauna hata mmoja anayesema katiba imevunjwa.

Mwanasiasa huyo Machachari nchini pia amesema uchaguzi wa rais wa Zanzibar,wawakilishi na madiwani ukifanyika machi 20 kama ilivyotangazwa na tume ya uchaguzi, Rais John Magufuli naye atakuwa amevunja katiba.

Kauli ya Duni Haji imekuja baada ya Viongozi kadhaa na watu maarufu nchini kutoa tahadhari kuhusu hali ya kisiasa inayoendelea Zanzibar, wakitaka haki ifuatwe baada ya ZEC kufuta matokeo ya uchaguzi wa oktoba 25 na kutangaza mwingine utakaofanyika Machi 20, huku chama kikuu cha upinzani ,CUF kikipinga vikali.

Katika mahojiano maalum na Mwananchi, Duni alisema anashangazwa na Rais John Magufuli, Jaji Joseph Warioba na Jaji Mark Bomani kushindwa kusema Katiba Zanzibar imevunjwa hasa baada ya kufutwa kwa uchaguzi.

“Jaji Warioba anasema ‘jamani Zanzibar kuna hatari’, lakini hasemi Katiba imevunjwa, Bomani anasema ‘jamani Zanzibar kuna hatari’, lakini hasemi Katiba imevunjwa,” alisema Duni.

“Kama viongozi wote hao hawaoni Katiba imevunjwa, basi ni miujiza kujiingiza kwenye uchaguzi,” alisema Duni, ambaye kabla ya uchaguzi alijivua wadhifa wa makamu mwenyekiti wa CUF na kujiunga na Chadema alikopewa nafasi ya kuwa mgombea mwenza wa urais wa Edward Lowassa chini ya makubaliano maalum ya vyama hivyo viwili.

Hata hivyo, Jaji Warioba hakutaka malumbano baada ya kuulizwa kuhusu maoni yake kuhusu kauli hiyo ya Duni Haji,

“Sitaki kujibishana na yeyote juu ya mgogoro uliopo Zanzibar,” alisema Jaji Warioba na kusisitiza:

“Hakuna asiyejua kuwa Zanzibar kuna tatizo, lakini sitaki kuingia kwenye malumbano na mtu yeyote. Kila mmoja na maoni yake. Ni vema vyombo vya habari vikajikita kutafuta suluhu badala ya kuangalia yasemwayo.”

Kwa upande wake, Jaji Bomani hivi karibuni alisema kitendo cha ZEC kutangaza tarehe ya marudio ya uchaguzi wa rais, wawakilishi na madiwani kimepunguza imani ya wananchi kwa chombo hicho.

Katika mahojiano na Mwananchi, Duni Haji alisema ukifanyika uchaguzi Zanzibar Machi 20, Rais Magufuli atakuwa amevunja Katiba.

Pia, alisema maana yake ni kwamba kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania uchaguzi ni wa vyama vingi, lakini Zanzibar uchaguzi ni wa chama kimoja.

“Wito wangu ni lazima tuheshimu Katiba. Suala la ubabe halifai. Hakuna ubabe ambao unafanikiwa. Ukitaka ubabe utakurudisha kwenye meza,” alisema.

Kuhusu majadiliano yanayoendelea, Duni alisema suala hilo ni la amani na ndiyo maana katibu mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad, ambaye ni mgombea wa urais Zanzibar, aliamua wajadiliane kwa kuwa vurugu zozote zitakazotokea Zanzibar zitawarudisha mezani.

“Hivi sasa anachokifanya Seif ni kuwaambia tukae, tujadili kabla ya kutokea mapambano yoyote,” alisema Duni kwa msisitizo na kudai kuwa suala lililopo ni kwamba wengine hawana haki ya kutawala.

“Kama ni hivyo basi, hatuna hata haki ya kuishi? Na kama hatuna watutafutie pa kuishi,” alisema.

Kwa kujigamba Duni alisema kama wanataka uchaguzi kweli Tume huru isimamie uchaguzi huo ili haki itendeke.

“Ni ubabe tu unaendelea. Tukiingia kwenye uchaguzi ni kuhalalisha uovu uliofanywa na Jecha Salum Jecha,” alisema na kuongeza kuwa iwapo kutakuwa na chombo kingine huru cha kusimamia uchaguzi, CCM haitaambulia lolote kwenye marudio.

Kuhusu hatma yake Chadema

Kuhusu mustakabali wake kwenye chama chake cha CUF baada ya kuhamia Chadema kwa makubaliano maalum, Duni alisema anaendelea kuwa mwanachama wa chama hicho kikuu cha upinzani nchini na kwamba hakutimuliwa CUF.

“Ilikuwa ni political agreement (makubaliano ya kisiasa) ya jinsi ya kuunda timu bora ya ushindi ndiyo nikaambiwa na CUF na wananchi wakaridhia, nikaingia kwenye mapambano,” alisema.

Alisema kwa sasa anaingia kwenye kikao cha Baraza Kuu la CUF kwa kuwa ni makamu mwenyekiti wa zamani wa chama hicho kikuu cha upinzani visiwani, na anatoa maoni yake ambayo si lazima yakubaliwe.

mwananchi

Tagsslider
Share: