Habari

Dunia yapaza sauti alichofanyiwa Lissu

Wafuasi wa CHADEMA mjini Dar es Salaam wakiwa kwenye maandamano ya amani yaliyoanzia Makao Makuu Kinondoni, mjini Dar es Salaam Ijumaa, 8/9/2017 ikiwa ni kuonyesha hisia za kulaani kushambuliwa kwa risasi kwa Tundu Lissu.

Lakini, Dar es Salaam maandamano yakifanyika Ikungi, Mkoani Singida inaelezwa hali ilikuwa ni tofauti baada ya wanachama na viongozi wa CHADEMA kushikiliwa na polisi wakidaiwa kufanya maandamano. Wanachama na wafuasi hao wa CHADEMA walikuwa na lengo la kufanya maandamano ya amani, kulaani shambulio la risasi dhidi ya Lissu.

Waandishi wa Mwananchi/MTANZANIA
Saturday, Septemba 9, 2017

WATU 11 wakiwemo madiwani wanne wa Halmashauri ya Wilaya ya IKungi. Mkoani Singida wamekamatwa wakiwa na mabango yenye ujumbe wa kuishinikiza serikali kutoa tamko kuhusu kuvamiwa na kupigwa risasi Mwanasheria Mkuu wa CHADEMA, Tundu Lissu.

Mkuu wa Wilaya ya Ikungi, Miraji Mtaturu amesema watu hao wamekamatwa na polisi leo Ijumaa (siku ya tarehe 8/9/2017) mchana wakiwa na mabango katikati ya mji wa Ikungi, wakiwa kwenye harakati za kuhamasisha maandamano:

“Walitaka kufanya maandamano, tuliwawahi kabla hawajaanza, miongoni mwao wapo waliotokea Arusha na Dodoma, kwa hiyo wamekamatwa kwa ajili ya mahojiano zaidi,” amesema Mtaturu.

Amesema tukio la Lissu ambaye ni Mbunge wa Singida Mashariki kupigwa risasi halijatokea Singida, hivyo hawataruhusu maandamano ya aina yoyote yanayoweza kuhatarisha amani..

DEREVA WA LISSU: Anasema aachiwe bado hayuko sawa.

Wakati huo huo: Dereva aliyekuwa akimwendesha Tundu Lissu, Alhamisi, 7/9/17 wakati tukio la kupigwa risasi lilipomkuta, amesema hawezi kuzungumza kitu chochote kwa sasa kutokana na kutokuwa sawa, baada ya bosi wake huyo kunusurika kifo.

Akizungumza na Gazeti la MTANZANIA  la Jumamosi, 9/9/17 Dereva Adam alimuomba mwandishi wa habari hii amwache kwanza hadi atakapokuwa sawasawa: “Siko sawa, siwezi kuzungumza chochote kwa sasa, bado siko sawa,” alisema kwa ufupi.

Dereva huyo ndiye mtu muhimu na anayejua mbinu gani alizozitumia kumuokoa Lissu, kunusurika asipatwe na risasi nyingi mwilini, kati ya risasi 28 hadi 32 zilizoshambulia gari lake.

Si hilo tu, ndiye mtu pekee anayeweza kuelezea kwa undani tukio hilo alivyoliona na jinsi alivyoweza kunusurika risasi zilizopigwa kwenye gari alilokuwamo pamoja na Lissu.

Angekuwa sawa, pia angeweza kuelezea mazingira ya tukio lenyewe, iwapo kulikuwa na walinzi katika eneo hilo ambalo nyumba ya Lissu ipo jirani kabisa na nyumba ya Naibu Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson inayolindwa na askari wenye silaha.

Adam iwapo angezungumza, angejibu pia maswali iwapo ana mafunzo yoyote ya kiaskari au ulinzi na usalama juu ya mbinu za kujihami katika kujikinga na mashambulizi.

Dereva huyo, pia angeweza kujibu maswali wanayojiuliza watu wengi iwapo kama anaweza kuwatambua wahusika wa tukio hilo, ambalo katika moja ya maelezo yake, alisema kuwa aliliona gari jeupe aina ya Nissan lililokuwa likiwafuata ambalo watu waliomjeruhi Lissu, walikuwamo ndani.

Kadhalika, angeweza kujibu pia ni watu wangapi walihusika kummiminia risasi Lissu na ndani ya gari pia kulikuwa na watu wangapi.

Alihamisi siku ya tukio, kiongozi mmoja wa CHADEMA alisema, dereva huyo aliwaambia kuwa wakati wanatoka bungeni, waliliona gari hilo likiwafuatilia kwa nyuma, hivyo akalitilia shaka kwa sababu Lissu, amekuwa akilalamika kwamba kuna watu wanamfuatilia.

“Kwa hiyo, alichokifanya ni kwamba, baada ya kukaribia kuingia nyumbani kwake, dereva alimshauri Lissu asiteremke kwenye gari ili ajiridhishe na usalama wa gari hilo:

“Wakati wanasubiri kuona mwisho wa hilo gari , mfyatuaji wa risasi alishuka kwenye gari hilo lililokuwa nyuma yao na kumimina risasi kwa kutumia bunduki aliyokuwa nayo na kisha akarudi kwenye gari na kuondoka.”

Alisema kiongozi huyo kwa kifupi, akikariri maelezo ya dereva huyo, ambaye alionekana pia hospitali akiwa amebeba nguo za Lissu, zilizokuwa zimetapakaa damu.

Zitto: Kunahitajika uchunguzi wa kimataifa..
Mbunge wa Kigoma Mjini na Kiongozi Mkuu wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe amesema kunahitajika uchunguzi wa kimataifa dhidi ya shambulio la Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu: “Washambuliaji wamelenga kutunyamazisha.”

Akituma ujumbe wake kwenye Twitter, Zitto amesema kwamba vyombo vya ndani  vinaweza visiaminike kutokana na mkanganyiko wa fikra na mawazo ya kada mbali mbali na uzito wa tukio hilo.

Amesema kwamba: “Washambuliaji wa Lissu wamelenga kutunyamazisha. Iwapo tutaendelea kunyamaza, watashinda. Hatuwezi kuwapa nafasi hiyo, tunaongea kuhusu haki.”

SIRRO: TUNAWASAKA
Wakati matamko hayo yakitolewa Jeshi la Polisi limesema limejizatiti kwa dhati kuwasaka wahusika wa tukio la kushambuliwa Lissu kwa vile limewastaajabisha wengi.

Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Simon Sirro alisema katika hatua za awali tayari ametuma timu ya wapelelezi kwenda Dodoma kwa ajili ya kuongeza nguvu na kuwa upelelelezi huo utafanyika kwa umakini wa hali ya juu.

“Nataka niwathibitishie nyinyi waandishi wa habari kuwa Jeshi la Polisi liko imara na linafanya kazi yake imara. Lakini pia nataka muelewe hili tukio tumelichukulia ‘serious’ hivyo tuombe wananchi waendelea kutupa ushirikiano,” alisema Sirro.

SALAMU ZA MASIKITIKO ZA KUMUOMBEA LISSU

Matamko kutoka sehemu mbalimbali yametolewa kumuombea afya njema mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu na kulaani shambulio la risasi dhidi yake na kutaka hatua kali zichukuliwe kwa waliohusika.

Lissu alipigwa risasi siku ya Alhamisi, Septemba 7, 2017 akiwa na dereva wake katika gari nje ya nyumba yake mjini Dodoma na watu wasiojulikana, tukio ambalo limezua mshtuko mkubwa ndani na nje ya nchi.

Spika wa Bunge, Job Ndugai Ijumaa, 8/9/17 alisema kuwa risasi zilizompata Lissu katika mwili wake ni tano; mbili mguuni, mbili tumboni na moja mkononi. ‘Risasi 28 mpaka 32 zilishambulia gari lake.’

Matamko hayo yalianza kumiminika juzi jioni wakati Chama cha Wanasheria Kenya (LSK) kilipolaani kupigwa risasi kwa Lissu ambaye ni Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS).

Rais wa LSK, Isaac Okero alisema tukio hilo limewashtua wanasheria wote wa Kenya na mpaka nje ya Kenya, kwa sababu limekosa utu na huruma za maumbile za binadamu.

Naye, Mwenyekiti wa zamani wa LSK, Eric Mutua ameiomba Serikali ya Kenya kumpa Lissu ulinzi wakati akiwa kwenye matibabu hospitalini hapo:

“Hatuna uhakika kama watu waliotaka kumuua (Lissu) nchini Tanzania, hawatafikiria kuja hapa kutimiza lengo lao. Ni muhimu kwa Serikali ya Kenya kuweka askari watakaomlinda kuhakikisha anakuwa salama,” alisema Mutua.

Marekani yasema ni upuuzi

Taarifa ya Ubalozi wa Marekani Tanzania, ilielezea kusikitishwa na tukio la kushambuliwa kwa risasi mbunge huyo ikisema, “Tunalaani kitendo hicho cha kipuuzi na cha kutumia nguvu.”

Ubalozi huo ulisema unaungana pamoja na Watanzania kumtakia nafuu ya haraka Lissu, ili arejee katika majukumu yake.

Ulaya, THBUB walaani

Nao, Umoja wa Ulaya (EU) ulitoa tamko kulaaani shambulizi hilo na kutaka wahusika wake wasakwe, wakamatwe na kufikishwa mbele ya vyombo vya sheria.

Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, EU ilisema inaungana na Serikali ya Tanzania, Bunge na vyama vya kiraia kulaani tukio hilo:

“Ujumbe wa Umoja wa Ulaya unaungana na Serikali ya Tanzania, Bunge na taasisi za kiraia kulaani vikali jaribio dhidi ya maisha ya Tundu Lissu, mbunge wa Singida Mashariki wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” inasema taarifa ya EU.

Taarifa hiyo fupi inataka mamlaka ziwafikishe haraka wahusika mbele ya sharia, “wale waliohusika katika shambulio hilo lisilokubalika dhidi ya demokrasia.”

Mbali na taasisi hizo, magazeti na vyombo vingine vya habari vya kielektroniki na mitandao duniani, viliripoti habari za shambulio hilo, baadhi vikihusisha suala la kisiasa na vingine vikihusisha na kesi zake alizofunguliwa hivi karibuni.

Kwa upande wake, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) imesema tukio hilo ambalo limetokea siku chache baada ya ofisi za wanasheria wa kampuni ya Immma mjini Dar es Salaam kushambuliwa, limejenga hofu siyo kwa familia ya Lissu pekee, bali kwa wananchi wengi.

“Isitoshe, matukio haya hayaleti picha nzuri kwa nchi inayoheshimu demokrasia, haki za binadamu na utawala bora. Ni shambulio linalotia hofu katika jamii.

Hivyo, tume inalitaka Jeshi la Polisi kuhakikisha linakamilisha haraka upelelezi wa tukio hilo na kuwapeleka wahusika katika vyombo vya sheria,” inasema sehemu ya taarifa ya tume hiyo iliyosainiwa na Mwenyekiti wake, Bahame Nyanduga.

Amnesty International
Mbali ya kulaani tukio hilo, shirika la kimataifa la kutetea haki za binadamu la ‘Amnesty International’ limeungana na watu wengine kuzitaka mamlaka zinazohusika kuithibitishia dunia kuwa shambulio hilo halikuwa na sura ya kisiasa.

Naibu Mkurugenzi wa ‘Amnesty’ wa kanda ya Afrika Mashariki na Maziwa Makuu, Sarah Jackson alisema kushambuliwa kwa Lissu si tu kunatuma ujumbe wa kutaka kuwatisha watetezi wa haki za binadamu, bali pia kunaacha maswali mengi.

“Hili shambulio la kikatili dhidi ya mwanasiasa ambaye aliyeweka nyuma woga, linatia wasiwasi wa hatima ya watu wanaojitoa kwa ajili ya kutetea haki za binadamu.”

“Mamlaka zinazohusika zinapaswa kuwajibika kwa kuueleza ulimwengu kuwa mashambulizi haya hayakufanywa kwa misingi ya kisiasa,” alisema Jackson.

Ndugai aeleza Lissu alivyojeruhiwa
Kuhusu shambulio hilo, Spika Ndugai alisema Lissu alishambuliwa kwa risasi kati ya 28 na 32, huku tano zikimpata na kumjeruhi mwilini.

Akitoa taarifa ya tukio hilo bungeni mjini Dodoma Ijumaa, 8/9/17, Ndugai alisema risasi mbili zilimpata kwenye miguu, mbili tumboni na moja mkononi.

Alisema watu wasiofahamika wakiwa kwenye gari aina ya Nissan, walimpiga risasi kisha kutoweka: “Baada ya tukio hilo watu hao walikimbia,” alisema Ndugai.

Ndugai alisema Lissu alipelekwa Hospitali ya Rufaa ya Dodoma kwa kutumia gari la familia ya Naibu Spika, Dk Tulia Ackson kwa kuwa wanaishi jirani.

Alisema ofisi ya bunge kwa kushirikiana na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) waliandaa ndege saa 10:30 jioni kwa ajili ya kumpeleka Hospitali ya Muhimbili kwa ajili ya matibabu zaidi.

Hata hivyo, baada ya kushauriana na familia na Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe waliona ni  vyema apelekwe  Hospitali ya Aga Khan, Nairobi.

“Hivyo kwa kushirikiana na Ofisi ya Bunge ilipatikana ndege nyingine ya flying doctors (madaktari wanaofanya kazi popote) na kuondoka na mgonjwa saa 6:00 usiku kuelekea Nairobi,” alifafanua Ndugai.

Spika alisema kuwa tukio hilo liliripotiwa polisi ambao waliahidi kufanya msako kuwatafuta watu hao na kwamba serikali itatoa taarifa kamili kwa kuzingatia utaratibu wa kibunge.

Aliongeza kuwa tukio hilo ni la kwanza la aina yake tangu Bunge lilipohamia Dodoma na kwamba haijawahi kutokea mbunge akashambuliwa kwa risasi.

Alisema ingekuwa mbunge huyo anatakiwa kusafirishwa nje ya nchi, serikali ina mkataba na Hospitali ya Apollo ya India na kuwa, Lissu alipelekwa Nairobi kwa sababu familia yake iliomba.

“Kwa nini mwenzetu alipelekwa Nairobi, ni kwa sababu familia iliomba. Nimnukuu mheshimiwa Mbowe kwa niaba yake si kwamba wana shaka na umahiri na uwezo wa madaktari wetu,” alisema  Ndugai.

Pia, aliwataka Watanzania kuendelea kumuombea kiongozi huyo katika kipindi hichi kigumu na kuwawashauri wabunge walioanza kutuma ujumbe kwenye mitandao ya kijamii kutumia maneno ya hekima badala ya kuendelea kuzichonganisha pande mbili.

Wabunge wajawa hofu
Wakizungumzia tukio hilo, wabunge wamevitaka vyombo vya ulinzi na usalama kuchukua hatua kuhakikisha kuwa matukio ya aina hiyo yanadhibitiwa.

Mbunge wa viti maalumu (CCM), Ritta Kabati alisema malalamiko yamekuwa mengi na ndio maana bunge limeona kuna umuhimu wa Kamati ya Bunge ya Ulinzi na Usalama kukaa na vyombo vya usalama kujua sababu za matukio yasiyoeleweka.

“Mtu kavamiwa unasikia kuwa wanafanya upelelezi halafu baadaye hatupati mwisho wake ni nini?. Alihoji Kabati na kueleza: “Tukio la Lissu linasikitisha sana. Tukio hili limetuchanganya akili, kumbe hatuko salama kabisa.”

Alisema: “Limetokea katika jengo la mawaziri, naibu spika na wabunge. Huwa tunaamini kuna maaskari (maeneo hayo), lakini nao wamepitwa.”

Mbunge wa Mtwara Mjini (CUF), Maftaha Nachuma alisema tukio hilo limemsikitisha hasa ikizingatia kuwa Dodoma ni makao makuu ya nchi na kwa hiyo serikali yote iko hapo na bunge linaendelea na vikao vyake, lakini mbunge alipigwa risasi na watu hawajulikani.

“Kimsingi ni jambo ambalo linatia simanzi sana hasa upande wetu  kama wabunge kwa sababu leo ni kwa Tundu Lissu, kesho mimi keshokutwa kwa mwingine hatuwezi kujua,” alisema Nachuma.

Mbunge wa Chalinze (CCM), Ridhiwani Kikwete alisema mshtuko mkubwa alioupata ni kwa sababu katika jamii alitegemea mbunge angekuwa mtu salama zaidi, lakini anashambuliwa na kuhoji kuwa usalama wa wananchi mitaani ukoje.

“Lakini pili niuombe sana umma katika kipindi hiki kizito wawe watulivu kwa sababu haya mambo yanapotokea yanaweza kuwa na sura nyingi na tafsiri nyingi,” alisema Kikwete ‘Junior’.

“Lakini tuviamini vyombo vyetu vitatuletea majibu sahihi ambayo yatatoa  mwanga jinsi gani limetokea, ukweli na kuona tunatokaje kuanzia hapa.”

Mbunge wa Mtama (CCM) Nape Nnauye alisema Lissu ni miongoni mwa wabunge waliolalamika kufuatiliwa na magari na hadi akataja namba, rangi na idadi ya watu waliokuwa wakimfuatilia, lakini kinachomsikitisha hakuona kama jambo hilo lilipuuzwa: “Sasa Bunge limepeleka katika kamati, ninaamini baada ya pale hatua zitachukuliwa.”

“Tusipokomesha, jambo hili linajenga chuki kati ya Watanzania na serikali yao, kati ya Watanzania na chama kilichounda Serikali, lakini linapeleka sura mbaya duniani.”

Mbowe awatoa hofu wananchi
Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe alisema Lissu ni mzima, lakini hayuko katika hali nzuri. Kauli hii ni baada ya kufika Nairobi.

Mbowe alisema hafikirii kama wahuni ndiyo waliofanya shambulio hilo kwa kuwa Lissu hana maadui nje ya siasa.

“Tunashuku kuna msukumo wa kisiasa katika shambulio hili, ikizingatiwa silaha nzito iliyotumika na idadi ya risasi zilizofyatuliwa. Ni wazi wahusika walikuwa na nia ya kumuua na sio kumuibia au kuchukua chochote kutoka kwake,” alisema Mbowe.

Hata hivyo, kiongozi huyo alisema katu wanachama wa chama chake hawataogopa kupaza sauti na wataendelea kupambana kuhakikisha demokrasia inasimama imara.

Vyombo vya habari vya kimataifa
Baadhi ya magazeti yaliyoripoti tukio hilo la Lissu ni Independent Times la Uganda, Daily Nation la Kenya, New York Times la Marekani na Mashirika mbalimbali ya habari pamoja na Mitandao ya Kijamii ndani na nje ya Tanzania.

 

Share: